September 12, 2023

Benki ya Exim, TIRA watangaza ushirikiano uendeshaji wa Akaunti ya Dhamana

Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim, Jaffari Matundu (kulia) na Mkurugenzi wa Usimami wa Soko wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Abubakar Ndwata wakionyesha bango kuashiria uzinduzi wa Akaunti ya Dhamana (Trust Account) ulioenda sambamba na warsha iliyoandaliwa na benki ya Exim jijini Dar es Salaam  jana kwa wadau  wa sekta ya bima nchini.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim, Jaffari Matundu akitoa hotuba fupi wakati wa uzinduzi wa Akaunti ya Dhamana (Trust Account) ulioenda sambamba na warsha iliyoandaliwa na benki ya Exim jijini Dar es Salaam  jana kwa wadau  wa sekta ya bima nchini.

Baadhi ya viongozi wa ngazi za juu kutoka Benki ya Exim na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) katika picha ya pamoja mara baada ya uzinduzi wa Akaunti ya Dhamana (Trust Account) ulioenda sambamba na warsha iliyoandaliwa na benki ya Exim jijini Dar es Salaam  jana kwa wadau  wa sekta ya bima nchini. Katikati ni Mkurugenzi wa Usimami wa Soko wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Abubakar Ndwata na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim, Jaffari Matundu (wa pili kulia).

 

Na Mwandishi Wetu

 

Benki ya Exim imetangaza ushirikiano wake na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) unaolenga katika kutekeleza Akaunti ya Dhamana (Trust Account) kwa makampuni ya bima nchini.

 

Hatua hiyo inayolenga kutimiza matakwa ya kisheria na kanuni zilizowekwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) inasisitiza dhamira ya benki hiyo katika kuchochea ukuaji wa sekta ya bima hapa nchini Tanzania.

 

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Akaunti ya Dhamana iliyokwenda sambamba na warsha iliyoandaliwa na benki ya Exim iliyowakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya bima wakiwemo TIRA, na makampuni ya bima, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim, Jaffari Matundu, aliipongeza TIRA kwa kuipatia benki yake  fursa ya kushiriki katika uanzishwaji wa Akaunti ya Dhamana (Trust Account).

 

"Katika Benki ya Exim tunaamini kuwa sekta ya bima ni chachu katika kuchangia maendeleo kwenye sekta ya kifedha na kiuchumi. Tunafurahi kwa fursa hii ya kushiriki katika uanzishwaji wa Akaunti ya Dhamana ya Bima na tunaamini kwa dhati kuwa hatua hii italeta uwazi na uwajibikaji katika sekta ya bima,” alisema.

 

Matundu alisema benki hiyo kwa miaka mingi imekuwa ikifanya kazi na kampuni kadhaa za bima nchini kutoa huduma maalum na kuongeza kuwa benki hiyo itaendelea kushirikiana na wadau wote kusaidia na kuchangia ukuaji wa sekta hiyo.

 

"Kama sehemu ya dhamira yetu ya kuongeza kasi ya uchukuaji wa bima, Benki ya Exim iliianzisha bidhaa ya mkopo wa bima maarufu kama Insurance Premium Finance (IPF) ambao inamwezesha mtu kukopa bima bila dhamana yoyote na kuilipa badae ili kujikinga dhidi ya majanga. Kupitia Insurance Premium Finance (IPF) tunafadhili malipo yako kamili kwa kampuni ya Bima na kukupa uhuru wa kueneza ulipaji wa malipo huku ukiwa na uhuru wa kutumia pesa zako kwa fursa zingine za biashara,” alisema.

 

Naye Mkurugenzi wa Usimami wa Soko wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Abubakar Ndwata wakati wa hafla hiyo alisema kuwa uanzishwaji wa akaunti hiyo ya dhamana ya bima ni hatua nzuri ambayo itasaidia kuimarisha usimamizi wa sekta ya bima kuendana na matakwa ya kisheria na udhibiti yaliyowekwa na Mamlaka ya Uismamizi wa Bima.

 

“Nachukua fursa hii kuipongeza Benki ya Exim kwa kuwa benki ya nne katika sekta ya benki nchini Tanzania kutekeleza mchakato wa kuanzisha Akaunti ya Dhamana. Hii ni hatua nzuri ambayo itasaidia kuimarisha usimamizi wa sekta ya bima kwa kuzingatia matakwa ya kisheria na kikanuni yaliyowekwa na TIRA,” alisema.

 

Ndwata alisema chimbuko la akaunti hiyo ya dhamana ya Bima ni Kanuni ya Bima ya mwaka 2009 kifungu namba 20 inayozitaka kampuni za Bima kuweka amana za usalama angalau asilimia 50 ya kiwango cha chini cha mtaji halisi wa kampuni husika ya bima

Aliongeza kuwa utaratibu uliokuwa ukitumika mwanzoni katika usimamizi wa dhamana ya bima haukuwa mzuri jambo ambalo lilipelekea Mamlaka kushindwa kusimamia vizuri amana hizo pindi ziliporejeshwa kwa makampuni kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT) baada ya kuiva.

 

Alisema kuwa awali kampuni nyingi za bima zilikuwa zikitumia fedha za amana ya Akiba katika matumizi mengine, pasipo kupata idhini ya TIRA hivyo kupelekea kuingia katika changamoto ya ukwasi, na wakati mwingine kushindwa kulipa fidia kwa wateja kutokana na fedha kuwekezwa katika miradi mingine.

 

No comments:

Post a Comment

Pages