June 03, 2024

CRDB Bank Foundation, SUGECO yawaaga wahitimu wanaoenda mafunzoni Sweden

Mkuu wa Uendeshaji wa Biashara Changa Taasisi ya CRDB Bank Foundation, Fadhili Bushagama (kulia) na Meneja Mikopo Benki ya CRDB, Baraka Kiyalo (kushoto), wakikabidhi fedha kwa vijana wanaokwenda nchini Sweden kujifunza masuala ya Kilimo muda mfupi kabla ya kupanda ndege, vijana hao ni Robinson Pallangyo (wapili kulia) na Danson Shabani (wa pili kushoto). (Na Mpiga Picha Wetu).


NA MWANDISHI WETU

SIKU 52 tangu waliposaini Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) ya kufadhili Mafunzo ya Kukuza Ujuzi (Internship Program), Taasisi ya CRDB Bank Foundation na Ushirika wa Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUGEGO), wameliaga kundi la kwanza la wahitimu wanaokwenda masomoni nchini Sweden.

Aprili 9 mwaka huu, CRDB Bank Foundation na SUGECO, walisaini makubaliano hayo yanayolenga kunufaisha zaidi ya vijana 2,500 kwa kuongeza umahiri wa fani walizosomea, kupitia Programu ya IMBEJU, inayotoa mafunzo ya ujasiriamali pamoja na mtaji wezeshi kwa vijana na wanawake.

CRDB Bank Foundation na SUGECO, jana imewaaga wahitimu wawili Robinson Pallangyo na Danson Shaaban waliohitimu Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), wakielekea Sweden kwa mafunzo ya mwaka mmoja, kabla ya kurejea nchini kutekeleza mafunzo yao kwa vitendo.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuwaaga wahitimu hao, Mkuu wa Uendeshaji wa Biashara Changa wa CRDB Bank Foundation, Fadhili Bushagama, alisema makubaliano yao na SUGECO yameanza na vijana hao wawili, lakini idadi kubwa zaidi ya wanufaika itaongezeka siku za usoni.

“Tumeanza na vijana hawa wawili tuliowapata kwa ushirikiano wetu na SUGECO, vijana hawa wanaenda Sweden katika mafunzo ya kilimo kwa mwaka mmoja, baada ya hapo watarejea nchini kutekeleza mafunzo hayo ya kilimo kwa vitendo mkoani Morogoro.

“Wakiwa Morogoro, vijana hawa watalima kupitia mafunzo haya wanayoyaendea Sweden, nasi jukumu letu litakuwa kuwatafutia soko la bidhaa zao za kilimo huko Dubai, ambako wataenda kuuza mazao yao. Hii ni fursa kubwa kwa nchi yetu na tutaendelea kushirikiana na SUGECO kufanikisha kila kitu.

“Tunawaomba kwenda kuzingatria kinachowapeleka Sweden na kuhakikisha wanajifunza vema ili kuja kujitegemea na kujiajiri watakaporejea. Hawa wawili ni mwanzao, wengi zaidi wataenda na kujifunza kwa gharama ambayo haina riba, hata katika mitaji yao ya baadaye,” alisema Bushagama.

Kwa upande wake, Revocatus Kimario, ambaye ni Mkurugenzi wa SUGECO, alisema Robinson na Danson ni sawa na ‘watoto wa kwanza kuzaliwa’ kupitia mashirikiano baina ya CRDB Bank Foundation na Taasisi yake, yanayolenga kuwafungulia fursa wahitimu walio chini ya SUGECO kote nchini.

“Benki ya CRDB kupitia CRDB Bank Foundation, itawasapoti vijana hawa kupitia mitaji ya kuanzia inayohusisha gharama za usafiri kwenda na kurudi mafunzoni Sweden, ambapo wametenga zaidi ya Sh. Bil. 67 kwa miaka mitatu na hawa ndio hawa wanufaika wa kwanza kabisa.


“Vijana wengi zaidi watanufaika na fungu hilo, matarajio yetu ni kuwaona wakirejea wakiwa bora zaidi ya wanavyoenda, wanapaswa kuwa waaminifu huko, wakasome kwa bidii ili kunufaika na fursa hizi muhimu zinazolenga kuwakwamua vijana katika kukidhi mahitaji ya kimtaji na fursa.

“CRDB Bank Foundation na SUGECO ni daraja kati ya kijana, wanachojifunza na namna ya kupata pesa za kukidhi mahitaji na fursa za masoko. Sisi tunawaonesha fursa, na CRDB Bank Foundation jukumu lao ni uwezeshaji kifedha bila riba,” alibainisha Bushagama katika hafla hiyo ya kuwaaga.

Mnufaika Robinson Pallangyo kutoka SUA, aliishukuru SUGECO na CRDB Bank Foundation kwa uwezeshaji huo unaoenda kumpa mafunzo yatakayomwezesha kujitegemea na kujiajiri, huku akiwataka vijana wanaohitimu vyuo kujiunga SUGECO ili kunufaika na fursa hizo.

Naye Danson Shaban, ambaye pia ni Mhitimu SUA, hakusita kuishukuru CRDB Bank Foundation kwa kugharamia malipo ya masomo ya program hiyo, usafiri wa kwenda na kurudi, pesa za kujikimu, bima na mitaji wezeshi, gharama ambazo wasingeziweza kuzilipa kwa mifuko yao.



No comments:

Post a Comment

Pages