Na Shamimu Nyaki
Waziri
wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt.
Dorothy Gwajima ametoa wito kwa Vyama na Mashirikisho ya michezo vitoe
nafasi kwa Wanawake kugombea nafasi za uongozi na viwaamini kuwa
wanaweza kuongoza nafasi hizo.
Mhe. Gwajima ametoa wito huo
Oktoba 21, 2023 Jijini Dar es Salaam wakati akihitimisha Tamasha la
Michezo kwa Wanawake (Tanzanite Women Sports Festival), ambapo amesema
Tamasha hilo limekua jukwaa kuwakutanisha Wanawake kufurahia mafanikio
yao katika michezo.
"Michezo ni Afya na Uhai, ni jukumu la kila
mmoja kushiriki katika michezo. Wanawake katika siku za hivi karibuni
tumekua tukililetea heshima Taifa letu kupitia michezo ya ndani na ya
Kimataifa ikiwemo Mashindano ya CECAFA na Kombe la Dunia" amesisitiza
Mhe. Gwajima.
Awali akimkaribisha Mhe.Waziri Gwajima, Katibu Mkuu
wa Wizara hiyo Bw. Gerson Msigwa amesema. Wizara hiyo itashirikiana na
Wizara ya Maliasili na Utalii kuitangaza Tanzania kupitia michezo,
kuanzisha vituo vya Utamaduni na Michezo nchi nzima.
Katibu Mkuu
Msigwa amesisitiza kuwa wale waliovamia maeneo ya michezo wanatakiwa
waondoke wenyewe kwa kuwa Serikali imepanga kuyaendeleza maeneo hayo ili
yatumike katika michezo.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa
Baraza la Michezo Tanzania, Bi. Neema Msitha amesema lengo la Tamasha
hilo ni kuhamasisha Wanawake washiriki katika michezo pia kusherehekea
mafanikio ambayo wameyapata katika michezo.
Bi. Neema amesema
Tamasha hilo limekua na mada mbalimbali za kutoa elimu ikiwemo Uongozi
na Utawala wa Wanawake katika michezo, Mtazamo wa jamii juu ya ushiriki
wa Wanawake katika michezo pamoja na uzoefu wa mchango wa michezo katika
ukuaji na uendelezaji wa Wanawake kiuchumi.
No comments:
Post a Comment