HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 01, 2023

WAZAZI NA WALEZI WAIPONGEZA SHULE YA BOHARI KAGERA

Sehemu ya Wahitimu wa Darasa la Saba mwaka 2023 Shule ya awali na Msingi ya mchepuo wa Kiingereza Bohari iliyopo Omurushaka Kata ya Bugene Wilayani Karagwe.

Meneja wa shule ya awali na Msingi Bohari mchungaji Dioniz Karwani akizungumza katika mahafali ya kumi na moja ya shule hiyo

Mchungaji Paschal Byamungu wa Kanisa la Baptist Kiregete na Mwenyekiti wa makanisa jumuiya ndogo ya Karagwe akihubili neno la Mungu kabla ya mahafali  hayo.

 

Na Lydia Lugakila, Karagwe

Wazazi na Walezi wa Wahitimu wa Darasa la saba mwaka 2023 katika shule ya awali na Msingi ya mchepuo wa Kiingereza Bohari iliyopo Omurushaka wilayani Karagwe Mkoa wa Kagera wameupongeza uongozi wa shule hiyo  kwa namna walivyowanoa watoto hao kitaaluma na kimaadili ikiwa ni pamoja na kumjua Mwenyezi Mungu.

Wazazi hao akiwemo Johanitha Kobero, Phidel Domician Mwalimu Samwel Nanyaro wametoa pongezi hizo katika mahafali ya 11 ya darasa la saba yaliyofanyika shuleni Bohari Septemba 28,2023.

Wazazi hao kwa macho yao wamesema kuwa wameshuhudia na kujionea maajabu jinsi watoto hao walivyofahamu kwa kina cha lugha ya kiingereza, kugundua na kufahamu vipaji vyao huku wakijipa matumaini ya kufaulu kwa watoto wao katika mtihani wa Taifa walioufanya mnamo Septemba 13 hadi 14, 2023.

"Mimi naona maajabu nimewekeza ki elimu kwa Mwanangu Goodluck tangu awepo hapa shuleni nimekuwa nikiona maendeleo yake mazuri sasa nimefika shuleni katika mahafali haya nimejionea mwenyewe katika  hakika watoto wetu wameiva ki taaluma, ki maadili ikiwa ni pamoja na kwa namna wanavyoweza kujieleza mbele za Walimu wao hongera Bohari" alisema Mwalimu Samweli Nanyaro.

Naye Johanitha Kobero aliyeshuhudia mwanae Neema Kobero akipokea zawadi za vyeti mbali mbali vya ufanisi alieleza furaha yake kutokana na mtoto wake kuonyesha mabadiliko makubwa katika maendeleo yake kitaaluma na kujengeka ki nidhamu huku akiwapongeza Walimu hao.

Wazazi hao wamewapongeza Walimu hao chini ya Kanisa la Baptist Omurushaka kwa kuwafundisha maadili ya ki Mungu.

Wameongeza kuwa kutokana matunda hayo waliyoyaona katika mahafali hayo wana imani kubwa katika ufaulu wa mtihani wa Taifa walioufanya watafaulu vizuri.

Katika risala ya Wahitimu hao wametoa Shukrani kwa Walimu kwa namna walivyowapa moyo wa uvumilivu, ubunifu, kujengewa tabia ya nidhamu, na kuwa wamefanikiwa katika taaluma ambapo waliweza kuwa kati ya shule bora katika mtihani wa Taifa wa darasa la nne kwa mwaka 2020 pia kuwa miongoni mwa shule bora kimkoa katika mtihani wa utimilifu mock Mkoa Kagera 2023.

Aidha kwa upande wake mchungaji Pachal Byamungu wa Kanisa la Baptist ambaye pia ni Mwenyekiti wa makanisa jumuiya ndogo ya Karagwe wakati wa ibada kabla ya mahafali hayo aliwasisitiza wazazi kuondoa roho ya kusitasita pindi Mungu anapowaonyesha mkono wa mafanikio ya ki elimu kwa watoto wao na kuwa ni vyema kuwekeza kwa watoto wao kwa imani na matumaini.

Mchungaji Byamungu aliwapongeza wahitimu kwa safari ya kiimani huku akimpongeza meneja wa shule hiyo Mchungaji Dioniz Karwani kwa namna alivyopambana hadi kupata vijana wenye uwezo ki imani.

"Ndugu zangu tambua mtu anayesitasita katika mambo yake huwa hafanikiwi hivyo wazazi mnaoendelea kuwawezesha watoto wenu kwenda mbele  hakuna kusitasita wekezeni kweli kweli" alisema mtumishi huyo.

Aliwahimiza wahitimu hao kuondoa mawazo ya kuoa au kuolewa mapema kwani kunakatiza ndoto zao hivyo kuharibikiwa bure kile walichokivuna shuleni hapo.

Hata hivyo wahitimu hao katika nyimbo zao mbali mbali walizotumbuiza katika mahafali hayo walisikika wakieleza kuwa na matumaini ya kufaulu mtihani wa Taifa kutokana na bidii waliyoionyesha.

Hata hivyo kwa upande wake Meneja wa shule hiyo Mchungaji Dioniz Karwani ametoa pongeza na shukran kubwa kwa Wizara ya Elimu msaada wa kitaaluma, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Karagwe kwa ushauri na maelekezo, Ofisi ya Mbunge Wilaya ya Karagwe, Ofisi ya Elimu Wilaya na ukaguzi Wilaya, Mkoa kanda hadi Taifa kwa ushauri wa kina na wenye manufaa kwao na kwa jamii nzima.

No comments:

Post a Comment

Pages