NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu), Ummy Nderiananga (kushoto) akiteta jambo na Mkurugenzi Mwanzishilishi wa Shirika la EMEDO, Editrudith Lukanga leo wakati wa maadhimisho ya siku ya kuzuia kuzama maji duniani.
Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wakionesha namna ya kumuokoa mtu aliyezama maji na mavazi maalum ya kuingia majini kwa ajili yauokozi.
Na Irene Mark
WAKATI leo Julai 25, 2024 Dunia ikiadhimisha siku ya kuzama maji, Shirika la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo (EMEDO), limeiomba Serikali kuondoa kodi ya jaketi okozi.
EMEDO imeomba hayo leo pembezoni mwa ufukwe wa Kawe jijini Dar es Salaam, yalipofanyika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya Kuzuia Kuzama Maji yaliyoongozwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu). Ummy Nderiananga.
Akizungumza kwenye maadhimisho hayo, Mkurugenzi na Mwanzilishi wa EMEDO, Editrudith Lukanga, amesema kazi ya shirika lake ni kutoa elimu ya uokozi kwa wavuvi na jamii inayoishi pembezoni mwa Maziwa na Bahari.
“Vifo kwa kuzama maji ni muuaji aliyesahaulika, takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonesha watu zaidi 200,000 wanakufa kwa kuzama maji duniani kote kwa mwaka… kati yao asilimia 90 wapo kwenye nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.
“EMEDO tunatoa elimu lakini wavuvi wanashindwa kumudu gharama za vifaa hivyo hasa jaketi okozi hivyo kushindwa kupambana na vifo vya kuzama maji, sisi tunasema kuzama maji kunazuilika tuchukue tahadhari,” alisema Lukanga.
Naibu Waziri Nderiananga ameipongeza EMEDO kwa kuliona eneo la uvuvi na kulifanyia kazi huku akiahidi kufikisha kilio cha kupunguzwa ama kuondolewa kodi kwenye ngazi zinazohusika.
Kwa niaba ya serikali naibu waziri huyo ameahidi kuendelea kushirikiana na EMEDO kuhakikisha wanapunguza ama kumaliza vifo vinavyotokana na kuzama hapa nchini.
“Pamoja na juhudi za shirika hili na serikali, nawaomba vijana mnaofanya shughuli za uvuvi ama usafirishaji kwa njia ya maji jiepusheni na matumizi ya pombe ama vilevi vingine mnapoingia kwenye maji,” amesema Naibu Waziri Nderiananga.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kinondoni, Stella Msofe aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo, aliwataka viongozi wa Jumuiya za Watumia Maji (BMU), kuunda vikundi vitakavyokopeshwa mtaji kupitia asilimia 10 ya mapato ya wilaya hiyo.
“Halmashauri yetu ya Kinondoni inakusanya zaidi ya sh. bilioni 67 kwa mwaka ambayo inatengwa asilimia 10 ya fedha hizo kwaajili ya kuwakopesha vijana na wanawake walio kwenye vikundi ili kuwainua kiuchumi.
“Ninyi hapa Kawe ni wananchi wetu, nakuomba kiongozi wa BMU hakikisha wanapatikana wavuvi na wafanyabaishara nyingine waliopo hapa ambao mnaaminiana dirisha litakapofunguliwa mpate fedha za kukuza biashara na shughulj zenu za kiuchumi,” amesema Msofe.
Mwakilishi wa Shirika la RNLI lenye maskani yake nchini Uingereza, Rachel Roland amesema wataendelea kushirikiana na EMEDO kwa rasilimali fedha,vifaa na utaalam ili jamii ielewe na kuchukua tahadhari ya kupoteza maisha kwa kuzama maji.
No comments:
Post a Comment