Wakuu wa Idara na Vitengo katika Manispaa ya Singida wakifuatilia kwa karibu Kikao kinavyoendelea.
Na Mwandishi Wetu
Meya wa Manispaa ya Singida Yagi Kiaratu amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo kuhakikisha anashirikiana na Wataalamu wa Ardhi katika kutatua na kukomesha haraka tatizo la migogoro ya mipaka ya ndani na nje ya Manispaa hiyo kabla ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kufanyika.
Amesema migogoro ya mipaka isipopatiwa ufumbuzi haraka inaweza kuathiri kwa njia moja ama nyingi uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao unatarajiwa kufanyika hivi karibu kutokana na kutokuwepo kwa mipaka halisi ya kiutawala katika baadhi ya maeneo.
Meya Yagi Kiaratu ametoa agizo hilo le katika Kikao cha Baraza la Madiwani lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa VETA mjini Singida.
Amesema migogoro kati ya Manispaa na Halmashauri nyingine ni Vizuri Mkurugenzi akamshirikisha Katibu Tawala wa mkoa wa Singida, Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya SINGIDA pamoja na Wazee wa maeneo husika ili kurahisha utatuzi wa migogoro hiyo bila usumbufu.
Kuhusu ukusanyaji wa Mapato, Meya wa Manispaa ya Singida amesema hali ya ukusanyaji wa mapato kwa sasa inaridhisha lakini kasi zaidi inahitajika ili kufikia asilimia 1OO ya ukusanyaji wa Mapato ndani ya Manispaa hiyo.
Amesema hadi sasa Manispaa ya Singida imekusanya zaidi ya asilimia 91 ya mapato yake ya ndani na muda bado upo hivyo ni muhimu kwa Watendaji wote wakashirikiana na kuanzisha vyanzo vipya vya mapato ili kufikia malengo waliyojiwekea.
“Mnapaswa kujitathmini kwa siku unakusanya nini na unapaswa kukusanya nini kwa mwezi ili tufikie malengo ya ukusanyaji tuliyojiwekea”amesisitiza Meya Kiaratu.
Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Singida Lucia Mwiru amesisitiza usimamizi madhubuti katika miradi ya maendeleo ili kukomesha tabia la baadhi ya Miradi kutelekezwa chini ya kiwango.
Lucia Mwiru amesema kuna umuhimu mkubwa kwa viongozi wote kushirikiana katika usimamizi wa miradi hiyo ili kuondoa hali ya sintofahamu pindi miradi hiyo inapokwama au kutekelezwa kwa kiwango duni.
No comments:
Post a Comment