January 08, 2013

RAIS WA TOGO AMREJESHA EMMANUEL ADEBAYOR KIKOSINI


LOME, Togo

TOGO imethibitisha kuwa mshambuliaji na nahodha wa timu ya taifa ya nchi hiyo, Emmanuel Adebayor amebadili msimamo wake wa awali na sasa atakuwa sehemu ya nyota wa nchi hiyo wakaocheza fainali za Mataifa Afrika baadaye mwezi huu.

Adebayor, 28, nyota anayekipiga na klabu ya Tottenham, awali alikana kushiriki fainali hizo zinazoanza Januari 19 huko nchini Afrika Kusini, lakini mazungumzo yake na Rais wa Togo yamembadili msimamo.

Taarifa juu ya habari hii zimeongeza kuwa, mshambuliaji huyo ataungana na kikosi chake nchini Ghana, ambako kutakuwa na kambi fupi ya maandalizi ya mwisho mwisho ya timu hiyo maarufu kama ‘Hawks.’

Rais wa Shirikisho la Soka la Togo, Ameyi Gabriel, alisema: “Bila shaka tutakuwa katika michuano ya Mtaifa Afrika tukiwa na Adebayor, tutakuwa sote pamoja nchini Afrika Kusini.

“Ni jambo muhimu mno kwamba tutakuwa huko tukiwa naye kikosini, kwa sababu yeye ni mchezaji wetu na ni nahodha wa timu.”

Ingawa Adebayor ameifungia Spurs mabao matatu tu mwaka huu, uamuzi huu umetajwa kuweza kuiathiri klabu hiyo ya jijini London, ambayo itapaswa kumtegemea mshambuliaji Jermain Defoe pekee.

Kama Togo itaweza kutinga fainali za michuano hii, Adebayor anatarajia atakosa mechi nne za Tottenham, lakini anaweza kurejea mapema kupigania klabu yake kwa sababu kikosi chake kimepangwa kundi la kifo pamoja na Ivory Coast, Tunisia na Algeria.

No comments:

Post a Comment

Pages