January 02, 2013

MNYAMA CHUI AZIMA KELELE ZA TEMBO MTOTO


Na Elizabeth John
BONDIA Fadhil Awadhi ‘Mnyama Chui’ amefanikiwa kukata ngebe za Yohana Mathayo ‘Tembo mtoto’ kwa kumtwanga kwa KO katika raundi ya nne ya mchezo huo uliofanyika katika ukumbi wa Texas Manzese jijini Dar es Salaaam.

Mchezo huo ulifanyika juzi ulikuwa na upinzani mkubwa ulianza kwa kila mmoja kucheza kwa kujihami huku Tembo Mtoto alikuwa akirusha makonde mazito kwa kushtukiza lakini umahiri wa Mnyama Chui ulifanya kuhimili mikikimkiki hiyo.

 Mnyama Chui aliweza kuhimili makonde hayo mazito lakini muda mwingi alionekana kumkabili vema mpinzani wake kwa kumrushia makonde yaliyofanya katika raundi ya nne Tembo Mtoto kunyanyua mikono juu kuashiria kusitisha kuendelea na pambano hilo.

Mwamuzi wa pambano hilo, Emmanuel Mlundwa baada ya kuona Tembo Mtoto kusalimu amri alimtangaza Mnyama Chui kuwa mshindi wa poambano hili lililokuwa na upinzani wa aina yake hali iliyofanya kuvuta hisia za wadau wengi wa mchezo huo Mkoa wa Dar es Salaam.

Pambano hilo lililokuwa chini ya usimamizi wa Shirikisho la Ngumi za  Kulipwa Tanzania (PST) lilitanguliwa na mapambano mengine ya utangulizi ambapo Adam Yahya alimpiga kwa tabu Good Silver kwa point 39 kwa 37.

Rashid Chidox alimkata ngebe Bonny Gude kwa KO katika raundi ya pili, Habibu  Pengo alitandikwa na Roja Zengo kwa KO kwenye raundi ya kwanza, Fabian Lymo ‘Lampard’ alimkung’uta Hassan Mmanga kwa KO katika raundi ya tatu.  

No comments:

Post a Comment

Pages