July 16, 2024

KUELEKEA OLIMPIKI YA PARIS 2024: TOC ‘yauweka mtegoni’ mkataba wa udhamini RT

Yaigomea RT kuwavalisha wanariadha vifaa vya Xtep, yasema hawana mamlaka hayo kisheria
RT yakiri kosa, lakini yasema: Liwalo na Liwe, hatuko tayari kuuvunja mkataba wetu
Wanariadha wabaki njiapanda, wakiri kuvutiwa na mamilioni ya Bonasi ya Xtep


NA MWANDISHI WETU


WAKATI homa ya Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Joto itakayoanza kutimua vumbi Julai 26 na kumalizika Agosti 11 mwaka huu jijini Paris, Ufaransa likizidi kupanda, mtanziko umeibuka nchini baina ya Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) na Shirikisho la Riadha Tanzania (RT).

TOC ndio mratibu wa ushiriki wa Tanzania katika michezo hiyo itakayofunguliwa na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, ambako Tanzania itawakilishwa na wanamichezo saba tu, kutoka katika michezo mitatu ya Riadha (wakimbiaji wanne), Judo (mchezaji mmoja) na Kuogelea (waogeleaji wawili).

Katika riadha, Tanzania itawakilishwa na Alphonce Simbu na Gabriel Geay (marathoni wanaume), Jackline Sakilu na Magdalena Shauri (marathon wanawake), judo itawakilshwa na Andrew Mlugu, huku Collins Saliboko na Sophia Latiff wao wakibeba bendera ya uogeleaji (wanaume na wanawake).

Tayari nyota hao wanaendelea na mazoezi yao ya mwisho yanayosimamiwa na vyama vya michezo yao au kwa udhamini wa TOC na Olympic Solidality (OS), lakini tayari mtanziko umeibuka unaoitishia ari ya ushiriki ya baadhi yao, idadi yao na hata ustawi wa mafanikio yao na michezo kwa ujumla.

TOC ‘yautega’ mkataba wa RT na Xtep wenye mamilioni ya bonasi, vifaa

Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) mwaka jana lilisaini kandarasi ya ufadhili na udhamini wa vifaa vya michezo na pesa za bonasi na Kampuni ya Xtep ya China, unaoitaka kampuni hiyo kuzivalisha timu zote za riadha zitakazoshiriki mashindano ya kimataifa, pamoja na bonasi ya fedha kwa washindi.

Kupitia mkataba huo, Xtep mwaka jana ilitoa mafungu 50 ya vifaa vya michezo ikiwemo mavazi na viatu, ambako mwaka huu inaipa RT mafungu 250 ya vifaa hivyo, pamoja na bonasi ya Dola 50,000 kwa mshindi wa medali ya dahahabu, Dola 30,000 medali ya fedha na Dola 20,000 kwa medali ya shaba.

Wiki mbili kuelekea ufunguzi wa Olimpiki ya Paris, Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi – kupitia mahojiano maalum, ameweka wazi kwamba hawautambui mkataba huo na kwamba jukumu la kuwavalisha wachezaji wanaoshiriki Olimpiki na Michezo ya Jumuiya ya Madola ni la TOC, kupitia mdhamini wao Asics.


 “Kwa kifupi jibu la swali lako ni Hawana nafasi kabisaa. Michezo ya Olimpiki siyo ya Judo, Riadha na Kuogelea tu, kuna michezo zaidi ya 30 uitakayoshiriki Paris 2024,” anaanza kujibu Bayi alipoulizwa kama kuna nafasi yoyote ya RT kumtumia mdhamini wao Xtep katika Olimpiki 2024 na kuongeza:

“Kwa mfano Tanzania iwe na wawakilishi wa michezo zaidi ya mitano, kwa hiyo kila mchezo uwe na udhamini wa vifaa vyake watakavyotumia katika Michezo ya Jumuiya ya Madola au Olimpiki, hiyo itakuwa timu ya Taifa au itakuwa vurugu?

“Kwa Katiba ya TOC na ‘Olympic Charter,’ mamlaka ya kupeleka na kuvalisha timu ya kushiriki Jumuiya ya Madola au Olimpiki ni ya Kamati za Olimpiki na si vinginevyo. Kabla ya vyama/mashirikisho ya michezo kuingia mikataba yao, nashauri wasome Katiba ya TOC na ‘Olympic Charter.’

“TOC na IOC inaheshimu utumiaji wa viatu vya mashindano (spikes/marathon race shoes) kwa wanamichezo wenye mikataba yao binafsi, lakini siyo training shoes na mavazi wakati wa michezo ya Olimpiki.

“Vyama vya michezo vina Mashindano yao Kimataifa, (Kanda, Bara na Dunia), ambavyo wanaweza kusaini mikataba kwa ajili ya mashindano hayo tu, sio Olimpiki na Jumuiya ya Madola. Natoa rai kwa vyama vya michezo, wanaposaini mikataba na makampuni ya vifaa vya michezo wasihusishe michezo ya Jumuiya ya Madola na Olimpiki.

Alipoulizwa kuhusu kambi ya pamoja ya wawakilishi wote wa Olimpiki 2024, Bayi akajibu; “TOC haitakuwa na kambi kama ilivyozoeleka, kwani wachezaji wote waliofikia viwango vya Paris 2024 wa Riadha wawili wa kiume (Simbu na Geay) walikuwa kwenye udhamini mzito wa Olympic Solidarity.

“Wanariadha wa kike wawili (Magdalena na Jackline) waliofikia viwango vya kushiriki Paris 2024 watakuwa na udhamini wa TOC mpaka Julai 30, 2024.

“Wachezaji wengine (Mlugu anayecheza judo) na (Collins - kuogelea), wao walikuwa kwenye udhamini wa Olympic Solidarity na World Aquatics, isipokuwa Sophia Latiff, ambaye licha ya kutofikia viwango, alipewa nafasi ya upendeleo (Universality),” anamaliza Bayi

RT: Hatuko tayari kuvunja mkataba na Xtep

Alipotafutwa Kaimu Katibu Mkuu wa RT, Wakili Jackson Ndaweka, alikiri wazi kwamba uhalali wa kuvalisha wanamichezo wanaoshiriki Olimpiki ni wa TOC, lakini isingekuwa rahisi kwao kukataa udhamini wa Xtep, uliokuja miaka 16 tangu walipovunjiwa mkataba kwa mtindo huo huo mwaka 2008 kuelekea Olimpiki ya Beijing, China.


“Kwa nafasi yake (Bayi) kama Katibu wa TOC, aliwahi kutuandikia barua RT kuuliza juu ya uwepo wa mkataba baina yetu na Xtep, nilimjibu kwa maandishi kuwa ni kweli na nikaenda mbali zaidi kwa kumueleza moja ya matakwa ya kimkataba ni kutumia vifaa vyao katika Olimpiki.

“Na nikamueleza kwamba kwa zaidi ya miaka 16 tangu TOC waliposababisha mkataba wetu na Kampuni ya Li Ning kuvunjika baada ya kuvalisha wanamichezo wetu vifaa vya Kampuni ya Puma, RT haikuwa na mdhamini wa vifaa, jambo ambalo limetupa wakati mgumu sisi kama shirikisho na Serikali, ambao tulilazimika kununua vifaa.

“Kupitia barua yangu hiyo kwake, nikaiomba TOC ituruhusu wanariadha wetu wavae vifaa vya Xtep, ili sio tu kumlinda mdhamini wetu ambaye ataendelea kutupa vifaa vata baada ya Olimpiki, bali kutopoteza bonasi kubwa zilizoko mezani kwa wanariadha wetu iwapo watarudi na medali katika Olimpiki 2024.

“Xtep wameweka mezani Dola 50,000 kwa mwanariadha atakayetwaa medali ya dhahabu, Dola 30,000 kwa medali ya fedha na Dola 20,000 kwa medali ya shaba, hizi ni bonasi ambazo hata ukiwatafuta kina Simbu, Geay na wengineo, watakwambia wanavyopambana kupata pesa za ushindi na bonasi hizo.

“Sasa kama TOC watashikiria msimamo kwamba wanaraiadha wetu watavalishwa vifaa vya Asics na sio Xtep, sisi kama shirikisho tutachukua hatua. Wanayo mamlaka ya kuwavalisha Assics, lakini sisi ili kuondoa hatari hiyo ya kuwavalisha vifaa vya mpinzani wa mdhamini wetu.

“Hatutaruhusu wala kukubali watuvunjie mkataba ambao una manufaa kwetu hata baada ya Olimpiki, tutapata sapoti gani kutoka kwao kupitia mdhamini wao baada ya Olimpiki? Wachezaji watanufaikaje na kutumia vifaa vya mdhamini wao baada ya mshindano? Hapa ndipo tunaposema tutachukua hatua.

“Sisi kwa kweli hatutasita kuchukua hatua, hawajatuambia kwa maneno wala maandishi kwamba watalazimisha wanariadha wetu kuvaa Asics, lakini ikitokea wakatutaarifu, msimamo wetu wachezaji watavaa Xtep, tukishindwa njia zote, tutakuwa tayari kuwazuia wanariadha wetu Kwenda Olimpiki,” anasema Ndaweka.

Alphonce Simbu afunguka

Kwa upande wake, Simbu alikiri kupata kigagaziko kuzungumiza mtanziko huo, ambao anaamini unahusisha mamlaka ambazo zinapaswa kukaa kwenye meza ya mazungumzo ili kupata suluhu itakayowapa fursa ya wao kushindana wakiwa kwenye mavazi ya Xtep, kwani wana ari kubwa ya kutwaa Dola za bonasi


“Kimantiki RT ndio yenye wachezaji na mikataba mingi inasainiwa na RT, na kama Xtep ni mdhamini wa shirikisho, basi ni bora wakatuacha tukatumia vifaa vyao, ingawa pia natambua kwamba wenye mamlaka ya kutuvalisha ni kamati na sio shirikisho.

“Wasiwasi wangu ni kuja kuturudisha nyuma kule, ambako TOC na RT waligonganisha wadhamini, likaishia kwa kuvunjika mkataba wa shirikisho ambaye ndiye mlezi wa muda wote wa wanariadha. Ningekuwa na uwezo ningeziweka mezani TOC na RT kuhakikisha hili linamalizwa kwa maslahi mapana ya riadha.

“Kinachoweza kutuumiza zaidi sisi ni kushiriki Olimpiki hali ya kuwa tumeondolewa ahadi ya bonasi ya Xtep, itatushusha morali yetu hasa ukizingatia wametupa ahadi nono zinazotuongezea ari ya upambanaji, wakati hatujui tutanufaikaje kwa udhamini wa Asics, itatubidi tuulize na tuambiwe kabla hatujaondoka kwenda Paris,” anamaliza Simbu.

Wadau nao watoa ya moyoni

Kwa upande wake Kocha wa Kimataifa wa Riadha nchini, Boniface Kimmisha, anasema anaona sintofahamu hiyo inakuja kutokana na mawasiliano hafifu kati ya Kamati ya Olimpiki Tanzania na vyama wanachama wake.

Kimisha anasema, suala hilo linapaswa kuangaliwa kwa mapana marefu na kwa maslahi ya pande zote, isije ikatokea kama ilivyotokea Olimpiki ya Beijing 2008.

"Mimi kama mdau na ambaye nalifahamu vema sakata la 2008, najua TOC ndio wenye mashindano hayo, lakini inapaswa pande zote zikae pamoja kulitatua hili, kwani endapo na mkataba huu Xtep utavunjika, RT ndio itaathirika, kwani Olimpiki inakuja kila baada ya miaka minne, lakini RT wao wana matukio kila siku," anasema na kuongeza;

“TOC inapaswa kuangalia kwa uhai wa vyama wanachama wake kwa maslahi mapana ya maendeleo ya michezo nchini, kwani vyama kupata ufadhili si jambo rahisi hasa ukizingatia RT toka ilipovunjiwa mkataba na Li Ning imesota hadi mwaka jana kuja kuwapata Xtep.

Naye Mjumbe wa Chama cha Riadha Mkoa wa Dar es Salaam (DAA), na Kocha wa siku nyingi, Kapteni Mstaafu Lucas Nkungu, anasema hatamani kuona tukio la 2008 likijirudia tena, kwani itakuwa pigo kwa mchezo wa Riadha na kuomba Serikali kupitia Wizara yenye dhamana, kuingilia kati na kuhakikisha muafaka unapatikana.



No comments:

Post a Comment

Pages