NA MWANDISHI WETU
TAASISI za NMB Foundation na Mercy Corps, zimesaini Makubaliano ya Utekelezaji wa Mradi (MoU) wa Evolve, wenye thamani ya Sh. Bilioni 2.6, unaolenga kuchochea ustawi na ukuaji wa Sekta ya Usafirishaji kwa Vyombo vya Moto Vinavyotumia Umeme ‘E-Mobility’ jijiji Dar es Salaam.
Makubaliano hayo ya ushirikiano wa miaka miwili, yamesainiwa Dar es Salaam Ijumaa Julai 31, yakishuhudiwa na wawezeshaji wa mradi huo, ambao ni Umoja wa Ulaya (EU) na Shirika la Maendeleo la Ubelgiji Enabel, iliyowakilishwa na Mkurugenzi Mkazi wa Enabel Tanzania, Virginie Hallet.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini na uzinduzi wa Evolve, Meneja Mkuu wa NMB Foundation, Nelson Karumuna, alisema mradi huo utawagusa moja kwa moja wanawake na vijana walioko katika mnyororo mzima wa Sekta ya Usafirishaji ya ‘E-Mobility.’
“Ni siku ya kihistoria, tukisaini makubaliano ya utekelezaji wa mradi wa kwanza kabisa nchini wa Evolve, wanufaika wakiwa ni wanawake na vijana waliomo katika mnyororo wa ‘E-Mobility’ wanaoendesha biashara jijini Dar es Salaam, pamoja na wadau wake wakiwemo watengenezaji vifaa kama chaja.
“Makubaliano haya yatafanya kazi Dar es Salaam kwa kipindi cha miaka miwili, tutazifikia biashara zaidi ya 25, ambapo mradi huu pia utatoa Elimu ya Biashara na Elimu ya Ujasiriamali kwa wadau wa ‘E-Mobility’ kwa miaka miwili, alafu tutaangalia uhitaji wa mikoa na majiji mengine.
“Pamoja nasi, tutashirikiana na Benki ya NMB, ambayo iko hapa kama mwezeshaji katika kuchochea ukuaji na uwekezaji wa E-Mobility. NMB Foundation tunaamini Evolve unaenda kuwa wa mfano nchini, utasaidia kuleta wadau wengine kuinyanyua sekta hiyo muhimu kiuchumi.
“Tunasema ni muhimu, kwa sababu unachangia pakubwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050, kwani utaweza kufikia zaidi ya zile biashara tulizopanga kuzifikia katika awamu hii ya kwanza ya mradi huu wa kwanza kabisa kugusa biashara za Vyombo vya Moto Vinavyotumia Umeme,” alisema.
Kwa upande wake, Anthony Salota, ambaye ni Mratibu wa Mercy Corps Tanzania, ambao ni watekekelezaji wakuu wa mradi huo, alisema wanajivunia sana kuwa sehemu ya mapinduzi chanya yanayoenda kuletwa na Evolve, mradi unaofadhiliwa na EU kupitia Taasisi ya Maendeleo ya Ubelgiji Enabel.
Alibainisha kuwa, lengo la mradi huo ni kufanya uwezeshaji kwa wafanyabiashara waliomo katika ‘E-Mobility,’ unaoenda kuwa kichocheo cha ustawi na ukuaji wa wadau wenye mawazo yanayokosa mtaji na wafanyabiashara wanaoendesha biashara zao katika sekta hiyo, lakini wanapata ugumu katika uendeshaji.
“Tutapokea Mawazo na kuyachakata kuona yanayostahili kupewa uwezeshaji wa mitaji, ambayo sasa itatolewa kwao, lakini pia tutawagusa wale ambao wameshaanza lakini wanapata ugumu kumudu ushindani kutokana na ufinyu wa mitaji na changamoto nyinginezo. Wao watapata pia msaada wa kifedha kutoka NMB.
“Leo tulikuwa tunafanya uzinduzi rasmi na kusaini makubaliano na NMB Foundation, huku tukishuhudiwa na Mwezeshaji Mkuu (Europian Union) na Enabel. Ni siku muhimu sana kwetu sisi Mercy Corp, tunataka kuona jinsi tutavyochangia ukuaji wa 'E-Mobility,” alisema Salota na kuongeza:
“E-Mobility’ ni sekta muhimu mno kwa sasa, jitihada kibao nchini zinafanyika kuleta Suluhu ya changamoto zinazokwaza ustawi wa Sekta ya Usafirishaji nchini, ndio maana tunaamini kwamba kama itafanikiwa, maana yake Evolve itapunguza au kuachana na matumizi ya petroli kwenye usafiri wa umma.”
Naye Mkurugenzi Mkazi wa Enabel Tanzania, Virginie Hallet, alisema kupitia mradi huo, wanaamini watawasaidia wajasiriamali wa ‘E-Mobility' na miundombinu yake ikiwemo vituo vya kuchajia na kwamba majukumu yao makuu yatakuwa ni pamoja na kusaidia utengenezaji wa ‘business model.’
“Tutakuwa tunasaidia kupata ruzuku na mikopo kwa wasafirishaji itakayotolewa na NMB Foundation kupitia NMB Bank, lengo ni kuwawezesha kufanya biashara zao kwa tija kupitia uwezeshaji huo ambao huenda wasingeweza kufanya kama wasingeupata.
“Kuna fedha zimetoka EU kupitia Enabel, lakini pia na NMB Foundation na Mercy Corps, ambapo tunalenga kuwasaidia wajasiriamali wenye Mawazo wapatao 15 na wafanyabiashara ambao tayari wameianza biashara hii takribani wanane jijini Dar es Salaam,” alibainisha Giki.

.jpeg)


No comments:
Post a Comment