March 24, 2024

ACT WAZALENDO "WALIA" NA TUME YA UCHAGUZI

Chama cha ACT Wazalendo kimeitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ijiuzulu kupisha kuundwa kwa Tume Mpya itakayopatikana kwa utaratibu wa ushindani. 



Aidha Chama hicho kimetaka mapendekezo yaliyoainishwa na Tume ya Haki Jinai yafanyiwe kazi ili kuvifanyia maboresho vyombo vya ulinzi na usalama hasa Jeshi la Polisi katika kusimamia haki za wananchi kwa weledi na usawa.



Hayo yamebainishwa leo Machi 24, 2024 na Makamu Mwenyekiti Bara wa ACT Wazalendo, Isihaka Mchinjita, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu marudio ya chaguzi zilizofanyika hivi karibuni.



Amesema chama hicho kimeguswa na kusikitishwa na mwenendo usioridhisha  wa chaguzi za marudio zilizofanyika mara sita tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani mwaka 2021. 



"Katika chaguzi zote za marudio zilizofanyika ni wazi kwamba
hakuna tofauti hata ya msingi katika kuendesha na kusimamia uchaguzi," amesema na kuongeza:



"Mfano hivi karibuni Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliitisha uchaguzi wa marudio wa Udiwani uliofanyika kwenye Kata 23 siku ya tarehe 20 Machi, 2024.

 


Chama cha ACT Wazalendo kilisimamisha wagombea kwenye Kata 6 (Chipuputa, Wilaya ya Nanyumbu; Kabwe, Wilaya ya Nkasi; Kasingirima, Manispaa ya Kigoma Ujiji; Mlanzi; Wilaya ya Kibiti, Kamwene; Wilaya ya Mlimba na Bukundi Wilaya ya Meatu).



"Kwa matokeo tuliyokusanya, licha ya hujuma mbalimbali zilizofanyika kabla ya uchaguzi, Chama cha ACT Wazalendo kilistahili kushinda kwenye Kata tatu za Kasingirima (Kigoma), Kabwe (Nkasi Kaskazini) na Chipuputa (Nanyumbu)," amesema.



Amesema kupitia chaguzi hizi za marudio wamejiridhisha kuwa licha ya kauli za kufungua ukurasa mpya wa siasa za kistaarabu kupitia falsafa ya Rais Samia Suluhu Hassan ya 4R, hali halisi kupitia chaguzi za marudio ni tofauti.



"Kutokana na hayo, tunatoa wito Serikali kupeleka muswada wa marekebisho madogo (Minimum Reforms) ya Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuvifanyia mageuzi makubwa vyombo vya haki jinai na mfumo wa uchaguzi kwa ujumla wake.



"Pia, kwa vile muundo na utaratibu mpya umepitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano kupitia Muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi, Tume ya sasa ijiuzulu yote kupisha kuundwa kwa Tume Mpya itakayopatikana kwa utaratibu
wa ushindani," amesema.



Ameongeza kuwa ni muda muafaka kwa NEC kuwa na watumishi wake hadi  katika ngazi ya Halmashauri ili uchaguzi usisimamiwe na Watumishi wa  Halmashauri ambao wengi ni Makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM).



Pia ameitaka Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu ijipambanue kwa vitendo kwenye kusimamia demokrasia kwani chaguzi hizi za marudio zinaonesha kukosekana kwa nia ya dhati na ni dalili mbaya kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.



"Utaratibu wa uzalishaji, uhifadhi na usambazaji wa karatasi za kupigia kura  unahitaji kuangaliwa upya ikiwemo kushirikisha vyama vya siasa na wadau wengine kwenye kila hatua.



"Uamuzi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliopitishwa tarehe 2 Februari 2024 wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kusimamiwa na Tume Huru ya Uchaguzi badala ya TAMISEMI uheshimiwe," amesema.

No comments:

Post a Comment

Pages