September 01, 2023

JESHI LA POLISI LAPEWA MSAADA WA GARI

Mwakilishi wa kampuni ya Mufindi Wood Poles Plant and Timber Limited, Awadhi Nyagongo akikabidhi funguo kwa Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa ,Acp, Allan Bukumbi.
Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa ACP Allan Bukumbi akikata utepe kuzindua rasmi matumizi ya gari walilokabidhiwa.
  Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa ACP Allan Bukumbi akielezea kwa wanahabari magari yaliyokarabatiwa.
 Mwakilishi wa kampuni ya Mufindi Wood Poles Plant and Timber Limited, Awadhi Nyagongo, akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada wa gari kwa niaba ya Kampuni. ( Picha zote na Denis Mlowe).


NA DENIS MLOWE, IRINGA


JESHI la Polisi Mkoa wa Iringa limepatiwa msaada wa gari Moja aina ya Toyota Premio kutoka kampuni ya Mufindi Wood Poles Plant and Timber Limited na pikipiki Moja aina ya boxer iliyotolewa na kampuni ya Udzungwa Corridor kupitia dhana ya ushirikishwaji jamii.

Gari Hilo lenye thamani ya milioni 19 na pikipiki hiyo yenye thamani ya milioni 3.1 limekabidhiwa kwa Kamanda wa  Polisi Mkoa wa Iringa, ACP Allan Bukumbi ikiwa ni ushirikiano mzuri uliopo baina ya jeshi la Polisi na wadau mbalimbali.

Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo licha ya kuzishukuru kampuni hizo ACP, Bukumbi alisema kuwa dhana ya ushirikishwaji kwa jamii imeonyesha ushirikiano mzuri hali ambayo imeleta matunda kuweza kupata msaada huo.

Alisema kuwa katika kuendeleza na kuimarisha doria na kupambana na uhalifu watahakikisha vitendea kazi hivyo yakiwemo magari vinaendelea kuwa katika ubora. 

Aidha alisema kuwa jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limefanya matengenezo ya magari 12 ambapo yamegharimu sh. 28.6 

Alisema kuwa fedha za matengenezo hayo imepatikana kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wa jeshi Hilo mkoani hapa ikiwemo kampuni ya Asas Group of Companies, Ivori na Toyota Tanzania ltd

Aliongeza kuwa yatatumika katika kuzuia na kupambana na uhalifu ikiwemo udhibiti wa doria za barabarani ili kuzuia ajali zinazosababishwa na madereva wasiotii Sheria.

"Kwa niaba ya Mkuu wa jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa tunatoa shukrani za dhati kwa wadau wote waliojitolea na wengine wenye moyo huo wajitokeze ili kuongeza ushirikiano na kuifanya jamii ya wananchi wa Iringa kuwa salama"Alisema 

Kwa upande wake Mwakilishi wa kampuni ya Mufindi Wood Poles Plant and Timber Limited, Awadhi Nyagongo alisema kuwa wametoa msaada huo baada ya kuguswa na utendaji wa kazi wa jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa katika harakati za kupambana na uhalifu.

Alisema nyenzo hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa doria kwa jeshi la Polisi kutokana na juhudi ambazo wamekuwa wakizifanya katika kudhibiti na kupambana na uhalifu mkoani hapa.


No comments:

Post a Comment

Pages