Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimemtaka aliyekuwa Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman 'OMO', iwapo chama chake kina ubavu wa kushindana na CCM kisubiri Uchaguzi Mkuu ujao mwaka 2030.
Pia CCM kimeyaita madai ya kutaka Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar urudiwe huku OMO akiamini atamshinda Rais Dkt. Hussein Ali Mwimyi alisema hizo ni mbwembwe na maneno ya kujifariji kwa wafuasi wake.
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanziabr Idara ya Itikadi Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis amesema hayo huku akimtaka OMO aachane na stori za Uchaguzi kwa kuwa ukurasa huo umeshafungwa rasmi.
Mbeto alisema inashangaza kukisikia ACT kikidai kuwa kilishinda wakati wananchi wameshampigia kura Rais Dkt. Mwinyi ambaye sasa anaiongoza Serikali ya Mapinduzi na kujipanga kuendeleza maendeleo yanayoonekana.
"Mwambieni OMO aache porojo badala yake aende Ikulu akaape kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibari ikiwa ameshindwa kazi awapishe wenzake washirikiane na Rais Dkt. Mwinyi kuiletea maendeleo Zanzibar " alisema Mbeto.
Katibu huyo Mwenezi aliongeza kusema ACT kiache kuidanganya dunia badala yake kikubali ukweli nguvu za ushindi wa CCM zimetokana na haiba ya ustawi wa Maendeleo yanayoonekana hivi sasa Unguja na Pemba.
"Ile zama ya kusambaza propaganda uchwara kupitia radio vifua na watu kuwadanganya vibarazani imepita. Wananchi hawataki kushabikia siasa za chuki na migawanyiko" alisema.
Mbeto alibainisha madai kuwa uchaguzi ukirudiwa tena Rais Dk Mwimyi hatapata kura asilimia 30, Mbeto ameyaita hayo ni maneno yasioingia akilini na kuaminika.
Alieleza kuwa kwa wakati huu hadithi za uchaguzi mkuu hazina nafasi hata ya kusikilizwa au kufuatiliwa na wananchi, badala yake watu wanaitarajia SMZ izidi kuongeza kasi ya mabadiliko kiuchumi, kisiasa na kijamii.
"Uchaguzi wa Mwaka 1995 wapo waliodai Dkt. Salmi Amour ataondoshwa kabla ya mwaka 2000. Wakasema tena Dkt. Amani Karume hamalizi muda wake. Walipokataa kushirikiana na Dkt. Ali Mohamed Shein Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), iliundwa na kusongambele " alisema mwenezi huyo.


No comments:
Post a Comment