July 21, 2024

Wanafunzi na Wasomi waonywa matumizi ya dawa za kulevya

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni amewaonya wanafunzi walioko mashuleni,vyuoni na taasisi nyingine za elimu kuacha na kutojihusisha na matumizi ya dawa za kulevya kwani kushiriki katika matumizi ya dawa hizo itapelekea nchi kupoteza nguvu kazi ambayo inategemewa katika kujenga taifa huku akiitaka jamii kushirikiana na serikali katika vita dhidi ya dawa za kulevya.

 


Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara baada ya kufungua Kikundi cha Ujasiriamali kilichopo Visiwani Zanzibar ambacho kinajumuisha makundi mbalimbali ikiwemo kundi la vijana ambalo limekua likiathirika na matumizi ya dawa za kulevya ambapo wamekua wanatumia kwa njia ya kuvuta puani,kuvuta mdomoni na kujidunga sindano.

 

‘Ni muhimu kwa jamii nzima kushikamana ili kuweza kupambana na matumizi ya dawa za kulevya,tafiti zinaonyesha sasa janga la matumizi ya dawa za kulevya limehamia kwa wanafunzi ambao wengine wana digrii zao lakini wamejiingiza katika uraibu wa dawa za kulevya,jambo hili linahatarisha uhai wa taifa kwani vijana ni nguvu kazi ya taifa lolote lile duniani,sisi kwa upande wa serikali tumeunganisha nguvu ya pamoja katika kudhibiti uingiaji wa dawa za kulevya na wito wangu kwa wazazi na wanajamii kuhakikisha wanashirikiana na serikali katika kudhibiti janga hilo’ amesema Waziri Masauni.

 

Waziri Masauni pia amezungumzia matendo ya udhalilishaji ikiwemo ulawiti,ubakaji,ushoga ambayo yanaendelea kukithiri huku jamii pamoja na familia wakiendelea kuwaficha watu wenye kujihusisha na matendo hayo ambapo ameiasa jamii kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi waonapo dalili za udhalilishaji wa kijinsia kwa watoto na makundi mbalimbali.

 

‘Kuna mmomonyoko wa maadili unaopelekea matukio ya ukiukwaji wa maadili hayo ikiwemo unyanyasaji wa kijinsia,ubakaji,ulawiti na ushoga;mambo hayo hayajaisha katika jamii yetu na ni muhimu kwa jamii nzima kushikamana ili kupambana na majanga haya,na kumekua na desturi kwa baadhi ya watu wanaofanya matendo ya ubakaji na ulawiti hususani ya watoto tunawakumbatia na kuwaficha,imefikia hatua mtu amethibitika kufanya ulawiti lakini wanamficha katika kuhakikisha yule mtuhumiwa aendi kwenye mikono ya sheria hiyo sio sawa.’ Aliongeza Waziri Masauni

 

Taarifa  zinabainisha walevi wa uraibu wa dawa za kulevya wamekuja na mtindo wa kutumia dawa za kutibu binadamu kama mbadala wa dawa za kulevya huku wakichukua dawa aina ya methamphetamine ambayo waraibu uchukua dawa hiyo kuisaga na kuiweka kwenye kijiko huku mshumaa ukitumika kuipasha na mwisho mraibu huvuta moshi unaotokana na uunguaji wa dawa hiyo.

 

No comments:

Post a Comment

Pages