Dar es Salaam
Benki ya CRDB imeendelea kuhamasisha matumizi ya kadi na huduma za kidigitali kupitia kampeni yake mpya ijulikanayo kama “Fainali Ndiyo Mpango”, iliyozinduliwa mwezi Machi mwaka huu kwa lengo la kuhamasisha wateja kufanya miamala na manunuzi kwa njia ya kidigitali badala ya kutumia fedha taslimu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Wateja wa Awali na wa Kati wa Benki ya CRDB, Karington Chahe, amesema kampeni hiyo imeambatana na zawadi mbalimbali kwa washindi 20.
Amesema kati ya washindi hao, wateja 10 watapata nafasi ya kwenda kushuhudia fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Marekani na Canada, ambapo washindi sita watasafiri kwenda Canada huku washindi wanne wakielekea Marekani.
Chahe alieleza kuwa Kombe la Dunia la mwaka huu litachezwa katika nchi tatu ambazo ni Marekani, Canada na Mexico, lakini benki hiyo kupitia kampeni yake imechagua kuwapeleka washindi katika nchi mbili pekee — Marekani na Canada.
“Mwezi uliopita tuliendesha droo ambapo tulipata washindi wanne wa safari ya kwenda Marekani kushuhudia fainali za Kombe la Dunia. Pia tulipata washindi watatu waliojishindia televisheni za inchi 85,” amesema Chahe.
Amefafanua kuwa zawadi za televisheni zimewekwa mahsusi kwa wateja waliotumia vizuri kadi zao za TemboCard lakini hawakubahatika kushinda safari ya kwenda kushuhudia fainali hizo moja kwa moja uwanjani.
“Mbali na televisheni hizo, washindi pia wanapatiwa king’amuzi pamoja na kifurushi kitakachowawezesha kufuatilia michezo hiyo moja kwa moja wakiwa majumbani mwao,” ameongeza.
Kwa mujibu wa Chahe, leo benki hiyo imeingia katika awamu ya pili ya droo hiyo ambapo washindi watatu wamejishindia safari ya kwenda Canada huku wengine watatu wakijishindia televisheni kubwa.
Aidha, amesema sambamba na droo hiyo, benki hiyo pia imekabidhi zawadi za televisheni za inchi 85 kwa washindi wa droo iliyopita.
Chahe amesema kampeni hiyo itaendelea mwezi ujao kwa ajili ya kupata washindi wengine watatu watakaosafiri kwenda Canada pamoja na washindi wanne watakaojishindia televisheni kubwa.




No comments:
Post a Comment