Na Jasmine Shamwepu, Dodoma
Waziri wa Maliasili na Utalii Angellah Kairuki ameeleza kuwa idadi ya watalii wa kimataifa wanaotembelea nchi ya Tanzania imeongezeka kwa asilimia 96 kutoka watalii 922,692 Mwaka 2021 hadi watalii 1,808,205 Mwaka 2023.
Aidha, idadi ya Watalii wa Ndani waliotembelea vivutio vya utalii imeongezeka kwa asilimia 152 kutoka watalii 788,933 Mwaka 2021 hadi kufikia watalii 1,985,707 Mwaka 2023.
Waziri Kairuki ametoa takwimu hizo wakati akisoma bajeti ya wizara ya maliasili na utalii iliyowasilishwa bungeni jijini Dodoma leo tarehe 31 Mei, 2024.
Waziri Kairuki ameongeza kuwa idadi ya wageni imeenda sambamba na kuongezeka kwa mapato yatokanayo na shughuli za utalii ambapo mapato yameongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 1.3 mwaka 2021 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 3.4 Mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 161 kwa watalii wa kimataifa.
Amesema mapato yatokanayo na utalii wa ndani pia yameongezeka kutoka Shilingi bilioni 46.3 Mwaka 2021 hadi Shilingi bilioni 175.3 Mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 279. Aidha, ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali uliongezeka kutoka Shilingi 397,428,671,968 Mwaka 2020/2021 hadi Shilingi 680,150,218,337 mwaka 2022/2023.
Waziri Kairuki ameongeza kuwa kwa mwaka wa Fedha 2023/2024 kuanzia Julai 2023, hadi kufikia Aprili 2024, Wizara imekusanya jumla ya Shilingi 750,992,839,479.75 sawa na asilimia 97.12 ya lengo la makusanyo.
Kwa upande wa eneo la Hifadhi ya Ngorongoro pekee idadi ya wageni imeongezeka kutoka watalii 752,000 na mapato ya shilingi bilioni 171,322,125,734 mwaka 2022/2023 hadi watalii 780,281 na mapato ya shilingi Bilioni 188,519,361,412 kwa kipindi cha kuanzia mwezi Julai, 2023 hadi mwezi aprili, 2024 sawa na ongezeko la asilimia 52.66 ikilinganishwa na mapato ya Shilingi 123,490,469,339 zilizokusanywa kwa kipindi kama hicho Mwaka wa Fedha 2019/2020.
No comments:
Post a Comment