Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda akizungumza wakati wa kufunga Mkutano wa kwanza wa Elimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maadhimisho ya mwaka wa elimu wa Umoja Afrika uliofanyika jijini Arusha tarehe 12-15 Agosti, 2024.
Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda amefunga rasmi Mkutano wa kwanza wa Elimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maadhimisho ya mwaka wa elimu wa Umoja Afrika uliofanyika jijini Arusha.
Akizungumza katika hafla hiyo Prof. Mkenda amezitaka nchi wanachama kuandaa mpango kazi utakaoonesha namna bora ya kutekeleza maazimio yaliyotokana na mkutano huo ili kuhakikisha yanafanyiwa kazi kwa ukamilifu.
Pia ametaka kuhakikisha mafanikio yote yaliyopatikana katika maadhimisho ya mwaka wa elimu wa AU yanasherehekewa na kutafakari jinsi ya kuwa na mifumo bora zaidi ya utoaji elimu kwa vijana na hivyo baada ya miaka miwili mkutano ujao uone matunda ya mkutano huo.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Kisekta na Waziri wa Elimu na Mafunzo wa Sudan Kusini Mhe. Awut Deng Achuil alıtoa wito wa kuchukua hatua na kujitoa zaidi ili kuhakikisha malengo na maazimio ya mkutano yanatekelezwa kwa vitendo na ameipongeza Tanzania kwa kuwa mwenyeji pamoja na Sekretarieti ya EAC na nchi wanachama kwa kuandaa mkutano huo kwa mafanikio makubwa.
Mkutano huo wa kwanza na wa aina yake kufanyika katika ukanda wa Afrika Mashariki ulijumuisha wadau mbalimbali wa elimu kutoka Serikalini na sekta binafsi umejadili na kuweka mikakati mipya ya kukabiliana na fursa na changamoto zilizopo katika sekta ya elimu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na Bara la Afrika kwa ujumla. Kufanyika kwa mkutano huo ni utekekezaji wa maamuzi ya Mkutano wa 15 wa Baraza la Kisekta la Jumuiya ya Afrika Mashariki la Elimu, Sayansi na Teknolojia, Utamaduni na Michezo; na Umoja wa Afrika.
Mkutano huo wa elimu na Maadhimisho uliwakutanisha Mawaziri wa Elimu kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Wageni mashuhuri wakiwemo Wawakilishi wa Nchi mbalimbali kama Jamhuri ya Watu wa China; Wakuu wa Mashirika na Taasisi za Kikanda na Kimataifa zinazojihusisha na agenda ya kuendeleza sekta ya elimu kama vile Umoja wa Ulaya (EU), Umoja wa Afrika (AU), Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS), Taasisi ya Maendeleo ya Elimu Afrika (ADEA), Taasisi ya Haki Elimu, na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ).
Mkutano huo pia uliwakutanisha Wadau wa elimu zaidi ya 600 kutoka Nchi Wanachama, Taasisi za elimu, Mashirika yasiyo ya kiserikali, Sekta binafsi, Mashirika ya kimataifa, Asasi za kiraia waliokutana kutathmini, kubadilishana uzoefu wa mbinu bora za uendelezaji wa sekta ya elimu. Mkutano huo uliandaliwa na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Nchi wanachama, taasisi zisizo za kiserikali , wadau wa maendeleo na bhana vya elimu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ulianza tarehe 12 hadi 15 Agosti 2024.
No comments:
Post a Comment