Akizungumza na wanahabari Jijini humo wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Mkutano huo Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema mkutano huo utaleta pamoja wadau wa kimataifa katika sekta ya madini hivyo kuendelea kutangaza sekta ya Madini ya Tanzania.
Amebainisha kuwa mkutano huo utahudhuriwa na wadau mbalimbali toka nchi tofauti Duniani wakiwemo Wawekezaji wa Madini, Watafiti wa Madini, Wachimbaji, Wawakilishi wa Serikali, Viongozi kutoka Mataifa ya kigeni, Wawakilishi na Mabalozi wa nchi mbalimbali kwa pamoja wakilenga kujadili fursa za kipekee za Uwekezaji katika uongezaji thamani madini, uchimbaji na hususan wakati huu ambapo mahitaji ya madini muhimu yanaongezeka duniani.
“Ni
maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba madini yote
yanayochimbwa hapa nchini ili kuongeza mchango wa Sekta katika Pato la
Taifa, kulinda na kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania, kuchochea
ukuaji wa teknolojia katika Sekta, kuchochea maendeleo ya jamii na
uchumi kwa ujumla” amesema Waziri Mavunde na kuongeza kuwa,
“Kaulimbiu
ya mkutano huu ni, Uongezaji Thamani Madini kwa Maendeleo ya Kijamii
na Kiuchumi hivyo mkutano huo utakuwa jukwaa muhimu la majadiliano ya
kina yatakayotoa mwelekeo mpya kwa sekta ya madini nchini, huku ukiibua
fursa mpya za uwekezaji na uhamishaji wa teknolojia.
Hata
hivyo amesema, Mkutano huo pia unatarajiwa kuwa fursa ya kipekee kwa
washiriki kufahamu Sera za Madini za Tanzania, vivutio vya uwekezaji, na
mipango ya serikali ya kuboresha mazingira kwa ajili ya kuvuna madini
kwa maendeleo endelevu.
Kwa
upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo
amefafanua kuwa mkutano huo utakuwa msingi wa kujenga uwezo na
uhamishaji wa teknolojia kupitia majadiliano ya kina ya kitaalamu na
mawasilisho ambayo yatatoa mwelekeo mpya kuhusu jinsi ya kuboresha
sekta, pamoja na kutafuta fursa mpya za kuongeza thamani ya madini.
“Mkutano
huu pia utatoa fursa za uwekezaji kwa kuvutia zaidi kampuni za utafiti,
uchimbaji, usindikaji na uongezaji thamani madini, na watoa huduma ili
kuchimba na kuongeza thamani madini muhimu na vito vinavyopatikana
Tanzania” ameongeza Mbibo
Nae,
Mtendaji Mkuu wa Chemba ya Migodi Tanzania, Mhandisi Benjamin
Mchwampaka amesema kuwa wao kama Chemba ya Migodi wanaishukuru Wizara ya
Madini kwa kuwachagua kushirikiana kwa pamoja katika kuandaa mkutano
huo.
“Sisi
ndio sauti ya Wawekezaji katika Sekta ya Madini hapa nchini, tunaamini
kuwa mkutano huu utatuongezea ufanisi katika namna ya uendeshaji wa
shughuli zetu za kila siku na mnyororo mzima wa Sekta ya Madini, pia
kupitia ushirikiano huu tunaamini tutakuwa na Mkutano mzuri mwezi
Novemba 2024” amesisitiza Mhandisi Mchwampaka.
Sambamba
na hayo Mkutano huo utaambatana na Usiku wa Madini ambao utahusisha
Maonesho ya Vito yenye lengo la kutangaza utajiri mkubwa wa Tanzania
katika madini ya vito sambamba na tukio la kuwatambua kampuni na
wachimbaji waliofanya vizuri kwa kipindi kilichopo.
No comments:
Post a Comment