April 30, 2024

Waziri Mkuu apongeza jitihada za Benki ya CRDB kuiwezesha sekta ya kilimo


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akitoa hotuba yake kwenye Jukwaa la CRDB Bank Uwekezaji Day lililofanyika jijini Dar es Salaam na kuwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo.

Mkuugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, akizungumza na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo waliofika katika Jukwaa la CRDB Bank Uwekezaji na kujifunza fursa mbalimbali za kuboresha na kuongeza tija katika shughuli za kilimo na ufugaji.

 Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB, Ally Laay, akizungumza wakati wa Jukwaa la CRDB Bank Uwekezaji Day lililowakutanisha wadau wa sekta ya kilimo. 


 

 

Dar es Salaam, Tanzania Tarehe 28 Aprili 2024: Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameipongeza Benki ya CRDB kwa jitihada zake za kuiwezesha sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi nchini hali inayosaidia kukuza kipato cha wananchi na kurimaisha uchumi wa taifa. 


Waziri Mkuu ametoa pongezi hizo alipofungua semina maalumu ya CRDB Bank Uwekezaji Day iliofanyika jijini Dar es Salaam ikihududhuriwa na mamia ya wadau wa sekta ya kilimo nchini ambako Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela ameiomba serikali kushirikiana na wadau kuongeza uwezeshaji wa sekta ya kilimo nchini.

 

Nsekela amesema ingawa mikopo inayotolewa kwenye sekta ya kilimo inazidi kuongezeka lakini idadi ya wanufaika bado ni wachache hivyo juhudi zaidi zinahitajika kuongeza uwekezaji jambo litakalopandisha tija na kukuza kipato cha wakulima na pato la taifa kwa ujumla.

 

Akitoa pongezi hizo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema ubunifu wa Benki ya CRDB kuwakutanisha wadau wa kilimo kujadili fursa zilizopo na kuweka mipango ya kutatua changamoto wanazokabiliana nazo zinaendanana na mipango na juhudi za kuwajumuisha Watanzania katika uchumi.

 

Akieleza mikakati ya serikali, waziri mkuu amesema juhudi za makusudi zinafanywa kuwaongezea wananchi fursa ya kunufaika na vivutio vya uwekezaji kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ambacho kimepunguza kiwango cha mtaji unaohitajika ili kupata Cheti cha Kivutio Biashara (Certificate of Incentives) na kuwa nusu ya kile kinacholipwa na wawekezaji wageni. 

 

“Kabla ili mradi wa Mtanzania upate Cheti cha Kivutio ulitakiwa uwe na thamani isiyopungua dola 100,000 za Marekani (shilingi milioni 250) ambacho tumekipunguza kwa nusu nzima. Sasa hivi mradi wa dola 50,000 sawa na shiling milioni 125 unapata Cheti cha Kivutio kutoka Kituo chetu cha Uwekezaji,” amesema Majaliwa.

 

Waziri mkuu amesema anatambua umuhimu wa kuungana na sekta binafsi hasa Benki ya CRDB iliyotenga siku mahsusi ya kuonyesha fursa za uwekezaji zilizopo kwenye sekta ya kilimo na kuonyesha jinsi ilivyojipanga kutoa huduma za fedha kuwezesha uwekezaji katika kilimo. Amesema serikali imejipanga kushirikiana na sekta binafsi kuwezesha uwekezaji kwenye sekta ya kilimo.

 

Vilevile, Majaliwa amesema mabadiliko ya tabianchi ni changamoto kubwa kwa zama hizi kwani athari zake zinazojumuisha ukame, mafuriko, ongezeko la joto na upepo mkali na vimbunga, zinapunguza  kiasi cha maji ardhini, ongezeko la milipuko ya magonjwa ya mimea na wanyama, na wadudu waharibifu. 

 

Kutokana na hayo, amesema zinajitokeza changamoto mpya zinazofifisha jitihada za wakulima na wafugaji kuongeza tija hivyo serikali itaongoza mapambano kuhakikisha sekta hii muhimu inakuwa stahimilivu na inayokua kwa manufaa ya taifa. 

 

“Napenda mnapoendelea na semina hii mfikirie na mzungumzie ni kwa jinsi gani waTanzania wengi zaidi wataweza kuingia kwenye hizi sekta ili kuongeza tija na ufanisi. Mfikirie na kuzungumza, ni jinsi gani sote tunaweza kuongeza matumizi ya stadi, pembejeo na teknolojia bora zaidi zitakazowezesha kilimo stahimilivu wakati huu wa mabadiliko ya tabianchi. Mfikirie namna gani tutaongeza ushirikiano kati ya serikali na wadau wote wa kilimo,” amesisitiza Majaliwa.

 

Akionyesha kiwango cha mikopo kinachotolewa kwenye sekta ya kilimo, Nsekela amesema mwaka 2023, Nsekela amesema sekta ya kilimo ilikopeshwa dola milioni 686 za Marekani (shilingi trilioni 1.715) ambazo ni zaidi ya mara tatu ya zile zilizotolewa mwaka 2022, dola milioni 218 (shilingi bilioni 545). Mwaka 2021, sekta hiyo ilikopeshwa dola milioni 21 (shilingi bilioni 52.5) zikipanda  kutoka dola milioni 16 (shilingi bilioni 40) zilizokopeshwa mwaka 2020.

 

“Sekta yetu ya kilimo bado inaongozwa na wakulima wengi wadogo ambao ni asilimia 91. Katika zaidi ya hekta milioni 44 zinazofaa kwa kilimo nchini, ni asilimia 2.5 tu ya ardhi hiyo ndio imewekewa miundombinu ya umwagiliaji. Hiki ni kiasi kidogo hivyo tunahitaji juhudi za pamoja katika serikali na sekta binafsi,” amesema Nsekela.

 

Kati ya changamoto zinapaswa kushughulikiwa, Nsekela amezitaja kuwa ni ukosefu wa pembejeo, uzalishaji usiozingatia viwango vinavyokubalika kimataifa na kukosa taarifa sahihi za masoko ya mazao na bidhaa husika. Nyingine ni kukosekana kwa fedha za uwekezaji, kutokuwa na taarifa za kitafiti na ukosefu wa mafunzo kwa wakulima.

 

Ikishirikiana na wadau tofauti wa ndani na kimataifa, Nsekela amesema Benki ya CRDB imeshaanza kushughulikia baadhi ya changamoto hizo kwa kubuni huduma na bidhaa rafiki zinazoendana na mazingira ya wakulima wa nchini hasa kukidhi mahitaji yao ya mikopo.

 

“Tunatoa mikopo ya aina tofauti kuanzia ya kununua mitambo ya kilimo na umwagiliaji mpaka gharama za uendeshaji. Kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani, tunatoa mpaka  shilingi bilioni 80. Kuanzia wa mkulima mdogo mpaka mkubwa, tunatoa bima ya mavuno, ukame au mafuriko, na athari zitakazotokana na mabadiliko ya tabianchi,” amesema Nsekela.

 

Akieleza uwezo wa Benki ya CRDB ambayo mpaka sasa imeshakopesha zaidi ya shilingi trilioni 1.6  kufadhili miradi ya kilimo, Nsekela amesema wanashirikiana na wabia zaidi ya 200 ili kuimarisha uwezo wake wa kutoa mikopo ya kilimo.

 

“Benki ya CRDB peke yetu tunaweza kukopesha mpaka dola milioni 107 za Marekani (shilingi bilioni 267.5), lakini mteja anayekuja katika dirisha tunaloshirikiana na Mfuko wa Mazingira Duniani (GCF) anaweza kupata mpaka na dola 250 (shilingi bilioni 625), na kwa miradi itakayotekelezwa kwa ufadhili na wabia wetu wengine, kiwango wanachoweza kukopa hakina ukomo kwa mradi wowote wa kilimo walionao,” amesema Nsekela.

 

Semina ya CRDB Bank Uwekezaji Day ilitanguliwa na maonyesho ya bidhaa kutoka kwa wajasiriamali waliopo kwenye sekta ya kilimo, mifugo na ufugaji ambao ni wateja wa Benki ya CRDB. Wajasiriamali hao walijumuisha wauzaji na wasambazaji wa pembejeo za kilimo, dawa na chanjo za mifugo, vyakula na malisho ya mifugo.

No comments:

Post a Comment

Pages