January 15, 2013

MOURINHO: MADRID VS MAN UTD NI MECHI AMBAYO DUNIA INATAKA KUIONA MANCHESTER, England


MADRID, Hispania 
“Hii ni mechi ambayo dunia nzima inataka kuitazama. Real Madrid dhidi ya Manchester United. Sir Alex Ferguson dhidi ya rafiki yake Mourinho Haibu pekee kwa mechi hiyo ni ukweli kwamba sio fainali”

JOSE Mourinho anayeinoa klabu ya Real Madrid, amezitaja mechi mbili baina ya klabu yake na Manchester United za mtoano wa 16 bora, Ligi ya Mabingwa Ulaya, kuwa ni aina ya mechi ambazo “Dunia inataka kuziangalia.”

Mourinho aliyasema hayo jana kwenye Uwanja wa Old Trafford jijini hapa, alipokuja kuangalia pambano la mahasimu wa soka la England Man United dhidi ya Liverpool, akitumia nafasi hiyo kuisoma United anayocheza nayo Februari 13 jijini Madrid.

Na Mreno huyo maarufu kwa jina la ‘Special One’ alisema: “Hii ni mechi ambayo dunia nzima inataka kuitazama. Real Madrid dhidi ya Manchester United. Sir Alex Ferguson dhidi ya rafiki yake Mourinho.

“Haibu pekee kwa mechi hiyo ni ukweli kwamba sio fainali.”

Mourinho, aliye katika jaribio la kuipa Madrid ubingwa wa 10 wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, aliongeza: “Tunajua kwamba tunaweza kuwafunga. Tunajua pia kwamba wanaweza kutufunga – lakini kimsingi tuko tayari kwa mechi dhidi yao.”

Special One akaenda mbali zaidi na kusema anaamini Madrid, inayoongozwa na nyota wa zamani wa United, Cristiano Ronaldo, ina nafasi kubwa ya kusonga kutokana na kutokea katika ‘Kundi la Kifo’.

Akasema: “Kulikuwa na makundi dhaifu ambayo uliyepangwa ulikuwa unajua kabisa kwamba unaenda kushika nafasi ya kwanza ama ya pili baada tu ya mechi mbili ama tatu.

“Lakini katika kundi letu, kulikuwa na timu tatu bora kabisa katika michuano hii – ambazo ni Borussia Dortmund, Manchester City na sisi wenyewe. Sasa tumepata mpibnzani mgumu zaidi katika hatua hiyo ya mtoano wa 16 Bora – Man United.”

No comments:

Post a Comment

Pages