March 24, 2024

Tume ya Tehama yapongezwa bungeni



Na Mwandishi Wetu


KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeipongeza Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa usimamizi mzuri wa Taasisi zilizo chini yake ikiwemo Tume ya Tehama (ICTC) kutokana na kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato. 

Mbali ya ICTC inayoongozwa na Dkt. Nkundwe Mwasaga, nyingine zilizofanya vizuri kwa zaidi ya asilimia 85 ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).


Pongezi hizo zimetolewa baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kupokea taarifa ya utekelezaji wa mipango na bajeti ya wizara kwa mwaka wa fedha 2023/24 na makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka wa fedha 2024/25 iliyowasilishwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nnauye.  

  
Akitoa salamu hizo za pongezi kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Ally Jumbe Mlaghila, Mbunge wa Kyela alimpongeza Waziri Nape kwa uongozi wake makini na ubunifu wake wa kutafuta fedha na kujituma. 


“Unafanya kazi nzuri sana katika wizara hii ngeni, lakini inayopata mafanikio ya kasi kubwa sana…mnachapa kazi.


“Pongezi nyingi pia kwa taasisi zilizofanya makusanyo vizuri Kamati inazipongeza na tunaomba muendelee kufanya juhudi na zile mbinu ambazo mmezitumia kukusanya hebu endelezeni ili mkusanye zaidi, lakini wale ambao hawakufikia malengo pia tunawahamasisha wafanye vizuri…,” alisema Mlaghai.


Kamati pia imeielekeza Serikali kuhakikisha taasisi zinatekeleza na kukamilisha miradi yake kwa wakati.


Kwa upande wa Tume ya Tehama, katika mwaka huu wa fedha inatekeleza miradi kadhaa ukiwamo wa kuendeleza ubunifu na utengenezaji wa vifaa vya Tehama, Kuendelea na uanzishwaji wa vituo vya kuendeleza bunifu za TEHAMA (Soft centers) vya kikanda katika mikoa 8 pamoja na Zanzibar, na pia inaendelea na ukarabati wa kituo kikuu cha kukuza bunifu za TEHAMA kilichopo Upanga, Dar es Salaam.


Pia inaelekeza nguvu katika kuanzisha kituo cha kutengeneza na kuboresha vifaa vya Tehama (ICT Refurbishment and Assembly centre), kuwezesha uanzishaji wa vituo vya majaribio vya ubunifu TEHAMA katika ngazi za wilaya, kusajili wataalamu wa Tehama.


Aidha, ICTC imeandaa miongozo ya usimamizi wa usajili wa wataalamu wa TEHAMA, usimamizi wa taasisi zinazotoa mafunzo ya wataalamu wa Tehama na usimamizi wa watoa huduma za TEHAMA. Miongozo hii inalenga kuweka mazingira wezeshi katika utoaji wa huduma za Tehama na hivyo kukuza sekta ya Tehama nchini.


Inaendelea na utafiti kwa ajili ya kupima maendeleo ya intaneti nchini, mwingiliano wa mifumo ya Kitaifa na hali ya ukuaji na maendeleo ya kampuni changa za kukuza bunifu nchini.
Tume pia inaratibu na kuandaa matukio ya kuvutia uwekezaji na kutangaza masoko ya bidhaa za Tehama ndani na nje ya nchi.


Tume pia ipo katika mpango wa kujenga kituo cha Akili Mnemba/Bandia (Artificial Intelligence) na kuanzisha Kituo cha Resilience Academy nchini kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Turku cha Finland kwa ajili ya kuendeleza wataalamu wa Tehama. Tume inaendeleza bunifu za TEHAMA kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wa ndani na wa nje ya nchi.


Katika siku za hivi karibuni, Tume inatarajiwa kukutanisha wataalamu wa Tehama wa ndani na nje ya nchi katika Kongamano kubwa la Usalama wa Mitandao jijini Arusha. Tanzania ni moja ya nchi zinazofanya vizuri katika eneo la usalama wa mitandao, sasa ikishika nafasi ya pili kwa ubora barani Afrika.


No comments:

Post a Comment

Pages