Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Kukamilika kwa barabara za Juu (Flyover) Mwanakwerekwe ni sehemu ya matunda ya utekelezaji wa Ilani ya CCM iliyo katika ahadi za Rais Dkt. Hussein Mwinyi.
Akizungumza Mjini Unguja 28 Novemba 2025, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis alisema miundombinu ya kisasa iliyojengwa ni ya thamani kubwa inayohitaji kutunzwa kwani ni kwa ajili ya waTanzania wote na si kwa ajili ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Alisema si tu Flyover bali pia barabara za kisasa zenye taa na njia za waenda kwa miguu imejengwa sanjari na miundombinu yenye hadhi ya kimataifa inayohitaji kutunzwa.
Alisema suala la wivu wa maendeleo lipo kwani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Màpinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi wamefanyakazi kubwa sana kujenga miundombinu.
"Karibuni tumeshuhudia uharibifu wa miundombinu kwa wenzetu Bara" alisema na kuongeza kuwa wivu upo kwani Tanzania inaenda kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuwa na miundombinu ya kisasa inayoenda kuunganisha nchi zingine.
Mwenezi Mbeto alisema Dira ya Taifa ya Uchumi 2050 inataka Tanzania iwe mtoa huduma wa Ukanda mzima wa Afrika baada ya kukamilika ujenzi wa Reli ya Umeme ya Kisasa (SGR) itakayounganisha Ziwa Nyasa na bahari ya Hindi.
"Reli ya SGR itatoka bandari ya Mtwara hadi Ziwa Nyasa na treni ya mizigo itazihudumia nchi za Malawi, Zambia na zingine za ukanda huo" alisema Mbeto na kuongeza kuwa hali hiyo itainua uchumi wa nchi hizo na kuifanya Tanzania kuwa lango la biashara lenye miundombinu ya uhakika.


No comments:
Post a Comment