HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 06, 2025

TMA: Mwezi kupatwa kikamilifu Septemba 7, 2025

Na Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetoa taarifa ya kupatwa kwa mwezi ifikapo Septemba 7, 2025.

Hali ya kupatwa kwa Mwezi hutokea wakati Dunia inapita kati ya Jua na Mwezi na kusababisha kivuli cha dunia kuwa juu ya uso wa Mwezi. 

Kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa leo Septemba 6,2025 
hali hiyo pia hutokea wakati Dunia, Mwezi na Jua vinapokaa kwenye mstari mnyoofu. 

"Kupatwa kwa mwezi kumegawanyika katika aina kuu mbili... ya kwanza ni kupatwa kwa Mwezi kikamilifu (Umbra), hii hutokea wakati Dunia inapofunika mwanga wote wa Jua na kupelekea kivuli kizito (giza) katika uso wa Mwezi.  

"Aina ya pili ni kupatwa kwa Mwezi Sehemu (Penumbra) ambapo Dunia husababisha kivuli hafifu katika uso wa Mwezi. 

"Safari hii Mwezi utapatwa kwa sehemu na kikamilifu, ni tukio  linatarajiwa kuonekana katika maeneo ya Bara la Ulaya, Asia, Australia na Afrika. 

"Kwa hapa nchini, hali ya kupatwa kwa Mwezi inatarajiwa kuanza kwa kupatwa kwa Mwezi Sehemu kuanzia pale Jua linapozama hadi saa 2:29 usiku na kufuatiwa na kupatwa kwa Mwezi Kikamilifu kuanzia saa 2:30 hadi saa 3:52 usiku," ilisomeka sehemu ta taarifa hiyo ya TMA.

Taarifa hiyo inafafanua kwamba tukio hili linatarajiwa kuhitimishwa kwa kupatwa kwa Mwezi Sehemu kuanzia saa 3:53 hadi 5:55 usiku. Kwa ujumla hali hii inatarajiwa kudumu kwa saa sita.

"Kwa kawaida, mzunguko wa Mwezi una uhusiano mkumbwa na Kupwa na Kujaa kwa maji baharini. Hali hii inatarajiwa kuongezeka kwa kina cha maji katika bahari wakati wa tukio hilo. 

"Hali hiyo haitarajiwi kuwa na athiri kubwa huku anga likiwa lenye mawingu kiasi na kutoa fursa nzuri ya kuonekana kwa tukio hilo kwa macho," ilisomeka taarifa hiyo ya TMA.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imeahidi  kuendelea kufuatilia tukio hili la kupatwa kwa mwezi na itatoa mrejesho kila inapobidi.


No comments:

Post a Comment

Pages