September 04, 2023

TANTRADE YATAJA BIDHAA ZILIZOPATIWA MASOKO KIMATAIFA

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Latifa Hamis, akizungumza na Wahariri na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam leo Septemba 4, 2023 kuhusu utendaji kazi wa mamlaka hiyo. 
 
Kaimu Mwenyekiti wa Jukwa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena, akizungumza katika mkutano huo.







 

Na John Marwa

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imezitaja bidhaa ambazo zimepata masoko makubwa nje ya nchi. 

 

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Latifa Hamis, katika mkutano na Wahariri na Waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.


Amesema kama nchi kuna bidhaa ambazo zimekuwa zikifanya vizuri hasa kwenye eneo la bidhaa za kilimo katika kipindi cha miaka mitano Sasa kuanzia 2018 hadi sasa 2023.

"Tunafanya vizuri sana kwenye eneo la Bidhaa za kilimo lakini bidhaa ambazo zilitafutiwa masoko katika kipindi cha miaka mitano ni bidhaa za Nyama, Mchele, Soya, Karanga, Parachichi, Pilipili, Muhogo, Mahindi, Karafuu, Asali, Mbegu za Maboga, Korosho na Zabibu.

"Bidhaa ambazo zina fursa ni Dhahabu, Korosho, Ufuta, Mbaazi, Kahawa, Dengu Almasi, Vifungashio vya mifuko na Pamba, mikakati ya utekelezaji kwa mwaka 2023/24 tutaendelea kuratibu shughuli za utafutaji masoko na ukuzaji Biashara ili kuunganisha wazalishaji kuwaambia kuna fursa gani na kuimarisha itelejensia ya Biashara.

"Lakini Nchi ambazo zinaongoza kununua bidhaa zetu ni Qatar, UAE, Omani, Kenya, Rwanda Uganda, China, India, Uholanzi, Indonesia, Norway, Afrika Kusini, Germany, Irani, Singapore, USA, Vietnam na Comoro." amesema Latifa Hamis na kuongeza kuwa.

Katika kipindi cha miaka mitano Tantrade ilipanga kukusanya billion 52 lakini tuemefanikiwa kukusanya asilimia 76 sawa na billion 40, kwaiyo hiyo ni hatua nzuri sana na kama nilivyovitaja kutokana na vyanzo mbalimbali vya mapato yetu.

"Eneo hili la mapato ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara kwa mwaka 2022, mapato yetu yana vyanzo vitatu, tuna ruzuku toka Serikalini ambapo hiyo ruzuku ndio tunalipa mishahara, tuna fedha za maendeleo ambazo tumeanza kuzipata mwaka huu 2022 ambazo hizi zinaenda kwenye miradi, miongoni mwa miradi ambayo tumeifanya ni kuvipanua viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere (sabasaba) tunaamini mabadiliko ni mengi na sisi pia tubadilike, idadi ya watu imeongezeka hivyo tunapaswa kuwa na Uwanja mkubwa zaidi.

"Vyanzo vya ndani vya mapato sisi tuna Sabasaba ambacho ni chanzo kikuu cha mapato ya ndani lakini pia tunavyo vyanzo vidogo vidogo."

Amesema kulingana na mapato yao yamekuwa wakichangia mfuko Mkuu wa Serikali kila mwaka na wataendelea kufanya hivyo.

"Tumeratibu matukio mbalimbali zikiwemo programu za utafiti, sasa hivi kuna utafiti maeneo ya mipakani tunafanya, makongamano, misafara ya kibiashara hii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, pamoja na maonesho na mikutano ya kuwaunganisha wazalishaji na wanunuzi, matukio hayo tulifanya kwenye baadhi ya nchi, Kenya, Uturuki, Comoro, Saudia Rabia, Omani na DRC Congo, ilikuwa ni muhimu sana sisi kama Tanzania kwenda huko.

"Tulienda Congo na Sudan kusini kwa sababu watanzania wanaamini huko sio sehemu salama kwa sababu ya vita lakini kuna fursa katika maeneo kama hayo na tunafanya vizuri Afrika Kusini na Malawi pia." Amesema

Nae Kaimu Mwenyekiti wa Jukwa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena, ameipongeza Tantrade huku akitoa wito kwao kutoa taarifa zao kwa wakati ili ziweze kuwafikia watanzania juu hali zozote za changamoto wanazopitia.

"Naomba TanTrade mfanye mafunzo kwa waandishi wa habari ambao wanakuja kuripoti makongamano makubwa ya Biashara kama Sabasaba tunapokuwa tunaelekea huko, isiwe kikao cha nusu siku bali yawe ni mafunzo, tunalenga nini katika maonesho ya mwaka huu, wanakuja akina nani, tuna mipango ipi. Amesema Meena.

No comments:

Post a Comment

Pages