July 23, 2024

CHW kuwafuata vijana kwenye ‘vigodoro’

Na Irene Mark, Morogoro

 
WATOA Huduma za Afya ngazi ya Jamii (CHW) na wahudumu wa afya ya uzazi, wamesema wapo tayari kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa vijana hadi kwenye ngoma za usiku ‘vigodoro’ na mafunzo ya unyago.


Miongoni mwa desturi za wenyeji wa Mkoa wa Morogoro ni mafunzo ya jando na unyago kwa vijana wa kike na kiume waliobalehe na kuhitimu kisha kufanyiwa sherehe za ngoma ‘kigodoro’ mchana na usiku huku wakikaribisha vijana na wanajamii nyingine.

 
Wakizungumza kwa nyakati tofauti CHW na watoa huduma hao kutoka Wilaya ya Morogoro Vijijini, Mkoa wa Morogoro wanasema elimu hiyo ni muhimu licha ya kukwamishwa na desturi za wakazi wa maeneo hayo.


Wanasema wilaya yao imebahatika kuwepo kwenye mradi wa Afya kwa Vijana uliofa dhiliwa na Umoja wa Ulaya, lakini mwitikio wa vijana kufuata elimu ya afya ya uzazi ni mdogo hivyo ni bora kuwafuata kwenye starehe zao.

 
Mohamed Komola ni CHW wa Kijiji cha Fulwe Mikese mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 25 kwenye kada hiyo amesema ni muhimu wakishirikishwa kwenye tamaduni zao walau kwa dakika 20 huku akiamini wapo watakaoelewa.

 
“Huku bwana wazazi wakati mwingine ni kikwazo wanafikiri kijana akielezwa ukweli ndio ataanza tabia mbaya wakati sisi tupo pale kumsaidia kijana ajue namna ya kukabiliana na hisia za mwili hasa wakati wa balehe.

 
“Wanapokuja zahanati wanapata elimu ya matumizi sahihi ya njia za uzazi wa mpango zitakazo wasaidia kuzuia mimba, kujikinga na maradhi lakini kikubwa wanashauriwa wajitunze ili kufikia ndoto zao,” amesema CHW wa muda mrefu, Komola.


Mmoja wa wazazi walioruhusu vijana wao kushiriki kwenye huduma za elimu ya afya ya uzazi, Mwalimu mstaafu wa shule mbalimbali za Wilaya ya Morogoro Vijijini, Nurdin Mbwambo aliwashauri wazazi wengine kuwaruhusu vijana wao kupata elimu hiyo.


Amesema changamoto nyingi za vijana zikiwemo mimba za utotoni na magonjwa ya zinaa zinawakuta vijana kwa sababu hawana elimu sahihi ya masula ya uzazi.

 
“Ni ngumu kuwapata vijana wengi kwa pamoja na watulie wakusikilize lakini ukiwekwa utaratibu wa kuwalazimisha wana jamii wanapofanya desturi zao wawashirikishe hawa CHW ili wapate walau dakika 20 za kuzungumza na vijana.


“…Wanakuwa wengi lakini sio wote watakuelewa naamini walau wawili watatu watazingatia na kufika zahanati ili kupata elimu zaidi, hiki sio kipindi cha wazazi kuwaogopa vijana wao lazima wawaweke wazi ili kuwaokoa,” amesisitiza Mwalimu Mbwambo.


Rukia Mwamba, CHW wa Kata ya Mikese Kijiji cha Fulwe Wilaya ya Morogoro Vijijini Mkoa wa Morogoro amesema moja ya majukumu yake ni kuwafikia vijana kwenye vijiwe vyao ingawa sio rahisi kwa kuwa wengine bado hawajaelewa kuhusu elimu sahihi ya afya ya uzazi kwa vijana.


“Nawatembelea kwenye vijiwe vya bodaboda, wanapokuwa kwenye michezo hasa mpira wa miguu, mwanzoni haikuwa rahisi vipingamizi vilikuwa vingi lakini sijakata tamaa, nawafuata nikiwa na mipira ya kiume (Condom) na dawa za uzazi wa mpango.


“Namashukuru Mungu kiasi sasa wananielewa nikikuta kijiwe cha bodaboda wapo vijana wasiopungua watano nawafuata na kuwaeleza sio wote wanaonisikiliza wengine wanaondoka au wananifukuza ila sijakata tamaa naamini ipo siku watanielewa na nitawaokoa,” amesema Mwamba anayefanyakazi na mradi wa Afya kwa Vijana unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya.


Amesema anatamani kupata wasaa wa kuwaelimisha vijana wakiwa kwenye makundi makubwa hasa ya ngoma ‘vigodoro’ zinazochezwa usiku.


Mwajuma Dhahabu ni Muuguzi Mkunga wa Zahanati ya Fulwe Mikese, amesema kwa zaidi ya miaka mitano aliyofanyakazi kwenye zahanati hiyo, hajawahi kuona hamasa ya vijana kufuata huduma.


“Nipo hapa Fulwe Mikese kwa muda mrefu kidogo, vijana hawana mwitikio kabisa ila baada ya Serikali kutuletea Mradi wa Afya kwa Vijana chini ya Umoja wa Ulaya, sisi watoa huduma tulipata mafunzo ya huduma rafiki kwa vijana.


“Kabla ya kupata elimu ya huduma rafiki kwa vijana Oktoba 2022 kwa mwezi tulikuwa tunapokea vijana vijana wawili mpaka watatu, baada ya sisi kupata elimu tumekuwa mabalozi wazuri vijana wanatuamini na wanakuja zahanati kupata elimu na huduma rafiki kwa vijana.

 “Kila baada ya muda wa kazi kuanzia saa 9:30 mpaka saa 11:00 jioni tumejijengea utaratibu wa muuguzi mwenye mafunzo kubaki kituoni kuwasubiri vijana wanaotoka shule, pia tunatoa huduma za ‘week end clinic’ kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi… idadi ya vijana imeongezeka sasa tunapokea vijana 80 hadi 200 kwa mwezi.


Anaendelea kueleza kwamba wanashiriki nao kwenye michezo mbalimbali ukiwemo mpira wa miguu, tunazungumza lugha yao vijana wanafunguka wanaeleza changamoto zao kuhusu afya ya uzazi.”


Kwa mujibu wa Dhahabu, licha ya ongezeko la idadi ya vijana kwenye kituo hicho bado, wengi hawajafikiwa na elimu hiyo hivyo ameomba serikali ya kijiji kushirikiana na watoa huduma za afya kwa vijana na uzazi kwa ujumla kusambaza elimu hiyo kwenye ngoma za utamaduni, ‘vigodoro’ na unyagoni.


“Kipindi cha mavuno ngoma zinakuwa nyingi na zinafanyika kwenye jamii… viongozi wa kijiji wanauwezo wa kuamuru pale kwenye ngoma ikifika wakati fulani mtoa huduma rafiki kwa vijana apewe dakika kadhaa za kuzungumza na vijana kuhusu afya zao hiyo itaongeza ufikiwaji wa elimu kwa vijana,” amesisitiza Dhahabu.

 
Kwanini Afya kwa Vijana?


Mratibu wa Huduma za Afya ya Uzazi Mkoa wa Morogoro, Catherine Madaha amesema Mradi wa Afya kwa Vijana chini ya ufadhili wa Umoja wa Ulaya ni mkombozi kwa janga la mimba za utotoni mkoani hapa alizosema kwa kiasi kikubwa zinachangiwa na desturi na tamaduni za ngoma kwa wenyeji wa mkoa huo .

Anasema mkoa huo umeshika namba tatu kwa mikoa yenye mimba za utotoni nchini Tanzania hivyo ni busara za serikali kupitia Wizara ya Afya kupeleka mradi huo Morogoro hasa ukifanyakazi kwenye Halmashauri nne za Morogoro Vijijini, Gairo, Ulanga na Malinyi ambapo kila halmashauri inahudumia vituo saba vya afya.


Madaha anataja halmashauri mbili zenye idadi kubwa ya mimba za utotoni kwa Mkoa wa Morogoro kuwa ni Malinyi na Gairo huku akibainisha kwamba Mradi wa Afya kwa Vijana uliofadhili Umoja wa Ulaya umeasaidia kuongeza huduma za afya ya uzazi kwa vijana.


“Wakati mradi unaanza mwaka 2022 hata matumizi ya uzazi wa mpango kwa vijana yalikuwa chini ambapo Desemba mwaka 2022 matumizi ya njia za uzazi mpango kwa vijana yalikuwa asilimia 65.5 lakini takwimu za Desemba mwaka 2023 tulifikia asilimia 73 ukiangalia unaona kuna ongezeko.

 
“Upande wa watumiaji wa njia za muda mrefu wa njia za uzazi wa mpango zimeongezeka kutoka asilimia 56.1 mpaka asilimia 62.1 ongezeko hilo limetokana na kuwepo kwa watoa huduma waliofundishwa kupitia mradi wa Afya kwa Vijana unaona jamii imeamka hasa vijana wanajiamini kufika kituoni kupata huduma bila wasiwasi,” anasema Madaha.


Mratibu huyo anaushukuru Umoja wa Ulaya na kuuomba uendeleze mradi huo hata kwa halmashauri nyingineili kuutoa mkoa huo kwenye mstari mwekundu wa mimba za utotoni hapa nchini.

No comments:

Post a Comment

Pages