March 28, 2024

WANAOKWAMISHA WAWEKEZAJI KUCHUKULIWA HATUA

Na Mwandishi Wetu

 

MAKAMU wa Rais Dk. Philip Mpango amesema Serikali haitasita kuchukua hatua kwa watumishi ambao watashiriki kukwamisha wawekezaji wanaotaka kuwekeza nchini, huku akitaja hatua nne walizochukua ili kuvutia wawekezaji.



Dk. Mpango amesema hayo jana mkoani Dar es Salaam wakati akifunga la Kongamano la Uwekezaji kati ya China na Tanzania lililokutanisha zaidi ya kampuni 300 za mataifa hayo kujadili fursa mbalimbali za uwekezaji.

Makamu wa Rais amesema kumekuwa na kasumba kwa baadhi ya watumishi wa umma kukwamisha wawekezaji kwa kuendekeza urasimu na rushwa, jambo ambalo hawapo tayari kuvumilia.



“Napenda kuchukua nafasi hii kuwaagiza watumishi wa umma ambao mnashiriki mchakato wa uwekezaji, na nitumie nafasi hii kuwaomba wawekezaji ambao watakutana na vikwazo wawasiliane na mimi,” amesema.



Amesema Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kukuza uchumi kupitia sekta ya uwekezaji hivyo atashangaa kuona mtumishi anashiriki kukwamisha.



Aidha Makamu wa Rais ametaja maeneo hayo kuwa ni kuondoa vikwazo kama urasimu, kupambana na rushwa, kuweka mazingira wezeshi na kuboresha sera na sheria.



“Ili uwekezaji uweze kufanikiwa, tumechukua hatua za kuboresha mazingira kwa kuondoa vikwazo vya urasimu, kupambana na rushwa, kuweka mazingira wezeshi na kuboresha sera na sheria,”amesema Dk Mpango.



Makamu wa Rais amesema iwapo watendaji wote ambao wanasimamia sekta ya uwekezaji wataepuka maeneo hayo manne ambayo ameanisha ni wazi kuwa sekta hiyo itakuwa na mchango mkubwa.



Amesema ni wakati wa kila Mtanzania kutamani maendeleo ya nchi yake na kuachana na urasimu ambao unakwamisha wawekezaji wa ndani na nje.



Dk Mpango amesema wawekezaji wanaokuja kuwekeza Tanzania wasisite kutoa taarifa kwa viongozi akiwemo yeye pale ambapo wanakutana na vikwazo kwa watendaji wa Serikali.



Amesema Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji katika sekta ya kilimo, viwanda, afya na nyingine nyingi, hivyo Serikali inataka zitumike kuchochea maendeleo.



Ameitaka nchi ya China kuleta wawekezaji wengi zaidi, hali ambayo itaendelea kudumisha uhusiano wao ambao umedumu kwa zaidi ya miaka 60 sasa.



Amesema  urafiki na uhusiano wa Tanzania na China umechangia ukuaji wa pato la taifa kutoka asilimia 4.8 mwaka 2020 hadi kufika asilimia 5.5 mwaka 2023 na inakadiriwa kuanzia mwaka 2024-2027 pato litafikia asilimia 6.0.

Dk Mpango amesema taarifa za ukuaji wa pato la taifa la Tanzania zimethibitishwa na Taasisi ya Moody’s na Fisch, hivyo kuwataka wawekezaji kuja kuwekeza kwa kuwa taifa hilo fursa nyingi.



“Novemba mwaka 2022, Taasisi ya Moody’s iliizawadia Tanzania alama ya B2 kwa mtazamo chanya na Desemba mwaka 2023, Fisch iliipa Tanzania Tuzo ya alama B+. Machi 22, Moody’s ilipandisha Tanzania daraja B1 kwa mtazamo thabiti, kwa vigezo hivyo ni wazi kuwa Tanzania inaenda kwenye mafanikio,” amesema.


Amesema ukadiriaji huo ni kielelezo cha ukuaji uchumi wa nchi ambao umeweza kuhimili changamoto za mtikisiko wa uchumi duniani baada ya janga la virusi vya corona.



Amesema Tanzania iko kwenye eneo la kimkakati kijiografia ambalo linaifanya kuwa kitovu cha biashara cha kikanda, soko kubwa la ndani lenye watu milioni 64.



“Soko la kikanda la watu takribani bilioni 1.4 chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA) ni sababu nyingine ya kuwaomba wawekezaji kuja kuwekeza,” amesema.



Mpango amesema mageuzi ya uwekezaji na biashara ambayo yanaonekana kwa asilimia kubwa yamechangiwa na falsafa ya 4R ya Rais Samia.



Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema wawekezaji kutoka China wamekuwa wakizingatia muda mfupi wa majadiliano na ni wavumilivu.



“China inakwenda mahali ambapo mataifa mengine yenye nguvu yanashindwa kwenda. Miaka 50 iliyopita tulikuwa na tatizo la reli, na karibu mataifa yote yenye nguvu yalikuwepo lakini hayakuwa tayari kutusaidia kujenga reli, na wakati huo China haikuwa nchi tajiri kama ilivyo sasa, lakini ilikubali kutujengea reli yetu ambayo ni reli ya kukumbukwa, imani yetu watakuja wengi kuja kuwekeza Tanzania,” amesema.



Prof. Kitila amesema Tanzania ina soko kubwa la ndani, hivyo kuwataka wawekezaji na wafanyabiashara kuja kuwekeza nchi kwa kuwa mazingira ni mazuri.



“Tuna bidhaa nyingi ambazo tunaagiza kutoka nje, ambazo tulipaswa kuzalisha hapa ikiwemo mafuta ya kupikia, sukari ba nguo, hivyo ujio wa kampuni hizi 60 kutoka china ni ishara nzuri kwa siku zijazo,” amesema.



Kitila amesema Tanzania ina vigezo vyote 10 vya kuvutia uwekezaji duniani, ambapo mojawapo ya vigezo ni utulivu wa kisiasa na amani uliopo nchini.



Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Dk Tausi Kida amesema kuanzia mwaka 2021 hadi Desemba 2023 jumla ya miradi 256 kutoka China ilisajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ambayo ina thamani ya Dola za Marekani bilioni 2.4 huku ikitoa ajira zaidi ya 29,122.



 
“Hawa ni wadau wetu na washirika wa maendeleo na uchumi katika kongamano hilo kampuni 60 kutoka Jimbo la Jinhua,China zimekuja  nchini na zimetembelea eneo la uwekezaji la Sino-Tanzania mkoani Pwani na kuona fursa na miradi ya uwekezaji inayoendelea,”amesema Dk Kida.



Aidha, Dk Kida amesema uwekezaji wa moja kwa moja kutoka taifa hilo nchini unaongezeka kutoka Dola za Marekani milioni  92 mwaka 2019 hadi Dola za Marekani milioni 221 mwaka 2021.



Ametaja midair ambayo watu kutoka China wamewekeza ni viwanda, ujenzi wa biashara, kilimo, uchukuzi na huduma.



Balozi wa China nchini,  Chen Mingjian, amesema Tanzania ina nafasi maalum na muhimu katika urafiki kutoka na uimara wa misingi waliyoiweka waasisi wetu Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Mao Zedon.



“Tunafurahi kuona uwekezaji wa China hapa Tanzania ukitoa mchango mkubwa wa uchumi wa nchi na jamii kwa ujumla, na hii inatupa faraja kwetu kuona kwamba tuna na safari inayofanana. Hadi sasa ajira zaidi ya 150,000 zimezalishwa kutokana na miradi ya uwekezaji kutoka china,” amesema.



Amesema wawekezaji kutoka China wanaiona Tanzania kama ni nchi ya ahadi na kutumia rasilimali zilizopo kuleta tija kwa malengo ya kunufaisha nchi zote mbili, lakini pia kuifanyaTanzania kuwa ni kituo cha uzalishaji.



Amesema kuwa maendeleo makubwa ya utulivu pamoja na uongozi madhubuti wa Serikali, wafanyabiashara wengi wa China wamevutiwa kuja kuwekeza Tanzania, na zaidi mapokezi wanayopata yanawafanya waendelee kushiriki.



Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Angelina Ngalula amesema chini ya uongozi wa Rais Samia, Tanzania imeweka alama katika kuboresha mazingira ya uwekezaji, hali ambayo inavutia wawekezaji.



“Urari wa biashara kati ya Tanzania na China umezidi kuongezeka, na kufikia mwaka 2022 urari wa biashara katika nchi hizi ulifikia zaidi ya dola bilioni 8, na kupelekea China kuwa ni mbia mkubwa wa biashara kwa nchi ya Tanzania, kwa kipindi cha zaidi ya miaka 8 mfululizo,” amesema.



Katibu wa  Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) wa serikali ya Jinhua nchini China Zhu Chonglie amesema wao kama Mkoa wa Zhejiang, na Serikali yao ya Jiji la Jinhua watahakikisha wawekezaji wanakuja kuwekeza nchini.



Amesema wamekuwa na ushirikiano kwa muda mrefu akitolea mfano kongamano la elimu liliratibiwa na Chuo cha Zhejiang Normal University Tanzania China Education Forum.



Amesema, Tanzania imekuwa nchi ya kwanza Afrika kupokea vikundi mbalimbali vya maonyesho ya utamaduni lakini pia vikundi vya Tanzania vimefika Zhejiang kubadilishana uzoefu.



“Ujio wetu hapa kwa ajili ya Kongamano hili la Uwekezaji ni matokeo ya ushirikiano wa kihistoria uliopo lakini na ukuaji unaoendelea, tunapaswa kuutunza kupitia mabadilishano kama haya ya kiuchumi,” amesema.


No comments:

Post a Comment

Pages