September 16, 2026

CRDB YAIGUSA SEKTA YA ELIMU KIGAMBONI

 Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam


MKUU wa Wilaya ya Kigamboni, Dalmia Mikaya, amesema upatikanaji wa madawati katika shule za msingi na sekondari ni muhimu katika kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira bora na rafiki.


Amesema hayo wakati Benki ya CRDB kupitia CRDB Bank Foundation ilipokabidhi madawati yenye thamani ya Sh milioni 10 kwa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni kwa ajili ya kusaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia.



Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Wilaya, baadhi ya shule katika wilaya hiyo bado zinakabiliwa na upungufu wa madawati, hali inayosababisha baadhi ya wanafunzi kukaa chini wakati wa masomo.


Ameipongeza CRDB kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha sekta ya elimu na kuwataka kuendelea na misaada hiyo katika maeneo mengine yenye mahitaji.


“Tunawashukuru sana CRDB kwa kutuunga mkono na kutuletea madawati. Hili ni jambo kubwa sana kwetu kama Serikali,” amesema.


Aidha, ameeleza kuwa pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuboresha elimu, bado kuna mahitaji mbalimbali ya miundombinu na vitendea kazi shuleni.


Amesema Kigamboni inatarajia kuwa na ongezeko la mahitaji ya madawati kutokana na wanafunzi wa madarasa ya sita na saba kuhitimu kwa pamoja mwakani, hivyo ameiomba CRDB na wadau wengine kuendelea kushirikiana na Serikali.



Kwa upande wake, Meneja wa Kanda ya Dar es Salaam wa CRDB, Muhumuliza Buberwa, amesema benki hiyo imekabidhi madawati hayo kupitia CRDB Bank Foundation ikiwa ni sehemu ya utaratibu wake wa kurudisha kwa jamii sehemu ya thamani inayotokana na shughuli zake.



Amesema madawati hayo yenye thamani ya Sh milioni 10 yatagawiwa katika shule za msingi na sekondari za Kigamboni kwa lengo la kuunga mkono juhudi za kuboresha elimu.


“Benki yetu ina utaratibu wa kurudisha kwa jamii na leo tupo Kigamboni kuunga mkono sekta ya elimu. Tunaamini madawati haya pamoja na viti vitasaidia kuboresha mazingira ya wanafunzi,” amesema Buberwa.


Amesema CRDB itaendelea kutekeleza miradi ya kijamii katika mikoa mbalimbali nchini ili kuwafikia Watanzania na wateja wake.

No comments:

Post a Comment

Pages

▼