Na Lydia Lugakila, Misenyi
SHIRIKA la Matumaini na Maendeleo (SMMK) kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya kilimo mkoani Kagera wameiomba Serikali kuingilia kati bei ya zao la Vanilla.
Wadau hao wametoa kauli hiyo katika kikao maalum cha majumuisho kilicholenga kuwasilisha taarifa zilizofanyiwa ufuatiliaji katika eneo la mradi kwa kata 8 za Wilaya ya Misenyi zikiwemo Kanyigo, Kashenyi, Buyango, Bwanjai, Bugandika, Gera, Ishozi na Ruzinga katika mapendekezo yaliyokubaliwa katika kikao kilichofanyika mwezi Aprili, 2023 ambapo washiriki waliazimia kwamba wataalam wa utafiti waendelee kuchunguza kwa nini zao la Vanilla linakufa ambapo walishauri utafutwe mbinu mbadala ya kunusuru zao la Vanilla kuanzia bei na utunzaji.Awali akisoma taarifa ya maendeleo ya kilimo cha zao la Vanilla katika kata ya Ruzinga Mratibu msaidizi wa shirika la matumaini na Maendeleo Kanyigo Joas Rwegasira amesema kuwa zao la Vanilla ni zao muhimu sana lakini kwa mwaka 2023 limeonekana kushuka bei ghafla kutoka kilo moja 30,000 hadi 3,000 ambapo shirika hilo mimeendelea kufanya ufuatiliaji kwa Wakulima ili kujua wana mawazo yapi.
"Baada ya kuwatembelea Wakulima katika kata ya Ruzinga mnamo Septemba 22, 2023 baadhi ya Wakulima hao Felician wa Kijiji Ruhija, Pracidia wa Kijiji Mugongo na Edwin walisikitika juu ya kushuka kwa zao hilo kwani walitumia gharama kubwa ikiwemo, kulilinda likiwa shambani, kuchevusha maua kwa kutumia wafanyakazi wa mashambani, mbolea, nyasi za kutandaza shambani"alisema Joas.
Ameongeza kuwa matokeo hayo yamesababisha mkulima mmoja Wilayani humo kuvuna kilo 50 za vanilla na kukosa pa kuzipeleka hivyo kuamua kukausha kupitia wataalam walioitwa na wakulima wa vanilla Ruzinga ambapo tayari amekausha na kubaki na kilo 10 akiwa bado anaangaika na wanunuzi.
Ameongeza kuwa hadi sasa takribani wakulima 20 Wilayani Misenyi wameshauriana na kutafuta wataalam kutoka Mayawa ili wawafundishe namna ya kukausha Vanilla ambapo wamekausha na kutunza tani 1 na nusu huku wakiwa wanafanya utafiti kwa kushirikiana na Wanachama wenzao walioko jijini Dar es salaam ili wapate mashine ya kuchakata huku akiwashauri wakulima kuendelea kutunza mashamba yao vizuri.
Wadau hao akiwemo akiwemo Sevelian Katalama kutoka kata ya Ishozi alionekana kuongea kwa uchungu na masikitiko ikiwa ni baada ya kushuhudia hivi karibuni kushinda kituo cha kuuzia vanilla cha Mayawa hadi usiku bila kupata muafaka wa malipo ya mazao yao.
"Nakumbuka hata Kahawa nayo iliwahi kuwa na changamoto Kama hii hivyo kwa hali hii na mazao mengine yapo hatarini kuwa kama Vanilla hivi Wakulima tunaelekea wapi?" Alisema Sevelian.
Ameongeza kuwa kama Serikali imejitoa kwenye biashara ni vyema watu waliojitoa kununua mazao ya Wakulima iwasimamie hadi hatua ya mwisho.
Naye katibu shirika la matumaini na Maendeleo Kanyigo Sebastian Marwa James amesema kuwa kilio cha shirika hilo ni kuona Serikali inaliangalia kwa jicho la pili zao la Vanilla ili liingizwe kisera kama yalivyo mazao mengine kama Kahawa huku akiamini kuwa soko lipo sema utaratibu haujawekwa sawa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa shirika la matumaini na Maendeleo Kanyigo Samwel Bashweka amesema kuwa Serikali inatakiwa kutambua kuwa watu wake wa chini hasa Wakulima wanapata shida huku akiomba serikali kuwasaidia maafisa ugani kwa kuwawezesha vyombo vyao vya usafiri ili wapate mafuta na kuwafikia Wakulima kwa haraka ikiwa ni pamoja na kuwaogezea maafisa ugani wa kutosha hadi ngazi za Vijiji.
Akizungumzia hali hiyo Diwani wa kata ya Ruzinga Rafiu Hussein Abeid amewaomba Wananchi kutokata tamaa wala kuondoa marando ya vanilla mashambani mwao bali waendelee kustawisha hadi muafaka wa zao hilo utakapopatokana huku akiiomba Serikali kuona namna ya kuwasaidia kwa haraka Wakulima wa zao hilo.
Aidha naye Afisa kilimo Wilaya ya Misenyi Eliah Rugatiri aliwashauri Wakulima kuanza kulima na kujua kutunza, kusindika na hatimaye kuwa watumiaji hata ikiwezekana kuwauzia watu wengine ambapo ameishukuru kampuni ambayo imefikiria wataalam kupata elimu ya uzalishaji na utunzaji na hata uchakataji huku akiwashukuru baadhi ya Wakulima walioanza kutafuta mashine ya kusindika na kukausha Vanilla ili ipande thamani.
Hata hivyo kwa upande wake Mgeni rasmi katika kikao hicho Devotha Rutalemwa kwa niaba ya Afisa maendeleo ya jamii Wilaya ya Misenyi alilishukuru Shirika hilo ambalo limekuwa chachu ya maendeleo katika Wilaya hiyo huku akiwaomba wadau hao kuendelea kuwa Mabalozi wazuri ili wawaeleze ndugu zao waanzishe vikundi mbali mbali hasa vya kuweka na kukopesha fedha ili wapige hatua kubwa na kuwasihi Wakulima wa zao la Vanilla kutokata tamaa ikiwa ni pamoja na kutoishia kulima vanilla tu bali walime mazao mengine mbadala ili kujikwamua kiuchumi ili inapotokea limekwama zao A zao B liwaletee manufaa.
Ikumbukwe kuwa shirika la matumaini na Maendeleo Kanyigo ni shirika la kiraia lisilotegemea faida lilianzishwa mwaka 2016, linatekeleza mradi wa uwezeshaji wa jamii kufanya ufuatiliaji wa uwajibika jamii sekta ya kilimo katika kata 8 za Wilaya ya Misenyi ambapo tayari limeacha alama katika jamii kutokana na kufanya utetezi hadi mazao mengine ikiwemo Kahawa kupanda bei.
.jpg)


No comments:
Post a Comment