July 19, 2024

DKT. SELELA LEO KUKABIDHI BENDERA NA KUIAGA TIMU YA TANZANIA ITAKAYOSHIRIKI MICHUANO YA OLIMPIKI JIJINI PARIS, UFARANSA

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Suleiman Selela kesho anatarajiwa kuikabidhi bendera na kuiaga timu ya Taifa itakayoshiriki katika  Michezo ya Olimpiki ya Majira ya joto  inayoanza siku ya Ijumaa Julai 26 hadi Jumapili Agosti 11, 2024 jijini Paris na miji mingine 16 nchini Ufaransa.

Makamu wa rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) Henry Tandau amesema hafla hiyo ya kukabidhi bendera na kuwaaga jumla ya wanamichezo 15 wataoiwakilisha Tanzania katika michuano hiyo ya Olympiki mwaka huu, itafanyika kuanzia saa tatu asubuhi katika Uwanja wa Benjamin William Mkapa jijini Dar es salaam.

Tandau amesema katika  toleo hili la 33 la Michezo  hiyo ya Olimpiki, kikosi cha Tanzania kitakuwa na nahodha mkimbiaji Alphonce Felix Simbu ambaye pamoja na mkimbiaji mwenzie Gabriel Geay  watashiriki katika mbio za Marathon kwa wanaume.

Ametaja wengine kuwa ni  wanariadha Jackline Juma Sakilu na Magdalena Crispin Shauri,  ambao watashiriki michuano ya Marathon kwa wanawake.

Pia amewataja  waogeleaji wawili, Sophia Anisa Latiff atakayechuana mita 50 freestyle, kategoria ya wanawake na Collins Phillip Saliboko atakayecheza mita 100 freestyle kwa wanaume.

Mwanamichezo wa saba ni Andrew Thomas Mlugu, atayeshiriki katika mashindano ya mchezo  wa Judo,

Tandau amesema timu hiyo itaambatana na makocha 3 wa fani hizo tatu za michezo, daktari wa timu, Mwambata wa Mawasiliano na Habari pamoja na maafisa wawili kutoka TOC.

Zaidi ya wanamichezo 10,500 kutoka mataifa 206 wanatarajiwa kushiriki katika matukio 329, na fani 45  tofauti za michezo. Kwa mara ya kwanza kila jinsia  itawakilishwa na wanamichezo 5,250.

Katika michezo hiyo  kutakuwepo na Breaking (aina ya breakdancing) ambayo itakuwa ikichezwa kwa mara ya kwanza kwenye Olimpiki, pamoja na kuteleza kwa ubao (Skateboarding) kupanda ukuta na kuelea  kwenye mawimbi (surfing) makubwa ya bahari.

Tanzania ilishiriki kwa mara ya kwanza katika Michezo ya Olimpiki mwaka 1964 huko Tokyo, Japan, na toka wakati huo  imepeleka wanariadha kushiriki katika kila Michezo ya Olimpiki ya Majira ya joto isipokuwa ile iliyosusiwa mwaka 1976,  ila haijawahi kushiriki Michezo ya Olimpiki ya Majira ya baridi.

Mwaka huo wa 1976, nchi 29, nyingi zikiwa za Kiafrika, zilisusia Michezo ya Olympic iliyofanyika Montreal, Canada, baada ya  Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) kukataa kuipiga marufuku New Zealand, baada ya timu yake ya kitaifa ya raga (rugby)  kuzuru Afrika Kusini mapema mwaka 1976 kinyume na wito wa Umoja wa Mataifa wa michezo ulioiwekea Afrika Kusini vikwazo kutokana na msimamo wao wa ubaguzi wa rangi.

Kamati ya Taifa ya Olimpiki ya Tanzania iliundwa mwaka 1962, ili kushiriki michezo ya Jumuiya ya Madola mjini Glasgow, Scotland.  Mwaka 1968  TOC ilitambuliwa rasmi na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC).

No comments:

Post a Comment

Pages