March 23, 2024

TANZANIA YAWAFUNDISHA WANAMIBIA MASUALA YA HALI YA HEWA

Na Mwandishi Wetu, Windhoek, Namibia

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imewafundisha watumishi wa Taasisi ya Hali ya Hewa nchini Namibia kuhakiki weledi wa wafanyakazi wao wanaotoa huduma za hali ya hewa katika viwanja vya ndege vya nchi hiyo.

Mafunzo hayo yalifanyika katika ofisi za Hali ya Hewa Namibia kuanzia Machi 04 hadi 18, 2024 jijini Windhoek, Namibia.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Balozi wa Tanzania nchini Namibia, Caesar Waitara aliishukuru Mamlaka ya Hali ya Hewa Namibia kwa kuichagua TMA kuendesha mafunzo hayo pamoja na uwepo wa taasisi nyingi za hali ya hewa barani Afrika.

 Aidha, alizitaka taasisi zote mbili kuongeza ushirikiano zaidi katika masuala mbalimbali kwa lengo la kunyanyua uchumi na maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika.

“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya hali ya hewa nchini kwetu ikiwemo kufunga miundombinu ya kisasa ya hali ya hewa, mafunzo kwa watumishi kuzingatia vigezo vya kitaifa, kimataifa na kuweka mifumo wezeshi ya usambazaji wa taarifa za hali ya hewa kwa urahisi kwa watumiaji.

"...Licha ya kusambaza taarifa hizo na kuimarisha mifumo ya uhakiki wa ubora wa huduma (QMS) na weledi wa wafanyakazi," amesema Balozi Waitara.

Amesema Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi za mwanzoni kabisa kufanikisha kupata cheti cha ubora wa kimatiafa cha “ISO 9001:2015” katika utoaji wa huduma za hali ya hewa katika sekta ya usafiri wa anga.

Kupitia mafanikio hayo, TMA imesaidia nchi zingine zikiwemo Nigeria, Libya, Saudi Arabia, Maldives na Lesotho katika masuala uanzishaji na utekelezaji wa mifumo ya utoaji huduma bora za hali ya hewa katika viwango vinavyotambulika kimataifa.

Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Hali ya Hewa Namibia, Elias Aiyambo, aliishukuru serikali yake kwa kukubali maombi ya kufanya mafunzo hayo muhimu kwa nchi, vilevile aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanikisha mafunzo na kuomba ushirikiano huo uendelee baina ya nchi hizi mbili.


No comments:

Post a Comment

Pages