BAO pekee la mshambuliaji wa kimataifa wa Zimbabwe, Prince Mpumelelo Dube, limeipa Young Africans 'Yanga' ushindi muhimu wa 1-0 dhidi ya AS FAR Rabat ya Morocco katika mechi ya ufunguzi wa Kundi B la Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF CL 2025/26).
Bao la Dube lililokuja baada ya ukame wa muda mrefu, limefungwa kunako dakika ya 59 kwa shuti kali baada ya kuwazidi ujanja mabeki wa AS FAR Rabat, hivyo kumtungua mlinda mlango wao na kuipa ushindi huo unaowaweka kileleni mwa msimamo wa Kundi B - ingawa inaweza kuwa kwa muda tu.
Yanga inayonolewa Pedro Goncalves, ingeweza kupata ushindi mnono, kwani ilitawala mchezo kwa asilimia kubwa, lakini ubora wa mlinda mlango wa Wamorocco hao na ubutu na umakini mdogo wa washambuliaji wa Wana Jangwani hao, ukafanya mnyukano kuwa na ukame wa mabao.
Yanga itasubiri hadi saa 3 usiku kujua kama itabaki kileleni mwa msimamo wa Kundi B, au itashushwa, kwani Al Ahly ya Misri watashuka dimbani kuwaalika JS Kabil ya Algeria, mechi itakatoanza saa 1usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Aidha, uongozi wa Yanga ulitumia mechi hiyo kumkabidhi straika aliye majeruhi Clement Mzize tuzo yake ya Goli Bora la Mwaka la Mashindano yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), ambayo alituukiwa wiki jana nchini Morocco na kupokelewa na Rais wa Yanga, Injinia Hersi Saidi, ambaye leo akiwa na Makamu wake Arafat Haji, walimkabidhi nyota huyo.







No comments:
Post a Comment