Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso, ametoa wito kwa watanzania kufuatilia na kuzingatia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ili kusaidia kupanga vema shughuli za kiuchumi na kijamii.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya kamati hiyo TMA, Kakoso alisema mamlaka hiyo imekuwa ikitoa taarifa sahihi na za kuaminika kila siku kupitia vyombo mbalimbali vya habari, hivyo wananchi wanapaswa kuacha kupuuza taarifa hizo muhimu.
Alisisitiza kuwa sekta kama kilimo, biashara na maji zinategemea kwa kiasi kikubwa taarifa za hali ya hewa, na kuongeza kuwa uwekezaji uliofanywa na Serikali umewezesha upatikanaji wa teknolojia za kisasa za utabiri.
Katika ziara hiyo, kamati ilikagua miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa Ofisi ya Kanda ya Mashariki, Kituo cha Tahadhari ya Matukio ya Tsunami pamoja na Kituo cha Taifa cha Uhakiki wa vifaa vya hali ya hewa, ambapo imeelezwa kuwa baadhi ya miradi hiyo inasuasua.
Kutokana na hali hiyo, kamati imeiomba Serikali kuingilia kati ili kuongeza kasi ya usimamizi na kuhakikisha miradi hiyo ya kimkakati inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Makame Mbarawa, alisema Serikali itaendelea kuwekeza katika sekta ya hali ya hewa na kuhakikisha fedha za kukamilisha miradi hiyo zinapatikana kwa wakati.


No comments:
Post a Comment