January 15, 2013

HATIMAYE OKWI AUZWA TUNISIA


DAR ES SALAAM, Tanzania

BAADA ya sintofahamu ya muda mrefu iliyokuwa imewakumba wapenzi na mashabiki wa mabingwa wa soka Tanzania, Simba, juu ya nyota wao wa kimataifa, Mganda Emmanuel Okwi, hatimaye imebainika amepigwa bei katika klabu ya Etolile du Sahel ya Tunisia.

Okwi ameuzwa dola 300,000 za Marekani kwa klabu hiyo, ambako dili hilo lilikamilika leo mchana huko Tunisia, ambako alikwenda kwa majaribio ya kujiunga na klabu hiyo kongwe nchini humo.

Hivi karibuni, viongozi wa Simba walikaririwa kwa nyakati tofauti wakidai kwamba, Okwi ameshindwa kuungana na wenzake kutokana na kwenda nchini Tunisia kwa majaribio katika klabu ya Esperance, kabla ya baadaye kugeuka na kudai kuwa yupo Etoile du Sahel.

Okwi, amekuwa na historia ya kuumiza vichwa vya viongozi na mashabiki wa Simba mara kwa mara, kutokana na kushindwa kujiunga kwa wakati na timu hiyo kila alipokwenda kwao kwa mapumziko.

Hivi karibuni, Okwi alishindwa kuungana na kikosi cha Simba kilichopo nchini Oman kwa kambi maalumu, huku viongozi wakitangaza kumtema rasmi kwenye ziara hiyo na kumuadhibu kutokana na kuchelewa kwake.

Hivyo kwa habari hizo, ni wazi sasa Simba imemaliza biashara na mshambuliaji huyo mahiri.

Viongozi wa juu wa Simba walipotafutwa kwa simu jana kuzungumzia hilo, Mwenyekiti Ismail Aden Rage simu yake haikuwa hewani, huku Makamu wake Geofrey Nyange ‘Kaburu’ na Katibu Evodius Mtawala zilikuwa zikiita bila kupokelewa.

Katika hatua nyingine, Simba ambayko imepiga kambi Muscat, Oman, leo inashuka kwenye Uwanja wa Qaboos Sports Complex, kukwaana na timu ya taifa ya huko iliyoshiriki michuano ya Olimpiki.

Mbali na mchezo huo, Simba inatarajiwa kucheza mechi nyingine za kirafiki na timu za Fanja FC na timu ya jeshi kabla ya kurejea nchini Januari 23.

No comments:

Post a Comment

Pages