HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 13, 2023

SMZ, Green Economic Partnership wasaini mkataba wa biashara Hewa ya Kaboni

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dkt. Omar Shajak na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Green Economic Partnership, Arthur Chirkinian wakisaini mkataba wa Makubaliano juu ya biashara ya hewa ya Kaboni baina ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na Kampuni ya Green Economic Partnership,  hafla iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mkutano Migombani.


 

Na Talib Ussi Zanzibar 


Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na Kampuni ya Green Economic Partnership ya Dubai imetiliana saini mkataba wa makubaliano juu ya biashara ya hewa ya kaboni hafla ilioyofanyika kwenye ukumbi wa mkutano wa Ofisi hiyo uliopo Migombani.

Mkataba huo ulisainiwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dkt. Omar Shajak na kwa upande wa kampuni ya Green Economic Partnership ulisainiwa na Mkurugenzi Mtendaji, Arthur Chirkinian.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya makubaliano hayo Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dkt Omar D. Shajak amesema Mkataba wa makubaliano juu ya biashara ya hewa ya kabon unalengo la kufanya utafiti na kuchunguza kwa kina kiwango halisi cha hewa ya kaboni inayopatikana Zanzibar.

Amefahamisha kuwa utafiti huo utaifanya Zanzibar kuwa na fursa ya kufanya biashara ya hewa ukaa, na mataifa makubwa ambao ndio waathirika wakubwa kulikotokana na nchi hizo kuwa na viwanda vikubwa vinavyotoa hewa chafu jambo ambalo linaathiri na kupelekea mabadiliko ya tabianchi.

Aidha mkataba huu utaiwezesha Zanzibar kufanya uchunguzi wa misitu na kujua kiwango halisi cha gesi ya kaboni iliyopo kwenye misitu, kujua thamani yake ili kuandaa masoko na upatikanaji wa wanunuzi, ambapo fedha zitakazopatikana ziwasaidie wakulima wanaojishughulisha na misitu, wananchi pamoja na Serikali kufanya shughuli nyengine za maendeleo.

Dkt Shajak amesema kuwa Zanzibar ni waathirika wakubwa wa mabadiliko ya tabianchi na kutolea mfano wa kisiwa cha Pemba ambapo zaidi ya maeneo 143 yamepata changamoto hiyo ikiwemo mashamba ya kilimo kuingia maji ya chumvi.

“Mbadala wake ni kuwa sisi tuendelee kutengeneza hali ya hewa iwe nzuri kwa kuhifadhi na kupanda miti pamoja na kuepuka kuikata ovyo ikiwemo kuhifadhi matumbawe baharini” alisema.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Sheha Juma Mjaja, amefahamisha kuwa katika makubaliano na kampuni ya Green Economic Partnership wameamua kuhifadhi miti ambayo chanzo kikuu cha hewa hiyo.

Mjaja amesema kabla ya kufanya utafiti huo watalazimika kurudi kwa wananchi ili kufahamisha dhamira njema ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar juu ya utafutaji hewa hiyo, na kuwaomba wananchi kutoa mashirikiano ili hatimae wafurahie kuendelea kupanda miti kwa wingi, kulinda na kuhifadhi.

“Wananchi tupandeni miti ya asili pia tuongeze vitalu tukiongeza na kupanda miti mingi Zanzibar itauza kabon kwa wingi ambayo inazaliwa na pato letu la taifa litaongezeka” alisisitiza Mjaja.

Kwa upande wake Meneja anaeshughulikia uchumi wa buluu Kepteni Hamad Bakari Hamad kutoka Taasisi ya Ufuatiliaji na Usimamizi Utendaji kazi Serikalini (PDB) ameongezea kuwa mkataba huo ulisainiwa tarehe 18 Agosti,2023 kwa njia ya mtandao na kilichofanyika ni uthibitisho rasmi wa kuzikutanisha pande zote mbili ili kuweka kumbukumbu kama uthibitisho wa kisheria.

Kepten Hamad amesema Serikali kupitia rasilimali ya misitu na bahari inatarajia kunufaika na uuzaji wa hewa ukaa inayotarajiwa kuzalishwa hapa Zanzibar na pindi ikianza kuzalishwa itawanufaisha wananchi wa visiwa hivi na kupeleka mbele huduma za maendeleo.

Mkurugenzi mtendaji Bw Arthur Chirkinian na wataalamu wa Kampuni ya Green Economic Partnership wapo Zanzibar ambapo watapata fursa ya kuangalia maeneo ya matumbawe na maeneo ya misitu ili kuona iwapo yanaweza kuanzisha biashara ya hewa ya Kaboni kwa Mkoa Kusini na Kaskazini Unguja na Micheweni kwa Pemba.

Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais imeanzisha kampeni maalum ya mradi wa kurithisha vizazi, Zanzibar ya kijani ambao unahamasisha kupanda miti kwa utaratibu maalum kutokana na maeneo na uoto wa asili, hivyo biashara hii ya hewa ya kaboni itaongeza zaidi ari na hamasa kwa wananchi kupanda miti ambayo faida yake ni kuongeza tija na pato la taifa litaongezeka.
Gesi ya ukaa ni hewa Maalum ambayo kitaalamu inaitwa Carbon inatokana au huvunwa kutokana na miti ya asili au misitu ya asili kama vile Jozani kwa Unguja au Ngezi kwa Pemba hewa hii huvunwa kitaalamu kwa kutumia vifaa maalum vya kisayansi.

👇🏽PICHA

CAPTION
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dkt Omar D. Shajak na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Green Economic Partnership Bw Arthur Chirkinian wametiliana Saini Mkataba wa Makubaliano juu ya biashara ya hewa ya Kaboni baina ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na Kampuni ya Green Economic Partnership,  hafla iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mkutano Migombani.

No comments:

Post a Comment

Pages