March 19, 2024

TFS yavunja rekodi za mafanikio Miaka Mitatu ya Rais Samia

Kamishina Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Prof. Dos Santos, akielezea mafanikio ya TFS katika kipindi cha cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita, kwenye mkutano wa kikao kazi baina ya TFS na Wahariri wa vyomba vya Habari, kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) na kufanyika jijini Dar es Salaam.



Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Salim Said Salim akizungumza wakati wa mkutano huo.
Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo.


Afisa Mwandamizi wa Habari na Mawasiliano kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR), Sabato Kosuri, akifafanua jambo wakati wa Kikao kazi baina ya TFS na Wahariri.



Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo, akipeana mkono na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TEF, Salim Said Salim, baada ya kutoa hotuba yake.

 


NA MWANDISHI WETU, DAR

WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), umeipongeza Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa iliyofanya katika miaka mitatu madarakani ya kuboresha Sekta ya Maliasili na Utalii, huku ikiweka rekodi ya mafanikio makubwa katika maeneo 12.

TFS ambayo kisheria ndio msimamizi wa utekelezaji wa Sheria ya Misitu na Nyuki na Mkusanyaji wa Maduhuli yatokanayo na Mazao ya Misitu, imesema katika kipindi hicho imekusanya mapato ya jumla ya Sh. Bil. 371.9 na kutoa gawio la Sh. Bil. 62 Serikalini.

Mafanikio hayo yametajwa na Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo, alipokuwa akizungumza na Wahariri wa Vyombo vya Habari wanachama wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), katika mkutano wake ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Akizungumza katika mkutano huo, Prof. Santos Silayo ameyataja maeneo 12 ambayo TFS imepata mafanikio, ambayo ni Usimamizi wa Rasilimali Watu, Usimamizi wa Rasilimali za Misitu na Usimamizi na Uendelezaji wa Mashamba ya Miti ya Serikali.

“Maeneo mengine ambayo TFS imefanikiwa sana katika miaka mitatu ya Rais Samia ni pamoja na Kuendeleza Utalii wa Ikolojia na Utamaduni, Ufugaji wa Nyuki, Ukusanyaji Maduhuli na Gawio kwa Serikali na Maendeleo ya Biashara.

“Pia tumepata mafanikio katika Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo, Kuimarisha Mazingira ya Kazi, Ushirikishaji wa Wadau (katika uhifadhi, utalii na elimu kwa umma), Huduma kwa Jamii na Utekelezaji wa Miradi ya Kimkakati ya Taifa,” alibainisha Prof. Santos.

Akifafanua mafaniko ya maeneo machache kati ya hayo, Prof. Santos Silayo alisema katika Usimamizi wa Rasilimali Watu, TFS imefanikiwa kusimamia rasilimali watu 2,097, kati yao maafisa ni 643 na askari 1,454, huku ikiajiri watumishi wapya 495.

“Katika kipindi hiki, TFS imenunua vyombo mbalimbali vya usafiri na mitambo – yakiwemo magari 113, pikipiki 164, mitambo 17 kwa gharama za Sh. Bil. 18, huku tukijenga majengo 88 zikiwemo ofisi, nyumba, vituo vya ulinzi, maghala ya silaha na mifumo ya TEHAMA.

“Katika kuendeleza Utalii wa Ikolojia na Utamaduni, TFS imefaidika moja kwa moja na ubunifu wa Rais Samia kuandaa Filamu ya The Royal Tour iliyoitangaza vema Tanzania kimataifa na kuongeza idadi ya Watalii na kukuza mapato yetu,” alisema Prof. Santos.

 Akafafanua kuwa, juhudi hizo ziliongeza Idadi ya Watalii wanaotembelea Vivutio vya Ikolojia na Utamaduni kutoka 59,606 mwaka 2020/2021 hadi kufikia 242,824 mwaka 2022/2023 na kukuza pato lao kutoka Sh. Milioni 154.9 hadi Sh. Bil. 1.5 kwa kipindi hicho.

“Hayo ni mafanikio makubwa zaidi kuwahi kufikiwa na TFS katika Sekta ya Utalii wa Ikolojia kuliko wakati wowote mwingine. Tumejipanga kuongeza idadi yao na kufikia watalii 500,000 ifikapo mwaka 2025 na kukusanya Sh. Bil. 3 katika eneo hilo tu,” aliongeza.

Katika ushiriki wa TFS kwenye miradi ya kimkakati ya Taifa, Prof. Santos Silayo aliitaja baadhi kuwa ni Mkakati wa Kuibadili Dodoma kuwa ya kijani na kusafisha eneo la Mradi wa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) kwa kushirikiana na JWTZ.

Kwa upande wake, Mwanahabari mkongwe kutoka Zanzibar, Salim Said Salim, aliishukuru TFS kwa mkutano huo ulioakisi mafanikio makubwa ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania na kuahidi ushirikiano endelevu katika kutunza na kuhifadhi misitu.

“Wanahabari tunaahidi ushirikiano wa pamoja na mamlaka hii katika kulinda misitu na kuheshimu sheria zinalinda ikolojia, wito wetu kwa TFS ni kwamba isione tabu kupokea simu za wanahabari na kuzipa ushirikiano na majibu katika maswali yao.

“Kuhusu janga la ukataji miti hovyo, nashauri mamlaka kutunga sheria kali za kuzuia uingizaji wa mashine za kukata miti, sheria ambayo kwa Zanzibar imefanikiwa.

“Kule Zanzibar hizi mashine zimezuiwa kuingizwa na zilizopo ziko chini ya mamlaka na ambazo mtumiaji wa kawaida ataziomba na kurejesha kwa kibali cha matumizi,” alisema Salim katika mkutano huo.
 

 

No comments:

Post a Comment

Pages