Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amehutubia Baraza la Eid Al-Fitr lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Aidha, amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kulinda uhuru wa kuabudu kwa mujibu wa Katiba, huku akionya dhidi ya matumizi mabaya ya uhuru huo yanayoweza kuvuruga mshikamano wa Taifa au kuchochea migawanyiko katika jamii.
Katika hatua nyingine, amepongeza mchango wa viongozi wa dini nchini katika kujenga maadili na kuhimiza mshikamano wa kijamii, akieleza kuwa wamekuwa nguzo muhimu ya kuimarisha utulivu na maadili ya jamii.
Rais Dkt. Samia pia ameitaka jamii kuepuka vitendo, kauli au mienendo inayoweza kuchochea mgawanyiko au kuvuruga umoja wa kitaifa, huku akikemea matumizi mabaya ya uhuru wa kuabudu yanayoweza kuchochea chuki, uhasama au kuvuruga amani ya nchi.
“Tofauti zetu kiimani zijengewe daraja la kuimarisha udugu wa Watanzania na umoja wa Taifa letu,” amesema Rais Dkt. Samia na kuongeza kuwa Serikali itaendelea kulinda uhuru wa kuabudu kwa mujibu wa Katiba, huku akisisitiza umuhimu wa uhuru huo kuendana na uwajibikaji ili kuepusha matumizi mabaya yanayoweza kuhatarisha amani na mshikamano wa Taifa.
Akirejea mafunzo ya kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, Rais Dkt. Samia amesema kipindi hicho kimejenga misingi ya huruma, uvumilivu na kusaidiana, na kutoa wito wa kuyaendeleza mema hayo hata baada ya kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Kwa upande wake, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Dkt. Abubakary Zubery Ally, amesema jamii inapaswa kujenga utamaduni wa kuheshimiana na kushirikiana bila kujali tofauti za imani, akibainisha kuwa mshikamano wa kidini na kitaifa ni nguzo muhimu ya kudumisha amani.
Halikadhalika, ameonya dhidi ya fikra au vitendo vinavyoweza kuleta mpasuko katika jamii, akisisitiza kuwa hakuna nafasi ya migawanyiko katika Taifa lenye historia ya kuishi kwa umoja na amani. Naye, Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Alhaj Nuhu Jabir Mruma, amesema amani na utulivu wa nchi si jukumu la Serikali pekee, bali ni wajibu wa kila Mtanzania.
Ameongeza kuwa ni jukumu la kila mmoja kuchangia kwa vitendo katika kujenga jamii yenye maadili, heshima na uzalendo, akibainisha kuwa msingi wa jamii bora huanzia katika mwenendo wa mtu mmoja mmoja.


.jpeg)
.jpeg)


No comments:
Post a Comment