Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam
Shirika
lisilo la Kiserikali laThe Foundation for Civil Society (FCS) na
TradeMark Africa (TMA) yamesaini makubaliano ya utekelezaji wa Mradi wa
kuboresha mazingira wezeshi na jumuishi ya kibiashara yenye lengo la
kuhakikisha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wanajumuishwa
kikamilifu katika uendeshaji wa biashara.
Makubaliano
hayo pia yana lengo la kuyawezesha makundi hayo kukabiliana na
changamoto kubwa za kimfumo na tabianchi kama sehemu ya kuchochea ukuaji
endelevu wa uchumi Tanzania.
FCS imepokea
ruzuku ya Sh Bilioni 2.3 kutoka TradeMark Africa kutekeleza mradi huu
ambao umefadhiliwa na Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na
Maendeleo (FCDO), Ireland na Norway ambazo zimetoa dola za Kimarekani
900,000. Mradi pia unalenga kuunganisha nguvu za sekta binafsi na
mashirika ya kiraia ili kukuza ukuaji wa uchumi wa kijani.
Tafiti
zinaonyesha kwamba wanawake wanaweza kutoa mchango mkubwa wa kiuchumi
kama wakishirikishwa kikamilifu katika mifumo ya biashara. Hata hivyo,
wanawake wengi nchini Tanzania bado wanakumbana na vikwazo vingi
vinavyowazuia kushiriki kikamilifu katika sekta ya biashara.
Mradi
huu unalenga kukabiliana na vizuizi hivi na kuweka mazingira wezeshi ya
biashara ambayo yanajumuisha watu wote na kukuza ustawi wa wote.Mradi
huu ni wa kipekee na utajumuisha sekta binafsi pamoja na asasi za kiraia
ili kuimarisha biashara ambayo ni ya umoja na endelevu ya mazingira.
Katika kipindi cha miezi 18 ijayo, FCS itatekeleza mkakati katika sekta
nyingi za biashara, ikilenga kupunguza athari za matumizi ya mazingira
na kukuza ushirikishwaji katika manufaa ya kiuchumi.
Akizungumza
na wanahabari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkazi wa TradeMark
Africa, Elibariki Shammy, amesema, “Mradi huu ni muhimu kwa malengo yetu
ya kimkakati ya kuchochea ukuaji wa biashara ambao ni endelevu na
shirikishi. Tunaamini kwamba kupitia ushirikiano huu wa kimkakati baina
yetu na FCS, tunaweza kuleta matokeo chanya na makubwa katika kuboresha
mazingira ya biashara jumuisha nchini. Kuwawezesha wanawake ni jambo la
maendeleo. Kuwajumuisha wanawake katika biashara kunakuza uchumi na
kuinua jamii nzima. Kupitia mradi huu na ushirikiano baina yetu na FCS,
tunalenga kuendeleza mfumo bora wa biashara ambao unajumuisha na
unaoweza kukabiliana na changamoto za biashara ya kimataifa.”
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Justice Rutenge, ameelezea
umuhimu wa mradi huo."Ulinzi wa mlaji ni muhimu sana katika soko la
biashara la kitaifa na kimataifa. Ushirikiano wetu na TradeMark Africa
ni hatua kubwa ya kulinda haki za mlaji nchini na kuwezesha mazingira
wezeshi ya kibiashara yaliyo bora na yanayokabiliana na changamoto za
tabianchi nchini. Tutahakikisha kwamba faida za biashara ni shirikishi
na zinanufaisha wananchi wote katika jamii yetu,” amesema.
Amebainisha
kuwa FCS ina jukumu la kipekee kama AZAKI na itaweza kutumia vyema
ubobezi wake katika sekta kushirikiana na sekta binafsi kushughulikia
masuala muhimu ya uharibifu wa mazingira na ukosefu wa usawa katika
kijamii.
Amesisitiza kuwa mradi huo unalenga
kuweka mazingira ya biashara ambayo ni jumuishi na endelevu kwa kuongeza
fursa za kibiashara kwa makundi ya pembezoni, kushirikiana na asasi za
kiraia kushughulikia mahitaji yao, kukuza mazingira ya biashara rafiki
na kuimarisha ulinzi wa
walaji.
Ameongeza
kuwa TMA itasadia jamii za pembezoni kupitia kilimo-mahiri na programu
za masoko na kuchangia ukuaji endelevu wa biashara zao. Aidha, kwa
kutetea ukuaji wa biashara endelevu, mradi huu unalenga kuboresha
ustahimilivu wa biashara dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na hivyo
kuchangia katika uendelevu wa muda mrefu wa uchumi wa Tanzania na
uendelevu wa mazingira.
Amefafanua kuwa mradi
pia unajumuisha matumizi ya teknolojia za kibunifu za kidijitali kama
vile majukwaa ya kujifunza kielektroniki mbinu za kilimo mahiri,
kuimarisha utayari wa soko naushindani wa kimataifa wa bidhaa za
Tanzania.
Pia amesema makubaliano hayo ni
kielelezo tosha cha jinsi ushirikiano wa sekta za umma na binafsi
unavyoweza kushughulikia kwa ufanisi changamoto za kimfumo katika masoko
ibuka na kuunda njia za mazoea ya biashara jumuishi na endelevu.
No comments:
Post a Comment