April 06, 2024

JOWUTA yaandaa mpango mikakati wa miaka mitatu

Mwandishi Wetu

 

CHAMA cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) kimekamilisha  Mpango Mikakati wa Kazi  wa Miaka Mitatu ambao pamoja na mambo mengine unalenga kutetea haki za wafanyakazi kwenye vyombo vya habari nchini.



Wajumbe wa Kamati ya Utendaji wa JOWUTA wamekamilisha mpango kazi huo katika kikao ambacho kimefanyika leo April 5, 2024 katika Ofisi za JOWUTA jijini Dar es Salaam.


Katika kikao hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti wa JOWUTA Taifa, Mussa Juma pia JOWUTA kwa kushirikiana na mashirika ya kimataifa na  taasisi za ndani, imejipanga kutoa elimu juu ya masuala ya haki za wafanyakazi, namna ya kusaini mikataba ya kazi na mikataba ya hali bora maeneo ya kazi kwa waandishi nchini.

Juma amesema mpango kazi huo unatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni na kwamba wamejipanga kushirikiana na wadau wengine kutoa mafunzo kwa wanahabari juu kuandika habari za uchaguzi,  Akili Bandia (Artificial Intelligence), Ulinzi na Usalama kwa wanahabari wakati wa kutekeleza majukumu yao.

"Tunaendelea kutafuta wadau ambao tutashirikiana nao kuhakikisha taaluma ya habari inaheshimika nchini, kwa wanahabari kulipwa vizuri, kuwa  na mikataba ya kazi lakini kujua haki zao sehemu ya kazi," amesema

Awali Katibu Mkuu wa JOWUTA, Selemani Msuya amesema mpango kazi huo unakwenda kusaidia kuonekana mchango wa wanahabari katika pato la Taifa kwani watakuwa wakilipa kodi mbalimbali baada ya kupata ajira ama mikataba bora.

"Kuna waandishi zaidi ya 10,000 nchini wakipatiwa elimu ya masuala ya kazi na wakaajiriwa ama kujiajiri serikali pia itanufaika kupitia makato ya mshahara, michango ya mifuko ya hifadhi na kwingine, "amesema.

Naibu Katibu Mkuu wa JOWUTA, Said Mmanga na Mwekahazina Lucy Ngowi wamewaomba wadau mbalimbali kuendelea kuiunga mkono JOWUTA lakini pia wanahabari na wafanyakazi katika vyombo vua habari kujiunga na chama hicho.

"Kwa mujibu wa sheria JOWUTA ndio chama pekee chenye mamlaka ya kisheria kutetea na kupigania maslahi ya waandishi wa habari kwa njia ya mazungumzo hadi mahakamani, tunaomba waandishi wajiunge na chama hiki ili tuweze kusukuma hili gurudumu kwa pamoja," amesema.

JOWUTA imesajiliwa na msajili wa vyama vya wafanyakazi nchini na hadi  sasa ina zaidi ya wanachama 300 nchini nzima.


No comments:

Post a Comment

Pages