January 08, 2013

CAF YATAJA WAAMUZI WA AFCON 2013 AFRIKA KUSINI

JOHANNESBURG, Afrika Kusini

Waamuzi wote 18 na wasaidizi hao 21 waliotangazwa na CAF, wametakiwa kuwasili jijini Johannesburg, Afrika Kusini hapo Januari 15 kwa ajili ya mitihani yao ‘pre-tournament tests,’ kabla ya kuelekea Irene Lodge jijini Pretoria

SHIRIKISHO la Soka barani Afrika (CAF) limetangaza waamuzi 18 na washika vibendera 21 kuchezesha mechi za michuano ya Mataifa Afrika 2013, wakiwamo wawili raia wa Afrika Kusini, ambao ni Daniel Bennett na Zakhele Siwela.

Mabadiliko mawili ya waamuzi wapya na wasaidizi wao yamefanyika kwa kuongeza waamuzi wapya katika kundi la waliochezesha fainali zilizopita za AFCON zuilizopigwa katika mataifa mawili ya Equatorial Guinea na Gabon mwaka jana.

Orodha hiyo ya Caf inajumuisha waamuzi wawili waliochezesha mechi mbili za fainali zilizopita, ambao ni Komlan Coulibaly wa Malia (2010 - Angola) na Msenegali Badara Diatta (pichani kulia) wa fainali ya mwaka jana kati ya Zambia na Ivory Coast jijini Libreville.

Coulibaly, 42, anatarajia kuweka rekodi wakati atakapokuwa akicjhezesha fainali hizo za Afrika Kusini zinazotarajia kuanza Januari 19. Hii itakuwa michuano yake ya saba tangu alipoitwa kuchezesha katika fainali zake za kwanza mwaka 2002.

Waamuzi wawili wapya miongoni mwa waliotajwa wametokea nchi za Kenya – Sylvester Kirwa, na Bernard Camille wa Shelisheli, huku nchi za Algeria na Senegal zikitoa waamuzi wengi zaidi – watatu kila moja.

Mohamed Benouza wa Algeria hizi zitakuwa fainali zake za tano za Mataifa Afrika, kama ilivyo pia kwa Diatta, aliyetajwa kuchezeasha fainali zote tangu alipoitwa kwa mara ya kwanza mwaka 2006.

AFCON 2013, zitakuwa fainali za tatu kwa Bennett na za pili kwa Siwela waamuzi wa taifa taifa mwenyeji, ambao watakuwamo pia katika fainali zijazo za Kombe la Dunia hapo mwakani nchini Brazil.

Waamuzi wote 18 na wasaidizi hao 21 waliotangazwa na CAF, wametakiwa kuwasili jijini Johannesburg, Afrika Kusini hapo Januari 15 kwa ajili ya mitihani yao ‘pre-tournament tests,’ kabla ya kuelekea Irene Lodge jijini Pretoria.

No comments:

Post a Comment

Pages