Serikali yaendelea kutekeleza mikakati ya kuhakikisha wachimbaji wadogo wanapata fursa ya kukopeshwa magari na mitambo ili waweze kuongeza ufanisi katika kazi zao na hatimaye kuongeza vipato vyao na Taifa kwa ujumla.
Hayo yamesemwa leo tarehe 25 Septemba, 2023 na Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde alipokuwa akizindua rasmi Ofisi za Mkoa wa Geita za Kampuni ya GF Trucks and Equipments inayojihusisha kuuuza mitambo na magari kwa wachimbaji.
"Wachimbaji wadogo wanachangia asilimia 40 ya makusanyo yote yanayotokana na madini nchini. Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametuelekeza tuendelee kiwawezesha wachimbaji wadogo katika shughuli zao ili kuongeza mchango zaidi katika maendeleo ya uchumi wetu"
"Hapo zamani wachimbaji wadogo hawakuwahi kuamini kwamba mitambo ya kisasa na magari wanaweza kuyamiliki ili kuwezesha shughuli zao za uchimbaji kiufanisi, mazingira mazuri yaliyowekwa na Serikali yamewezesha wachimbaji wadogo kuendelea kunufaika na teknolojia za kisasa" alieleza Mhe. Mavunde.
Aidha, Mheshimiwa Mavunde alibainisha kwamba MoU iliyosainiwa kati ya Kampuni ya GF Trucks & Equipments na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ina lengo la kuwezesha wachimbaji wadogo kupata mitambo sahihi na magari ili kurahisisha shughuli zao za uchimbaji, ikiwa ni pamoja na kupatiwa mafunzo ya namna ya kutumia mitambo hiyo.
Pia, Mheshimiwa Mavunde alikiri kwamba hatua hiyo ya kuwezesha wachimbaji wadogo kupata magari na mitambo inaenda kuwaongezea uwezo wachimbaji wadogo wa kuzalisha madini kiufanisi na kupelekea kuongeza upatikanaji wa maduhuli ya Serikali.
Katika kuendeleza jitihada za kutatua changamoto za mitaji kwa wachimbaji wadogo, Mheshimiwa Mavunde alieleza kwamba Serikali imepanga kufanya kikao cha pamoja kati ya Mabenki na wachimbaji wadogo ili mabenki waweze kuifahamu sekta yetu ya madini vizuri na kusaidia kutoa mikopo nafuu kwa wachimbaji wadogo.
Awali, akieleza utendaji wa Taasisi mkoani Geita, Mkurugenzi wa Biashara wa Kampuni ya GF Trucks & Equipments, Bw. Salman Karmali alieleza kwamba wamefungua ofisi kuwasogezea wachimbaji wadogo huduma ya kununua magari na mitambo ya kisasa kwa bei nafuu ili warahisishe shughuli zao za kiuchimbaji.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa, Dkt. Venance Mwasse alibainisha kwamba jukumu la kuwasimamia na kuwawezesha wachimbaji wadogo ni la kwao hivyo wataendelea kuwapa mafunzo na kuwaunganisha na wadau mbalimbali ili kurahisisha shughuli zao za uchimbaji.
No comments:
Post a Comment