May 09, 2024

‘WALIOTAFUNA’ MILIONI 39.5 KIBAONI KUCHUKULIWA HATUA



Mkuu wa wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi Alhaji Majid Mwanga akizungumza wakati wa uwasilishaji taarifa ya ukaguzi wa mapato na matumizi kutokana na migogoro ya ardhi katika kijiji cha Kibaoni halmashauri ya Mpimbwe mkoa wa Katavi.

 

 Na Munir Shemweta, MLELE

 

Mkuu wa wilaya ya Mlele mkoani Katavi Alhaji Majid Mwanga amesema wahusika wote wa ubadhilifu wa fedha shilingi 39,501, 665 katika kijiji cha Kibaoni halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

 

Alhaji Mwanga ametoa kauli hiyo katika mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji cha Kibaoni wakati wa uwasilishaji taarifa ya uchunguzi wa mapato na matumizi iliyotokana na migogoro ya ardhi katika kijiji cha Kibaoni iliyosomwa na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Mpimbwe Bi. Shamim Daud.

‘’Hatutamfumbia macho mtu hata tone moja, baadhi ya viongozi wa kijiji na wao wamehusika kwenye upotevu wa milioni 39, 501, 665 wote hao walihusika lakini na watu ambao ni nje ya serikali ya kijiji walihusika kama ilivyosemwa mmoja wa watumishi yuko kampuni hiyo’’. Alisema Alhaji Majid Mwanga.

Akiwasilisha taarifa ya uchunguzi wa mapato na matumizi iliyotokana na migogoro ya ardhi kwenye kijiji cha Kibaoni, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele Bi. Shamim Daud amesema, maeneo yaliyohusika katika ubadhilifu ni pamoja na eneo la shule mpya ya Kibaoni ambapo wakati wa kupatikana kwake ilipunguzwa ekari 3 na kuwa 15 badala ya ekari 18.

Eneo lingine kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo Mtendaji wa halmashauri ya Mpimbwe Bi.Shamim ni la Viwanda Vidogo la SIDO ambapo fedha kiasi cha shilingi milioni 8.8 kwa ajili ya mauzo ya viwanja 48 hazikupelekwa benki na hakuna matumizi yoyote yaliyoonekana ya shughuli za serikali.

Aidha, makusanyo ya mapato ya shilingi 21,240,000 kutoka vyanzo vya mapato mbalimbali ya kijiji cha Kibaoni   yanayojumuisha michango ya jamii, kukodisha mashamba, tozo na faini mbalimbali kiasi kilichopelekwa benki kati ya jumla ya milioni 21,240,000 ni shilingi milioni 2 tu huku kisichopelekwa benki ni 1,9210,000.

‘’Kumetokea pia ubadhilifu wa fedha za kijiji kutoka katika akaunti yake ya jumla ya milioni 2.80 zilizotolewa katika kaunti kwa ajili ya kurejesha kwa watu 39 wakati hakuna fedha yoyote iliyoingizwa kutokana na tukio hilo’’. Alisema Bi. Shamim.

Kuhusu malipo ya fidia kwa serikali ya kibaoni kutokana na maeneo ya wananchi kuchukuliwa kwa ajili ya kuchimba vifusi na kuchukua udongo kwa ajili ya ujenzi wa barabra ya kibaoni- Sitalike, amesema pamoja na kijiji cha Kibaoni kupokea shilingi milioni 21 kutoka kampuni ya RSG Ltd na wananchi wawili nao kufidiwa lakini pesa zote hazikupelekwa benki. Kwa mujibu wa ripoti ya uchunguzi baadhi ya viongozi wa kata, watendaji wa vijiji na watumishi wa kampuni ya RSG walishiriki kugawana fredha za fidia.

Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kibaoni wametaka hatua za kisheria zichukuliwe kwa wote waliohusika kwenye ubadhilifu wa fedha ikiwemo kurejesha fedha walizochukua.

‘’Hizi pesa zote zirudi ili kupunguza msongamano wa mizigo iwe kuuzwa nyumba, iwe kiwanja au kufanya nini pesa zote ili anayekuja leo kibaoni ajue anapodokoa hata hata mia tano ya kula ya wizi ajue hii ni pesa inayoweza kuniunguza’’ alisema Mathelius Matabula.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa jimbo la Kavuu Mhe, Geophrey Pinda ametaka sheria ifuate mkondo wake huku akisisitiza kutaka fedha iliyoibwa kurudi kwa wananchi kwa kuwa tangu fedha hizo zipotee miradi mingi imesimama.

Mkuu wa wilaya ya Mlele Alhaji Majid Mwanga amemuelekeza mkurugenzi kuchukua hatua kwa watumishi wote waliohusika sambamba na kuiarifu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na  Jeshi la Polisi ili hatua za kuwakamata waliohusika wote ifanyike.

Tarehe 3 Novemba 2023 Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Mpimbwe alielekeza ufanyike ukaguzi wa mapato na matumizi ya kijiji cha Kibaoni ikiwa ni pamoja na kuhakiki hoja zilizoibuliwa kwenye taarifa ya Kamati huru ya uchunguzi wa migogoro ya ardhi kijiji cha kibaoni ambapo kazi ya ukaguzi ilianza 9 Novemba 2023 na kukamilika 25/3/2024. Miongoni mwa mambo yaliyobainika ni kuwepo kwa ubadhilifu wa fedha za umma na matumizi mabaya ya madaraka yaliyosababisha baadhi ya viongozi wa kata, viongozi na wajumbe wa serikali ya kijiji kuwa ni pamoja na watumishi kujinufaisha kwa kujigawia viwanja bila kufuata taratibu.


No comments:

Post a Comment

Pages