September 01, 2023

SERIKALI YARIDHISHWA NA UKUAJI SEKTA YA MADINI - MAJALIWA

 *Asema Serikali itaendelea kuhamasisha biashara na uwekezaji katika sekta hiyo

 

Na Mwandishi Wetu

 

SEKTA ya madini ni miongoni mwa sekta zinazokua kwa kasi hapa nchini, hivyo Serikali imeendelea kuhakikisha uwekezaji katika Sekta ya Madini unaongezeka ili iweze kuchangia ipasavyo katika ukuaji wa uchumi.

Takwimu zinaonyesha kuwa kwa sasa kasi ya ukuaji wa shughuli za uchimbaji wa madini ni asilimia 9.6, kutokana na kasi hiyo ya ukuaji, sekta ya madini inashika nafasi ya tatu ikitanguliwa na sekta za sanaa na burudani pamoja na ile ya umeme.

Agosti 26 mwaka huu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alifunga Maonesho ya Madini na fursa za Uwekezaji mkoani Lindi yaliyofanyika kwenye viwanja vya soko la Kilimahewa wilayani Ruangwa, ambapo pamoja na mambo mengine alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha uwepo wa mazingira bora kwa wawekezaji wa ndani na nje.

Alisema kutokana na umuhimu wa sekta hiyo Serikali itaendelea kuhamasisha biashara na uwekezaji katika sekta ya madini, kuwaendeleza wachimbaji wadogo, kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini, kusimamia mifumo ya ukaguzi wa shughuli za migodi na kuzijengea uwezo taasisi zinazosimamia sekta hiyo. “Lengo la hatua hizi ni kuhakikisha sekta hii inachangia asilimia 10 katika Pato la Taifa ifikapo mwaka 2025.”

Waziri Mkuu alisema Serikali itaendelea kuwaendeleza wachimbaji wadogo ambapo kupitia taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST)  Serikali ilitoa mafunzo ya uchukuaji wa sampuli kwa ajili ya uchimbaji na uchenjuaji wa madini na namna bora ya kufanya tafiti kwa wachimbaji wadogo zaidi ya 2,200. Mkoa wa Lindi ni mmoja wa Mikoa iliyonufaika kwa mafunzo hayo.

 “Vilevile, Serikali itaendelea kuhakikisha uwepo wa mazingira bora kwa wawekezaji wa ndani na nje kwa kuendelea kutatua changamoto, kero na adha zilizokuwa zikiwakabili wawekezaji na wachimbaji wa madini. Pia, itaendelea kuhakikisha wachimbaji wadogo wanapata soko la uhakika la kuuza madini, pamoja na kuinua mitaji yao kwa mikopo yenye gharama nafuu.”

Pia, Waziri Mkuu aliziagiza Halmashauri zote zenye maeneo ya migodi ziweke mpango madhubuti wa kuhakikisha uchimbaji endelevu unaozingatia utunzaji na uhifadhi wa mazingira sambamba na kutoa elimu kwa umma kuhusu namna nzuri ya utunzaji wa mazingira hayo.

”Halmashauri zote zihakikishe zinatoa ushirikiano wa kutosha kwa wawekezaji waliobaini fursa ndani ya  maeneo yao. Uandaliwe mkakati rahisi na endelevu wa kuwezesha upatikanaji wa taarifa za fursa mbalimbali zilizopatikana kupitia maonesho haya."

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alitoa onyo kwa maafisa wanaohusika na utoaji wa leseni za madini kuacha tabia ya kuwazunguka wananchi wanaokwenda katika ofisi zao kuomba leseni za uchimbaji baada ya kubaini uwepo wa madini kwenye baadhi ya maeneo na kisha kuwapa wachimbaji wengine.

”…Acheni tabia ya kuwaonea wananchi wanaotoka kwenye maeneo yenye fursa ya madini anakuja kuomba leseni ya kumiliki eneo hilo na unamwambia aache taarifa zake aje kesho kuchukua majibu akija kesho unamwambia eneo hilo limeshachukuliwa na mtu mwingine kumbe wewe unamtafuta mtu wa kuweza kumiliki ili upate chochote kitu, tukikugundua hatua kali zitachukuliwa dhidi yako. ”

Pia, Mheshimiwa Majaliwa aliuagiza uongozi wa Wakala wa Jiolojia Tanzania ufanye tafiti za madini za kimkakati kwa kushirikiana na halmashauri kwa lengo la kuwasaidia Watanzania kufanya shughuli zao kwa tija na kuhakikisha mipango sahihi ya matumizi ya ardhi inafikiwa.

Aidha, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wachimbaji wote wa madini waweke kipaumbele katika kuyaongezea thamani madini hayo na kuzitumia taasisi za madini ili kufanya shughuli zao kwa tija, uhakika na faida zaidi.

Waziri Mkuu aliongeza kuwa Serikali inatambua uwepo wa fursa na rasilimali hizo na ndiyo maana inaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati kwa lengo la kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji katika maeneo mbalimbali nchini pamoja na mkoa wa Lindi.

“Sote tu mashuhuda kuhusu miradi ya Viwanja vya Ndege, Bandari na barabara inayoendelea kutekelezwa katika Mkoa wa Lindi na ukanda wa kusini. Barabara hizo ni kiungo muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa mkoa huu. Niwahakikishie wananchi wa Mkoa wa Lindi hiyo ndio azma ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha maendeleo ya wananchi wa Mkoa ya Lindi  yanapatikana kwa haraka.”

“Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitomshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuufungua zaidi Mkoa wa Lindi na Tanzania kwa Ujumla. Dhamira yake njema ya kuwaletea maendeleo ya haraka Watanzania inaonekana kwa vitendo, hivyo nitoe wito kwetu sote tuendelee kumuunga mkono na tumwombee kwa Mwenyezi Mungu ili amjalie nguvu na afya katika kuliongoza Taifa letu.”

Kwa upande wake, Rais Mstaafu wa awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya Kikwete alitumia fursa hiyo kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa maono yake mazuri ya kutengeneza mazingira ya kuvutia wawekezaji. ”Ndugu zangu tusijidanganye hakuna maendeleo bila ya uwekezaji.”

Alisema uwekezaji unatoa fursa mbalimbali zinazochangia katika kuchochea maendeleo na kukuza uchumi wa Taifa na wananchi kwa ujumla kwa kutoa ajira nyingi, hivyo aliwasisitiza wana-Lindi waendelee kutoa ushirikiano kwa wawekezaji.

Pia, Mheshimiwa Kikwete alitoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Lindi waendelee kulinda rasilimali mbalimbali ikiwemo ardhi. ”Zindukeni, jitahidini kuhifadhi rasilimali zenu, tumieni fursa ya kuwekeza au kuingia ubia na wawekezaji. Utauza ekari moja kwa shilingi laki moja leo baada ya miaka mitano mtu anaiuza kwa shilingi milioni 100.”

Naye, Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko alisema ukuaji wa sekta ya madini umeongezeka nchini kutoka asilimia 9.4 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 10.9 mwaka 2022, pia mchango wa sekta hiyo katika pato la Taifa nao umeongezeka kutoka asilimia 7.3 mwaka 2021 hadi asilimia 9.1 mwaka 2022.

Alisema mwenendo umeleta matumaini kwamba sekta ya madini itaweza kuchangia asilimia 10 au zaidi kwenye pato la Taifa ifikapo mwaka 2025, hivyo aliupongeza uongozi wa mkoa wa Lindi kwa kuandaa maonesho hayo muhimu kwa ajili ya ukuaji wa uchumi wa mkoa na nchi kwa ujumla.

Dkt. Biteko alitumia fursa hiyo kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha mapinduzi makubwa yanafanyika katika sekta ya madini nchini kwa kiendeleza ikiwemo kuzilinda rasilimaliu madini, kuvutia uwekezaji katika shughuli za uchimbaji, uchenjuaji, uongezaji thamani na kuongeza ushiriki wa Serikali kwenye shughuli za madini.

Awali, akizungumzia kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mkuu wa wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga alisema alisema mkoa uliamua kufanya maonesho hayo kwa lengo la kutangaza fursa za kiuchumi walizonazo kwani kwamiaka mingi mkoa huo umekuwa ukitambuliwa kwa kilimo cha korosho na ufuta tu.

”Fursa nyingine za madini, uvuvi wa baharini, hifadhi za wanyama, ardhi ya uwekezaji na gesi hazijatangazwa kwa kiwango cha kutosha. Ni kwa muktadha huo, tukaona tuwe na maonesho haya ili tujitangaza, kuwakutanisha wadau, kujifunza, kujenga mahusiano na ushirikiano utakaoweza kuinua sekta hii ndani ya mkoa wetu.”

Alisema katika kipindi cha mwaka 2022/2023, aina ya madini yalizalishwa na kuuzwa katika mkoa wa Lindi ni dhahabu, nikeli, jasi, shaba, kinywe, chumvi, chokaa, marble, vito na madini ya ujenzi, ambapo mpaka kufikia June 30 mwaka huu walikusanya maduhuli ya Serikali kiasi cha shilingi bilioni 4.33 sawa na asilimia 90.42 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 4.8.

Aliongeza kuwa kiasi hicho ni kidogo kulingana na taarifa za kiwango cha madini kilichopo ardhini, hivyo wanahitaji uwekezaji mkubwa na wa kati wenye vifaa vya kisasa vya kuchimba na kuchenjua ili waweze kunufaika zaidi na Serikali kupata mapato mengi.

Aidha, kiongozi huyo alisema changamoto zinazowakabili katika sekta hiyo ni pamoja na wawekezaji kutoendeleza kwa wakati leseni za utafiti au uchimbaji na hivyo kushikilia maeneo hayo na kuwazuia wawekezaji wapya kupata nafasi ya kuwekeza.

 

No comments:

Post a Comment

Pages