DAR ES SALAAM, TANZANIA
WIKI moja tangu walipowaduwaza Azam FC kwa mabao 4-1 katika fainali ya Ngai ya Jamii, Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara (NBC PL), Young Africans, wametanguliza mguu mmoja katika hatua inayofuata ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF CL 2024/25), baada ya kuwaangamiza Vital'O ya Bujumbura, Burundi kwa mabao 4-0 katika mechi ya kwanza raundi ya awali kwenye dimba la Azam Complex jioni ya leo.
Young Africans 'Yanga', walikuwa wageni wa Vital'O katika mechi hiyo, kutokana na Warundi hao kuomba kuutumia uwanja wa Azam Complex kama dimba la nyumbani, ambako Sasa watalazimika kushinda kwa mabao 5-0 wataporudiana na Yanga watakaokuwa nyumbani Benjamin Mkapa Agosti 24.
Mabao ya Yanga leo yamefungwa na Prince Dube, Clatous Chota Chama, Clement Mzize na Stephanie Aziz Ki, ushindi unaowapa uhakika wa kuumana na mshindi wa jumla wa mechi kati ya Sports Club Villa 'Jogoo' ya Uganda na Commercial Bank ya Ethiopia.
Katika mechi ya jioni hii, Commercial Bank 'CBE' ikiwa ugenini jijini Kampala, imechomoza na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji wao hao, ushindi unaowapa matumaini ya kuwang'oa jumla wataporudiana wikiendi ijayo jijini Addis Ababa, Ethiopia.
No comments:
Post a Comment