Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Rufiji mkoani Pwani Mhe. Mohamed Mchengerwa, ametoa Sh.milioni 40 kwa ajili ya kusaidia ununuzi wa mbegu kwa zaidi ya wakazi 1,000 wa maeneo mbalimbali ya wilaya ya Rufiji ambao mali, mashamba na makazi yao yameathiriwa na mafuriko ya maji, yaliyofunguliwa kutoka bwawa la uzalishaji umeme la Mwalimu Nyerere.
Akizungumza
na wakazi hao mara baada ya kufanya ziara ya kukagua athari ya mafuriko
hayo katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo, Waziri Mchengerwa amesema
analazimika kutoa kiasi hicho cha pesa ili kuwatia moyo wakazi hao
kurejea shambani kulima upya baada ya mazao yao kusombwa na mafuriko
hayo.
“Hili ni janga letu sote mimi na nyinyi, tuliamini kwamba
ujenzi wa JNHPP utakuwa mkombozi wa mafuriko ambayo yamekuwa yanatukumba
mara kwa mara lakini kwa bahati mbaya bado imejitokeza, tuendelee kuwa
na Imani kwamba mradi ukikamilika uwenda changamoto hii ikawa
imetatuliwa” alisema Waziri Mchengerwa.
Aliongeza kuwa “
Ninafahamu fika namna wakazi wa Rufiji mlivyokuwa mmelima kwelikweli
mwaka huu, ninaomba turejee shambani tulime tena vilevile kwa kiwango
kikubwa, mimi ninamkabidhi Mkuu wa wilaya shilingi milioni 40 kwa
kuanzia kwa ajili ya kusaidia ununuzi wa mbegu ili turejee shambani
tupande tena tusije kufa kwa njaa”
Alikadhalika Waziri
Mchengerwa ametoa wito kwa taasisi na mashirika ya misaada ya kibinadamu
Pamoja na wasamalia wema kuguswa na hali ya Warufiji kwa kuwashika
mkono kwa namna moja au nyingine katika kipindi hiki ambacho serikali ya
wilaya inaendelea na ufuatiliaji na tathimini ya athari za mafuriko
hayo kwa ujumla.
“Ukweli niseme kiasi hiki cha milioni 40
nilikuwa nimekidunduliza kutoka kwenye mshahara wangu kwa ajili ya
kuhakikisha tunakuwa na futari ya Pamoja katika kipindi hiki cha mwezi
mtukufu wa Ramadhan kama tunavyofanya kila mwaka, lakini kwa hali hii ya
mafuriko niseme tu kwamba futari si kitu nalazimika kutoa kiasi hiki
kwa ajili ya ununuzi wa mbegu na nitaenda kuwaomba marafiki zangu
wanichangie angalau tufikishe milioni 100 kwa ajili ya kusaidia warufiji
walioathirika na mafuriko haya” Aliongea Waziri Mchengerwa.
Halima
Mbwana mkazi wa Kijiji cha Chumbi ambaye ni miongoni mwa waathirika wa
mafuriko hayo amedai kuwa hali inazidi kuwa mbaya kuanzia chakula,
marazi na makazi na hivyo wanatamani kupata wasamalia wa kuwashika
mkono.
“Tumesalia watupu, mazao shambani yamesombwa na maji na
hata vyakula vya ziada tulivyokuwanavyo vimesombwa pia, nyumba nazo
zimesombwa na maji sasa hatuna pa kuishi wala hatuna chakula, tunaomba
tusaidiwe maana hali zetu ni mbya kwakweli” alisema Mbwana.
Kwa
mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ambaye pia
ni Mkuu wa wilaya ya Rufiji Meja Edward Gowele tathimini ya awali
imebaini kuharibiwa kwa nyumba 58, na jumla ya wakazi 951 waliokuwa
wakiishi kwenye maeneo ya vitongoji vya Kanga,Kiegele, Kilindi na
Nyandote katika kata ya Chumbi wameondolewa katika maeneo yao
nakuhamishiwa sehemu salama, huku zaidi ya hekta elfu 28,374.74 za mazao
ya kilimo na bishara kama vile mahindi, Mpunga, Ufuta nan dizi
zikiathiriwa na mafuriko hayo.
No comments:
Post a Comment