HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 02, 2024

Marekani na Tanzania zashirikiana kupambana na mlipuko wa Kipindupindu

Katika kukabiliana na mlipuko wa kipindupindu ambao umekuwepo kwa miezi kadhaa sasa, Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) na Taasisi ya Marekani ya Kudhibiti Maradhi (CDC) kwa ushirikiano na Wizara ya Afya ya Tanzania, zimekuwa zikifanya kazi na jamii zilizoathiriwa kusaidia kuzuia maambukizi ya kipindupindu, kupeleka wataalamu wa afya katika maeneo yaliyoathirika na kutafuta njia za kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama.

 

Kufuatia ombi la msaada la Wizara ya Afya, USAID imetenga Shilingi za Kitanzania milioni 480 kusaidia jamii zilizoathiriwa zaidi nchini Tanzania, huku CDC ikiunga mkono jitihada hizo kwa kupeleka wataalamu wa afya kutoka Programu ya Mafunzo ya Epidemiolojia na Maabara ya Mafunzo katika mikoa sita iliyoathirika. Kwa pamoja, msaada huu umekuwa na utaendelea kuimarisha elimu ya afya juu ya maji safi na salama, usafi wa mazingira, na tabia ya usafi binafsi (WASH); ukiwahimiza wagonjwa kutafuta huduma za matibabu; kurahisisha tathmini za kaya za namna zinavyozingatia usafi; na kuongeza usambazaji wa vidonge vya kutakasa maji.

 

"Balozi wa Marekani nchini Tanzania Michael Battle alisema, “Marekani ina dhamira ya dhati kuendelea kushirikiana na kusimama na serikali ya Tanzania katika mapambano yake dhidi ya ugonjwa huu,” Aliendelea kusema “Kipindupindu ni ugonjwa hatari, lakini unaweza kuzuilika. Kwa pamoja, tunaweza kuudhibiti na kuokoa maisha ya Watanzania.”

 

Ufadhili unaoendelea wa USAID wa Dola za Kimarekani milioni 50 unalenga kutoa suluhisho la muda mrefu kwa kuboresha miundombinu ya maji na kukuza uelewa wa jamii juu ya upatikanaji wa maji salama na kuwapatia zaidi ya Watanzania milioni mbili maji salama na salama na huduma bora za usafi wa mazingira.  Katika mwaka huu wa 2024, USAID itaanza kujenga mifumo mipya ya maji na mitambo ya kusafisha mahi taka ili kuwapatia watu wengi zaidi maji safi na salama, huku ikijenga uwezo wa usimamizi, matengenezo na matunzo bora ya miradi iliyopo ya maji, maji taka na usafi.

 

Tangu Septemba 2023, mlipuko wa kipindupindu umekuwa ukiongezeka nchini Tanzania na zaidi ya visa 2,500 na vifo 46 vimeripotiwa. Mlipuko huu, ulioathiri mikoa 18, ni wa nne kwa wingi wa visa vilivyoripotiwa na wa tatu kwa kiwango cha vifo vilivyojitokeza katika miongo minne iliyopita. Hatua zilizochukuliwa na Wizara ya Afya zimeweza kupunguza maambukizi na kuwezesha mikoa saba kutangaza kuweza kudhibiti mlipuko wake. Hata hivyo, bado kuna mlipuko katika mikoa 12, huku mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Mwanza ikiwa imeathirika zaidi.

 

Kujifunza jinsi ya kuzuia kipindupindu tembelea: https://www.cdc.gov/cholera/pdf/cholera-five-basic-prevention-steps-h.pdf

 

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na Kitengo cha Habari cha Ubalozi wa Marekani kwa Barua Pepe DPO@state.gov

No comments:

Post a Comment

Pages