January 08, 2013

PEP GUARDIOLA: LETENI OFA, NAREJEA RASMI

NEW YORK, Marekani

“Ndiyo, msimu ujao natarajia kurejea rasmi kuingoza klabu kama kocha. Sijui nitakuwa nafanya kazi na timu gani, lakini natarajia kurejea rasmi kazini”

KOCHA wa zamani wa FC Barcelona ya Hispania, Pep Guardiola amefungua milango kwa klabu za soka za Ligi Kuu ya England kwa kudai kuwa: Natarajia kurejea rasmi katika soka msimu ujao.

Na kauli hii ya kocha huyo aneyesakwa zaidi duniani kwa sasa, imetajwa kama ashirio la wazi ya kuzifungulia milango klabu za England zinazosaka saini yake za Chelsea, Manchester City, Manchester United na Arsenal.
Guardiola, aliye mapumziko kwa mwaka mmoja baada ya kukataa kurefusha mkataba wake Barcelona, alisema: “Ndiyo, msimu ujao natarajia kurejea rasmi kuingoza klabu kama kocha. Sijui nitakuwa nafanya kazi na timu gani, lakini natarajia kurejea rasmi kazini.”

Guardiola, ambaye anatarajia kutimiza miaka 42 ya kuzaliwa kwake wiki ijayo, aliongeza: “Natarajia kurudi kazini, kwa sababu mimi bado kijana. Niko vizuri sasa, naangalia mpira kama shabiki na nafurahia kuona wachezaji mahiri.”

Inaeleweka kuwa kipaumbele cha Guardiola kwa sasa anapofikiria marejeo yake katika soka ni kufanya kazi na klabu za Ligi Kuu ya England.

Mmiliki wa klabu ya Chelsea, bilionea Roman Abramovich hajaficha tama zake za kumpa mikoba Guardiola, huku majaaliwa ya Mtaliano Roberto Mancini huko Etihad yaliko makazi ya Man City yakiwa shakani.

Mkurugenzi mpya wa soka wa Man City, Txiki Beguiristain, aliwahi kufanya kazi na Guardiola wakati akiwa anainoa FC Barcelona.

Alex Ferguson hivi karibuni alibainisha nia ya kubaki akiinoa Man United kwa miaka miwili ijayo – lakini imeelezwa mapenzi na nia ya dhati ya kumuachia kiti hicho Guardiola, chagua namba moja Old Trafford, inaweza kubadili mawazo ya Mskochi huyo.

Wakati huo huo, Arsenal inaweza kuratibu jaribio la kufanya kazi na Guardiola kama mbadala wa Arsene Wenger, iwapo ataamua kutimka klabuni hapo baada ya miaka 17.

Guardiola aliifundisha Barca kwa mafanikio makubwa, akitwaa mataji 14 katika miaka minne ya uwapo wake Nou Camp yaliko makazi ya vinara hao wa Lal Liga.

No comments:

Post a Comment

Pages