May 19, 2026

CRDB Bank Foundation na Zuchu Wazindua Jukwaa la “Zuchu – IMBEJU Masterclass”

Lengo ni kuwawezesha vijana wa tasnia ya muziki na ubunifu

Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Mwambapa (kushoto) akifurahia jambo na msanii wa Bongofleva, Zuhura Othman almaarufu kama Zuchu wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la “Zuchu - IMBEJU Masterclass” linalolenga kuwawezesha vijana katika tasnia ya muziki na ubunifu kupitia elimu, mafunzo na fursa za kiuchumi ili kunufaika zaidi na vipaji vyao. PICHA ZOTE NA JUMANNE JUMA.



Dar es Salaam

CRDB Bank Foundation kwa kushirikiana na msanii wa Bongofleva, Zuhura Othman almaarufu kama Zuchu wamezindua jukwaa la “Zuchu - IMBEJU Masterclass” linalolenga kuwawezesha vijana katika tasnia ya muziki na ubunifu kupitia elimu, mafunzo na fursa za kiuchumi ili kunufaika zaidi na vipaji vyao.

Ushirikiano huo unalenga kuwapa vijana elimu ya fedha, mafunzo ya ujasiriamali, usimamizi wa chapa, ujumuishi wa kidigitali pamoja na kuwaunganisha na huduma za fedha zitakazowawezesha kukuza vipaji vyao kuwa biashara endelevu.

Kupitia ushirikiano huu, vijana wa tasnia ya ubunifu watanufaika na mafunzo kutoka kwa wataalamu wa sekta ikiwemo BASATA, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na wadau wa tasnia ya muziki na ubunifu nchini.


CRDB Bank kupitia CRDB Bank Foundation kwa kushirikiana na msanii wa Bongo Fleva Zuchu wamezindua rasmi jukwaa la “Zuchu – IMBEJU Masterclass” lenye lengo la kuwawezesha vijana katika tasnia ya muziki na ubunifu kupitia elimu, mafunzo na fursa za kiuchumi.

Mpango huo unalenga kuwapa vijana elimu ya fedha, mafunzo ya ujasiriamali, usimamizi wa chapa, ujumuishi wa kidigitali pamoja na kuwaunganisha na huduma za kifedha zitakazowawezesha kukuza vipaji vyao na kuvigeuza kuwa biashara endelevu.

Kupitia jukwaa hilo, vijana wa sekta ya ubunifu watanufaika na mafunzo kutoka kwa wataalamu mbalimbali wakiwemo BASATA, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na wadau wengine wa tasnia ya muziki na ubunifu nchini.

Ajira na ukuaji wa uchumi bunifu

Jukwaa hilo linatarajiwa kuongeza ajira na kukuza uchumi bunifu nchini kwa kuwawezesha vijana kutumia vipaji vyao kujenga biashara endelevu na kuongeza mchango wao katika uchumi wa Tanzania.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Zuchu alisema anatarajia kutumia jukwaa hilo kuwasaidia wasanii wachanga, ma-DJ, wanenguaji, mameneja wa wasanii pamoja na watu wengine wanaojihusisha na muziki kupata uzoefu wa mambo muhimu katika safari ya mafanikio.
Alisema kupitia “IMBEJU Masterclass”, washiriki watafundishwa mambo ya kuepuka katika tasnia, namna ya kujiandaa kuwa maarufu pamoja na jinsi ya kusimamia fedha watakazozipata mara watakapofanikiwa katika soko la muziki.

CRDB Bank Foundation yaeleza dhamira yake

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Mwambapa alisema taasisi hiyo ilianzishwa mwaka 2023 ikiwa na dhamira ya kuchochea elimu ya fedha na ujumuishi wa kiuchumi kwa vijana, wanawake na makundi maalumu.

Mwambapa alisema taasisi hiyo inalenga kukuza ubunifu, ujasiriamali, upatikanaji wa masoko na biashara changa za vijana (startups), pamoja na kuwezesha upatikanaji wa mitaji nafuu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.

“Tunafanya haya yote ili kutekeleza dira ya CRDB Bank Foundation ya kuchangia maendeleo endelevu ya uchumi jumuishi, kuchochea ukuaji wa ubunifu, teknolojia na ajira nchini, pamoja na kuleta ustawi katika maisha ya jamii na kukuza pato la taifa,” alisema Mwambapa.

Vijana milioni 1.7 wanufaika

Mwambapa alisema katika kipindi cha miaka mitatu ya programu ya IMBEJU, taasisi hiyo imefanikiwa kuwafikia vijana na wanawake milioni 1.7 katika sekta mbalimbali za kiuchumi.
Aliongeza kuwa zaidi ya shilingi bilioni 23 za mitaji wezeshi tayari zimetolewa kwa vijana na wanawake, huku marejesho yake yakielezwa kuwa mazuri kutokana na uwepo wa elimu ya fedha inayotolewa sambamba na mikopo hiyo.

Uchumi bunifu waendelea kukua

Mwambapa alisema dunia inaendelea kushuhudia ukuaji mkubwa wa uchumi bunifu (Creative Economy), ambao umefungua nafasi nyingi za ajira na biashara kwa vijana kupitia muziki, filamu, fasheni, sanaa za maonesho na uundaji wa maudhui ya kidijitali.
Alitaja wasanii mbalimbali duniani akiwemo Diamond Platnumz, Kanye West, Davido na Beyoncé kuwa mifano ya watu waliofanikiwa kujenga himaya kubwa za kiuchumi kupitia vipaji vyao vya muziki.

Aidha alisema muziki wa Tanzania umeendelea kuvuka mipaka na kupata soko la kimataifa, huku wasanii wa Tanzania wakijaza majukwaa mbalimbali duniani, kuingiza mapato kupitia majukwaa ya kidigitali, kuajiri vijana wengine na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.



Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Foundation, Tully Mwambapa (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na msanii wa Bongofleva, Zuhura Othman almaarufu kama Zuchu.

No comments:

Post a Comment

Pages