January 02, 2013

SERGIO AGUERO AZUA WASIWASI MANCHESTER CITY


MANCHESTER, England

"Tuna uhakika ya yeye kukosa pambano la Jumamosi dhidi ya Watford, lakini pia uzoefu wangu unanipa shaka ya kuweza kuiwahi mechi dhidi ya Arsenal. Lakini kuna viwango tofauti vya maumivu ya misuli, ndio maana tunahitaji kujua hilo baada ya saa 48"
 
WAKATI Manchester City ikijiandaa kupungukiwa nguvu kwa nyota wake Yaya na Kolo Toure kutarajia kujiunga na timu ya taifa itakayoshiriki fainali za Mataifa Afrika (AFCON 2013), imepata pigo kwa mshambuliaji wake Sergio Aguero (Pichani juu) kuumia.

Aguero nyota wa kimataifa wa Argentina, alipata majeraha na ameripotiwa kuwa na uwezekano wa kukaa nje ya kikosi kwa wiki mbili hadi tatu, baada ya kuumia misuli wakati mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu wakishinda 3-0 dhidi ya Stoke City Jumanne jioni.

Mkali huyo alilazimika kutolewa nje ya dimba baada ya kufunga mkwaju wake wa penati katika dakika ya 74, kukinyanyua juu kikosi cha Roberto Mancini kilichopata ushindi huo muhimu.

Man City ilikuwa na matarajio ya kumkosa Aguero katika kipindi cha wiki moja, lakini msaidizi wa Mancini, David Platt amedokeza kuwa nyota huyo hatukuwapo dimbani kwa muda, akitarajia kulikosa pambano la raundi ya tatu ya Kombe la FA dhidi ya Watford Jumamosi.

Aguero, ambaye alikuwa mfungaji bora wa Man City msimu uliopita, akikumbukwa kwa bao la dakika za lala salama dhidi ya QPR lililoipa ubingwa wa Ligi Kuu, pia atalikosa pambano kali na la kukata na shoka dhidi ya Arsenal hapo Januari 13.

"Kwa sasa ni vigumu kutathmini kiwango gani Aguero ameumia na atakuwa nje ya dimba kwa muda gani," alisema Platt.

"Tuna uhakika ya yeye kukosa pambano la Jumamosi dhidi ya Watford, lakini pia uzoefu wangu unanipa shaka ya kuweza kuiwahi mechi dhidi ya Arsenal. Lakini kuna viwango tofauti vya maumivu ya misuli, ndio maana tunahitaji kujua hilo baada ya saa 48.

"Kuna aina nyingi za maumivu ya misuli nah ii hatujaijua hadi vipimo ambavyo ndivyo tunasubiri.

"Kumekuwa na aina kibao za majeruhi zikiwamo za kuvimba na ile ya kutokwa na damu kwa ndani. Hatujui hii ni ya aina ipi na utamchukua muda gani," alimaliza Platt.

Kuumia kwa Aguero na kuondoka kwa familia ya Toure kunazua shaka katika kikosi cha Man City, ambacho kwa sasa kiko nyuma kwa pointi saba katika jaribio la kutetea ubingwa wao, ulio hatarini kuporwa na vinara Manchester United.

No comments:

Post a Comment

Pages