Wahitimu wa Female Future COHORT 11 (ambao pia ni wafanyakazi wa NMB) walitabasamu mahafali yaliofanyika chini ya udhamini wa NMB, ambako wahitimu 158 kutoka taasisi na kampuni mbalimbali nchini, wakiwemo 15 kutoka NMB, walitunukiwa vyeti kuhitimisha mafunzo yao yaliyotolewa na Chuo cha ESAMI. Mahafali hayo ni sehemu ya Benki hio kusherekea siku ya wanawake duniani yanayoadhimishiwa kila tarehe 8 mwezi wa tatu.
NA MWANDISHI WETU
BENKI ya NMB imeeleza mchango, mipango, malengo na mafanikio katika kujenga Usawa wa Kijinsia Mahali pa Kazi, huku ikisisitiza kuwa uongozi wa kweli hauwezi kufikiwa bila kutambua, kuthamini na kuendeleza Haki za Wanawake na Wasichana.
Benki hiyo imesema iko mstari wa mbele kufanikisha Ajenda ya Kimkakati ya Haki na Usawa wa Kijinsia, iliyoitaja kuwa ni moja ya vipaumbele vyake, huku ikizijivunia programu kadhaa ilizonazo ambazo ni kielelezo cha juhudi za taasisi hiyo za kuwaandaa wanawake kwenye nafasi za uongozi.
Hayo yamesemwa na Afisa Mkuu wa Rasilimali Watu wa Benki ya NMB, Emmanuel Akonaay, wakati wa Mkutano Mkuu wa Uongozi (ALC 2026), ulioandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), uliofanyika sambamba na Mahafali ya Awamu ya 11 ya Programu ya Mafunzo ya Mwanamke Kiongozi (Female Future).
Kongamano la ALC 2026 na Female Future COHORT 11, vimefanyika Jumatano Februari 4 chini ya udhamini wa NMB, ambako wahitimu 158 kutoka taasisi na kampuni mbalimbali nchini, wakiwemo 15 kutoka NMB, walitunukiwa vyeti kuhitimisha mafunzo yao yaliyotolewa na Chuo cha ESAMI.
Akonaay alizitaja baadhi ya program zao zinazolenga kuandaa wanawake katika nafasi za uongozi kuwa ni pamoja na ‘SHE Mentorship Programme’, ambayo inawakutanisha wafanyakazi na wasimamizi kwenye safari ya ajira zao.
Programu nyingine zilizotajwa na Akonaay ni pamoja na Rabobank Future Leadership Programme, CEO Apprenticeship Programme na Women in Management Africa (WIMA), ambazo zimewawezesha kutambulika kitaifa na kimataifa kama Muajiri Anayezingatia Usawa wa Kijinsia.
“Juhudi hizo zimetupatia tuzo mbalimbali ikiwamo ya Muajiri Kinara wa Usawa wa Kijinsia Tanzania kutoka Taasisi ya The EDGE Certified ya Uswisi, pamoja na Ithibati ya Kimataifa ya Mwajiri Kinara wa Mwaka Tanzania (2025-2026), iliyotolewa na Top Employers Institute,” alibainisha Akonaay.
Alifafanua kuwa, NMB imefikia Uwiano wa Kijinsia Katika Ajira kwa kiwango cha asilimia 48 ya waajiriwa wanawake, kwa asilimia 52 ya wanaume, huku akisema wanajivunia ushirikiano wao na Shirika la International Finance Corporation (IFC) kwenye kuendesha mradi wa ‘Ajira Sawa.’
Aliongeza kuwa, mradi huo umelenga kuimarisha ajira, pamoja na kukuza wanawake kitaaluma ndani ya benki, huku akiutaja ushirikiano wao huo kama unaowasaidia katika kuongeza uelewa na kuchukua hatua za kuzuia ukatili wa kijinsia kupitia sera madhubuti za ndani.
Mgeni Rasmi wa Mkutano huo na Mahafali ya Awamu ya 11, alikuwa ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu, aliyeipongeza wadhamini NMB na waandaaji ATE kwa uwezeshaji wa wazo bunifu lililozaa Programu ya Mwanamke Kiongozi na program mpya aliyoizindua ya Girls and Tech.
Alisema, Bunge la Tanzania litaendelea kutunga sheria za kulinda haki na ustawi wa wanawake na wasichana, pamoja na ushiriki wao katika uongozi na kwamba litaendelea kuwa chombo imara kinachosimamia usawa kijinsia kivitendo kwa maendeleo endelevu ya wanawake na jamii kwa ujumla.
“Mmoja wa watetezi nguli wa haki za binadamu duniani kutoka Amerika, amewahi kusema na hapa namnukuu: ‘Kiwango cha ustaarabu wa taifa kinaweza kupimwa kwa kiwango cha elimu ya wanawake wake’, hivyo niwahakikishie kuw bunge letu litendelea kusimamia haki za wanawake kupata elimu.
“Tunatamani kuona wanawake wanashika nyadhifa mbalimbali za uongozi kama vile wakurugenzi, makatibu wakuu, mawaziri, wabunge na hata nafasi za kimataifa, na hili linawezekana katika nchi ambayo ina Rais mwanamke anayefanya vizuri Dk. Samia Suluhu Hassan,” alisema Spika Zungu.
Zungu aliwapongeza wahitimu 158 sio tu kwa kuhitimu mafunzo yao, bali kwa moyo wa upendo uliowasukuma kuchanga Sh. Mil. 35 na kuzikabidhi kwa Heart Team Africa Foundation (HTAF), inayoshirikiano na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), kwa ajili kufadhili matibabu ya moyo kwa watoto wanaotibiwa hapo.
Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa ATE, Bi. Suzanne Ndomba-Doran, alimshukuru Spika Zungu sio tu kwa kuwazindulia Programu Mpya ya Girls and Tech, bali kwa kushiriki Mkutano Mkuu wa Mwaka na Mahafali ya 11 yaliyojumuisha wahitimu 158 wa Awamu ya 11.
Alisema katika kipindi cha miaka 11 ya uwepo wake, Programu ya Mwanamke Kiongozi imewanoa zaidi ya wanawake 642, huku 493 kati ya hao wakiwa ni wahitimu wa Awamu 10 zilizopita, wakiwamo Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawawakilishi Zanzibar wapatao 150.
Bi. Suzanne alibainisha kuwa Mafunzo ya Mwanamke Kiongozi yanalenga kuwaongezea wanawake ubunifu, na kuchochea maendeleo yao, jamii, taasisi wanazofanyia kazi na taifa kwa ujumla, kwani yamekuwa msingi imara katika ujenzi wa jamii yenye usawa na Maendeleo Jumuishi nchini.

No comments:
Post a Comment