November 04, 2025

TFF 'yamtimua' Hemed 'Morocco' Taifa Stars, Gamondi kuiongoza AFCON 2026 ‎

‎SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limetangaza kusitisha mkataba wa Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' Hemed Suleiman 'Morocco' na kumteua mu-Argentina Miguel Gamondi kuwa Kaimu Kocha Mkuu atakayeiongoza timu hiyo katika fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2026).

‎Kwa mujibu wa taarifa ya TFF iliyosainiwa na Afisa Habari wake Clifford Mario Ndimbo, usitishaji mkataba huo ni kwa makubaliano ya pande zote mbili na kwamba tayari imezungumza na mwajiri wa Gamondi, Singida Black Stars na kufikia makubaliano ya uteuzi huo. 

‎Fainali za AFCON 2026 zinatarajiwa kuanza kurindima Desemba 21 mwaka huu nchini Morocco na kufikia ukomo Januari 18, 2026, ambako Taifa Stars imepangwa Kundi C la michuano hiyo, linalojumuisha pia timu za Taifa za nchi za Nigeria, Tunisia na Uganda 'The Cranes.'

‎Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo, Tanzania itakata utepe Desemba 23 itapowavaa Tai wa Nigeria 'The Super Eagles,' kabla ya kurudi tena dimbani Desemba 27 kuumana na wapinzani wao wa Ukanda wa Afrika Mashariki, Uganda. 

‎Mechi ya mwisho hatua ya makundi kwa Taifa Stars itapigwa Desemba 30 pale watapowakabili Tunisia, jukumu Kuu la Gamondi aliyewahi kuinoa Yanga kwa mafanikio, litakuwa ni kuhakikisha timu inafanya vema hatua hiyo na kuipeleka kwenye mechi za mtoano.



No comments:

Post a Comment

Pages